HAKUNA siri kwamba idadi ya makocha wanaokea nchi za Ujerumani na Uholanzi wamekuwa na mafanikio zaidi katika vilabu vya England na pengine sehemu nyingine. Unapoajiri kocha yeyote jambo la kwanza ni kuhakikisha uwezo wake wa kujenga uhusiano na wachezaji pamoja na mbinu zake. Baadhi ya makocha wanaoajiriwa ni vijana na ambao wameonesha umahiri katika kazi yao.
Ligi ya Mabingwa ndani ya EPL
Unapozungumzia makocha wenye mafanikio ndani ya England mara nyingi majina yanayokuja yanatoka nje ya nchi hiyo. Si kwamba hapa England hakuna makocha bali mafaniukio yao ni madogo sana. unaweza kumtaja Sir Alex Ferguson kwa sababu anatokea Scotland ambayo ni sehemu ya Ufalme wa Uingereza. Lakini linapokuja suala la wazawa wa England hakuna hata kocha mmoja aliyewahi kutwaa Ligi ya Mabingwa. Angalia Sir Alex Ferguson alitwaa taji hilo akiwa kocha kutoka nje ya England. Thomas Tuchel aliyeipatia Chelsea taji la Ligi ya Mabingwa akiwa mgeni. Pep Guardiola amewapatia Manchester City taji la kwanza la Ligi ya Mabingwa akiwa raia wa nje. Rafa Benitez hali kadhalika aliwapa taji Liverpool akiwa kocha wan je. Jurgen Klopp naye amewapa taji Liverpool akiwa kocha wa kigeni. Orodha ni ndefu.
Taji la EPL
Makocha wa nchi za Ujerumani na Uhispania wamekuwa wakinyang’anyana taji hili kwa miaka mingi. Pep Guardiola amewaburuza wenzake kwa misimu mitano hadi saba sasa akiwa mwamba wa kunyakua taji hilo. Arsene Wenger aliweka rekodi ya kutofungwa akiwa na Arsenal katika kikosi kilichojulikana kama ‘Invicibles’ ni raia wa Ufaransa. Alex Ferguson alitamba nyakati zake kutwaa taji la EPL akiwa kocha wa kigeni.
Claudio Raineri alitwaa taji la EPL akiwa na Leicester City ni kocha wa kigeni raia wa Italia. Jose Mourinho alitwaa taji la EPL akitokea kwao Ureno na kuipa furaha Chelsea, sawa na Maurizio Sarri au maarufu kiama ‘Sarriball’ pamoja na Carlo Ancelotti alipokuwa Chelsea. Kwa kutumia mifano miachache hii unagundua kuwa makocha wazawa wa England hawajatanua mbawa zao kiasi cha kutosha badala yake wamekuwa wakishindania vilabu vingine visivyowania ubingwa.
‘Top Four’ EPL
Angalia timu zinazoshindana kileleni mwa Ligi Kuu England, makocha wake ni wageni. Manchester City wapo na Pep Guardiola. Liverpool wapo na Arne Slots, Arsenal wapo na Mikel Arteta,Unai Emery na kadhalika. Eddie Howe alijaribu kufurukuta mara kadhaa msimu uliopita lakini ndoto zake ziliishia kwenye ‘Top Four’ kisha msimu huu amekuwa wa kuhurumiwa kwa sababu Newcastle United haijaonesha makali kama ilivyokuwa awali.
Kimsingi nafasi nne za juu za Ligi Kuu England zinatawaliwa na makocha wageni, huku wazawa wakiwa kwenye timu zinahangaika kujinusuru kushyuka daraja. Ni ushahidi wa wazi kuwa wazawa hawafui dafu kwa wageni na zaidi wageni wenyewe wanatokea nchini mbili zenye shauku ya kufanikiwa kisoka.
Ujerumani na Uhispania
Jurgen Klopp, Fabian Hurzeler, Thomas Tuchel ni wawakilishi wazuri wa Ujerumani katika soka la England. Makocha hao wamefanya kazi kubwa na wametoa maarifa yaliyoleta ubingwa. Pep Guardiola, Mikel Arteta,XabI Alonso,Xavi,Rafa Benitez.
