Date::8/6/2008 |
Umoja wa Mataifa waagiza miji itenge viwanja vya michezo |
Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la makazi la Umoja wa Matifa (UN-HABITAT), Anna Tibaijuka amezitaka nchi zinazoendelea kutenga maeneo ya viwanja vya michezo kwa kuwa ni muhimu kwa makazi ya binadamu. Wito huo ameutoa katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na shirika hilo kuhusiana na na ziara yake nchini China atakaposhiriki ufunguzi wa michezo ya Olimpiki na kufafanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo kuhusiana na ongezeko la haraka lwa watu katika miji ya nchi hiyo. Tibaijuka, ambaye alishiriki kukimbiza mwenge wa Olimpiki ulipopita jijini Dar es Dalaam, pamoja na mambo mengine atakuwa na mazungumzo ya maandalizi ya mkutano mkuu wa makazi duniani utakaofanyika katika Jiji la Nanjing, nchini humo kati ya Novemba 3 na 6, mwaka huu. Alisema michezo ina nafasi muhimu katika maendeleo ya makazi, na michezo yote kama ilivyo hiyo ya Olimpiki inafanyika mijini penye watu wengi, hivyo mipangilio ya miji inatakiwa kutenga maeneo ya michezo kwa ajili ya wakazi wake. “Hata hivyo, katika miji na majiji mengi katika nchi zinazoendelea, jamii zinanyimwa viwanja vya michezo, na watoto katika maeneo yasiyopimwa hulazimika kuchezea katika njia chafu kwa kukosa maeneo ya kuchezea,” alisisitiza na kuongeza kuwa IOC inapenda kufanya kazi na UN-Habitat katika eneo hilo muhimu. Akizungumzia mwaliko wake, Tibaijuka alisema: “Rais wa Kamati ya Olimpiki Kimataifa (IOC) alinialika kushiriki ufunguzi na ufungaji wa mashindano hayo kwa kuzingatia umuhimu wa masuala ya makazi na miji endelevu.” Akiwa nchini humo, siku ya mkesha wa ufunguzi wa michezo hiyo, Tibaijuka atahutubia Kamati ya Utendaji ya Kikunchi cha Michezo kwa Maendeleo (Sport for Development and Peace International Working Group) kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimichezo. |