Chelsea jana walipata ushindi wao wa kwanza wa EPL msimu huu. Waliwafunga West Bromwich 3-2 kwenye mchezo ambao Chelsea walifanya kazi ya ziada kujihakikishia alama tatu muhimu.
Waliruhusu mabao zaidi ya moja kwenye mchezo wa tatu mfululizo baada ya kutoa sare ya 2-2 kwenye mchezo wao wa kwanza dhidi ya Swansea City na kupokea kipigo cha 3-0 kutoka kwa Manchester City wikiendi iliyopita kwenye mchezo wao wa pili wa EPL msimu huu.
Ukuta wa Chelsea unaonyesha udahifu mkubwa msimu huu ukiwa tayari umesharuhusu mabao 7 kwenye mechi tatu tu. Haya ni mabao mengi kuliko timu yoyote ukiwatoa Sunderland ambao wameruhusu mabao 8 mbaka sasa.
Nahodha John Terry alijikuta akipata kadi nyekundu kwenye mchezo wa hapo jana. Ilikuwa ni kadi yake nyekundu ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka mitano. Mara ya mwisho alipoonyeshwa kadi nyekundu ilikuwa ni Aprili 2010 kwenye mchezo dhidi ya Tottenham. Atakosekana kikosini kwa mechi kadhaa zijazo akitumikia kifungo kwa kadi hii nyekundu.
Kocha Jose Mourinho anaonekana kutostushwa sana na hili. Anaonekana kuwa na amani baada ya kufanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza msimu huu. Hajali chochote kuhusu kukosekana kwa Terry kwenye michezo kadhaa ijayo ya Chelsea.
Baada ya mchezo wa hapo jana alipoulizwa iwapo angekata rufaa juu ya kadi nyekundu ya Terry Mourinho alisema kuwa kukata rufaa ni kupoteza muda. Alisema kuwa huko ni kupoteza muda kwa kuwa hadhani kwamba wanaweza kufanikiwa kwa kuwa ni mara nyingi mno rufaa zao zimekuwa zikikataliwa. Nafikiri haoni umuhimu wa John Terry kwa sasa. Anachokitazama ni kutafuta mbadala wa mlinzi huyu.
Mourinho anatazamiwa kuendelea na mpango wake wa kuhakikisha anamvuta darajani beki kisiki wa Everton John Stones. Sidhani kwamba Mourinho atakubali kushindwa kumtwaa beki huyu kwa kuwa anaonekana ameshapoteza imani na John Terry ambaye wiki iliyopita alimtoa uwanjani kwa mara ya kwanza tangu aanze kuinoa Chelsea kwenye mchezo dhidi ya Manchester City.
Ujio wa John Stones ni swala lenye umuhimu mno kwa Chelsea ili kuimarisha safu yake ya ulinzi inayolegalega. Natarajia watamtwaa mlinzi huyu kabla ya dirisha la usajili kufungwa kwa gharama yoyote ile ili kuweka matumaini ya kutetea ubingwa wao.
Stones atakapotua Chelsea ni wazi kuwa ni lazima apate nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Mourinho ambaye amekuwa akimuwania mlinzi huyu kwa muda mrefu sasa. Je atachukua nafasi ya nani kati ya Terry na Cahill? Hawezi kuwa Garry Cahill. John Terry ni lazima atampisha kijana huyu kwenye kikosi cha kwanza.
Terry amekuwemo kwenye kikosi cha Chelsea kwa miaka 17 sasa akicheza michezo zaidi ya 460 na kushinda makombe 16 yakiwemo manne ya EPL na 1 la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa mlinzi tegemeo na nahodha wa timu hii.
Msimu uliopita pekee Terry aliichezea Chelsea takriban michezo 30 kati ya 38 ya EPL. Alitoa mchango mkubwa mno kwenye safu ya ulinzi ya Chelsea ambayo iliruhusu mabao machache kuliko timu nyigine yoyote.
Bado ana umuhimu mkubwa kama mchezaji na nahodha mwenye uzoefu ndani ya klabu ya Chelsea. Wachezaji kama John Stones wana mengi mno ya kujifunza kutoka kwake. Lakini ni wazi kuwa kwa anahitaji kupumzika. Hahitaji kucheza michezo mingi kama aliyocheza msimu uliopita na misimu ya nyuma. Umefika mwisho wa John Terry kama mlinzi muhimu kwenye michezo migumu na rahisi ya Chelsea.