Kwa mfano kocha kinda mwenye umri wa miaka 31 Fabian Hurzeler raia wa Ujerumani ni miongoni wa wawakilishi wazuri kwenye kizazi cha makocha wa nchi hizo mbili. Kihistoria makocha wa ujerumani wanaosifika ni Jupp Heyneckes, Ottmar Hitzfeld,Sepp Herberger,Otto Rehhagel,Franz Beckenbauer,Udo Lattek, Joachim Low,Helmut Schion, Dettmar Cramer. Kwa Hispania makocha kama Luis Aragones, Vicente Del Bosque,Julen Lopetugui,Luis Enrique,
Makocha wa Uholanzi
Katika Ligi Kuu Hispania makocha wa Kiholanzi wamekuwa wakipata nafasi kubwa. Kuanzia wachezaji hadi makocha wamenufaishwa na kizazi kilichopita cha Johan Cruyff hadi akina Patrick Kulivert, Marc Overmas, Philip Cocu na wengineo. Arne Slots ni jina kubwa EPL msimu huu akitokea Feyernood, hali kadhalika ilivyokuwa na Louis van Gaal na baadaye Eric Ten Hag.
Ruud van Nistelrooy anaelekea kufuata nyayo za makocha hao sambamba na wenzake akina Ronald Koeman, Marco van Basten,Guus Hiddink,Rinus Michels,Frank Rijkaard, Dick Advocaat,Leo Beehakker,Bert van Marjwik. Hao ni miongoni mwa makocha gwiji wlaiotamba nyakati tofauti na kudhihirisha kuwa kizazi cha ukocha cha Uholanzi kimekuwa na urithi toka zamani. Hilo ni tofauti na makocha wa England ambao hawana rekodi za kuvutia katika vilabu vyao na soka la Kimataifa.
Mbinu za kiufundi
Kwanza makocha wa nchi hizo mbili wanatokana na falasafa yao ya soka. Uchezaji wa soka la Hispania umebadilishwa na makocha wawili Luis Aragones na Vicent Del Bosque, ingawaje nao wamenufaika na ujuzi wa John Cryuff aliyewaletea ‘Tikitaka’ kupitia La Masia ya Barcelona. Kwa aisli makocha wengi wa Kihispania wanatoka jimbo la Basque. Ni eneo ambalo kumekuwa na juhudi kubwa za vijana kupenda mchezo wa soka.
Makocha wanaotokea hapo ndiyo wengi wao wanaotamba barani Ulaya. Kiasili makocha hao hupendelea mfumo wa 4-3-3 au 3-4-3 ambao unawafanya wapige pasi nyingi na kutawala mchezo kwingi. Wanaamini falsafa yao ya kumiliki mpira na kugawa pasi kwa wingi ni silaha ya kumchosha mpinzani ambaye anatakiwa kufanya juuhudi kurudisha mpira. Katika mbinu hizo utakutana pia na ufundishaji wa Thomas Tuchel na Jurgen Klopp, hata Julian Nangelsman naye amekuwa akifuata mfumo huo. Mara nyingi ni mifumo inayowapa uhuru zaidi kuunda mashambulizi na aina ya wachezaji.
Unaajiri kocha gani?
Labda katika somo ambalo vilabu vya nyumbani Tanzania vinatakiwa kujifunza ni pale wanapotakiwa kujua wanaajiri kocha wa anamna gani. Kwao kocha yupi mwneye falsafa inayoendana naye anafaa kuwanoa. Ulimwengu unataka kuona kocha mwenye ujuzi na mbinu za aina fulani katika falsafa yake kuwa silaha muhimu ya kuajiriwa kwneye vilabu.
Ni muhimu kuwaambia viongozi wa vilabu vya mpira wa miguu Tanzania kuondokana na kasumba ya kutegemea makocha wa kutuma CV zao ili zisomwe na kuonwa kisha wafikiriwe kuajiriwa. Tubadilike, hatujachelewa.