Menu
in , , ,

Uraia wa Bernard Morrison unawagusa wengi

Bernard Morrison

Bernard Morrison

Dunia inakwenda kwa kasi, Tanzania haipo kisiwani. Mataifa yanahaha kuchukua wachezaji mbalimbali na kuwashawishi wachezee nchi zao…

ZIPO taarifa kuwa Bernard Morrison anatamani kuchukua uraia wa Tanzania na kusakata kabumbu akiwa anapeperusha bendera ya nchi yetu. Inadaiwa kuwa Morrison tangu mwaka 2021 amekuwa akihitaji kuchukua uraia wa Tanzania na kutinga jezi za Taifa Stars.  Huu ni uamuzi mzito kwake binafsi, lakini kimichezo ni mwepesi mno. Hali kadhalika ni uamuzi mwepesi sana kwa Tanzania kimichezo bila kubeba makapu ya visingizio. 

TANZANIASPORTS imewahi kueleza kwa kina juu ya matamanio ya kuwaona  wa kigeni ambao hawana matumaini ya kuchezea nchi zao, lakini wana uwezo mzuri kisoka na kutoa mchango kwa kwa soka la Tanzania. Kwamba wapo wachezaji wa kigeni ambao vipaji na uwezo wao ni mzuri lakini hawawezi kuitwa kuchezea timu zao za Taifa kwa vile kuna rundo la wachezaji wengine wanaocheza nje au ndani. 

Kwa mfano kocha wa Brazil hawezi kumwita kikosini Bruno Gomes wa Singida Fountain Gate F.C wala Bernard Morrison hana nafasi katika kikosi cha Black Stars cha Ghana. Hali kadhalika wapo nyota wengine ambao wana viwango vizuri na wanaweza kushawishiwa kuchukua uraia wa Tanzania kutoa mchango kimichezo. 

Dunia inakwenda kwa kasi, Tanzania haipo kisiwani. Mataifa yanahaha kuchukua wachezaji mbalimbali na kuwashawishi wachezee nchi zao. Bukayo Saka wazazi wake wanatoka Nigeria, na wapo ndugu wa Xhaka wanaocheza mataifa mawili tofauti. 

Pengine swali la kuuliza je kuwachukua wachezaji wa kigeni kuwapa uraia kigezo cha vipaji vyao vya soka ni kupuuza vya wazawa? Jibu ni hapana, kwa sababu suala hili si geni duniani wachezaji kubadilisha uraia kwa kigezo cha mpira wa miguu. Hoja ya msingi ni uwezo wa mchezaji anayepewa uraia huo na matarajio ya Taifa. 

Shirikisho la soka TFF linatakiwa kutoa mchango mkubwa wa ushawishi pale inapohitajika wachezaji wa kupewa uraia. Kibu Dennis ni nyota ambaye alipewa uraia mara baada ya kujiunga na Simba, na sasa klabu na Taifa vinanufaika kwa kipaji chake. Hakuna la ajabu, bali msingi ni kipaji cha nyota husika. 

Wengi wanaumbuka namna Wabrazil wanavyozagaa katika mataifa mengine ambako wanapewa uraia. Qatar walikuwa wenyeji wa Fainali za Kombe la dunia mwaka 2022 na wengi wameona kikosi chao kinaundwa na wachezaji weusi ambao wana uraia wa huko. Miongoni mwao alikuwa mtoto wa Hassan Afif ambaye alikuwa tegemeo la Qatar. 

Hivyo unaona hata Qatar haikujiuliza mara mbili kumpa uraia mtoto wa Hassan Afif ambaye pia hutembelea  ndugu zake wa Tanzania. Hata kama mtoto huyo anao uraia wa kuzaliwa huko au la lakini ukweli unabaki Taifa letu haliwezi kusema linaishi kisiwani, kwamba lijitegemee kila kitu wakati fursa zipo. 

Chukulia kuitwa kwa Pape Ousmane Sakho ni kumtengenezea ‘CV’ yake pale fursa ya kucheza mataifa ya ulaya itakapotokea. Hii ina maana hata kama asingeliitwa bado imani ya kuwa nyota huyo anaweza kutoa mchango kwa Taifa Stars ilipaswa kubaki vilevile kama ilivyo kwa wengine. 

Nyakati za sasa mataifa yameacha kujinyima fursa ya vipaji kutoka kwingine kuchezea timu zao za Taifa. Wachezaji kutoka Cameroon, Senegal,Nigeria,Ghana,Mali na mengine wamekuwa wakigombewa kupewa uraia kwenye nchi zingine. Hata Australia, Uswisi,Sweden na mengine yaliyozoeleka kutapakaa wazungu, lakini sasa wameaza kunyemelea fursa ya wachezaji wa kigeni. 

Wafaransa kwao kuwapa uraia nyota wa kigeni sio suala la kufikiria mara mbili ikiwa wana vipaji vikubwa vya kusakata kandanda. Kwa kili ya Ufaransa unaweza kuona namna wanavyochukulia mafanikio ya nchi kwa umoja bila kujali rangi ya wachezaji wao au ubaguzi unaorindima viwanjani. Kwao sifa ya taifa kwanza, na wale wanaowakilisha wanatambulika kuwa wafaransa. Ndio maana kwenye michezo kuna utani unasema Ufaransa ni Taifa la Kiafrika kwa vile wengi wa wachezaji wake wametoka nje ya nchi hiyo. 

Kwa msingi huo akina Bernard Morrison na wengine wa kigeni wanaotaka au tukitaka kuwachukua litakuwa jambo la kawaida na hoja itakuwa imemama katika uwezo wao wa kusakata kandanda. Kigezo hicho kitawapa nafasi wengine kulitumia taifa letu kusaka fursa ng’ambo na sifa itakuwa ya nchi bila kujali asili zao. Hata ujio wa Pellegrino na wengine kwenye kikosi cha Taifa Stars kwenye mchezo uliopita dhidi ya Niger ni jambo la kufurahisha kuwa mvuto unaweza kusukwa kwa kukaribisha nyota wengine kutoa mchango wa nchi.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version