Menu
in , , , ,

UMAARUFU WA MICHEZO UNA MAADILI , FAIDA NA MAJUKUMU

Mapema mwaka huu, Aliyekuwa Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga, Benno Njovu alikemea tabia ya baadhi ya wachezaji wetu kunywa pombe na kuvuta sigara. Tabia hiyo aliendelea Bwana Njovu, si nzuri maana huathiri afya zao na alihimiza kuwa wachezaji wengi wametokea darasa la saba na “wanashindwa kujitambua.”

Klabu iliwaadhibu wachezaji mashuhuri Mrisho Ngasa, Jerry Tegete, Haruna Niyonzima, Nadir Haroub “Cannavaro”, Salum Telela, David Luhende, Simon Msuva na Athumani Idd “Chuji”…kwa kuwakata nusu ya mshahara kutokana na utovu wa nidhamu.

Suala la ulevi na kutokuwa na nidhamu limekuwa mada kubwa sana nchi za Kizungu hasa katika vipindi vya sikukuu ya Krismasi inayokaribia. Miaka ya zamani wachezaji kijumla walikuwa na tabia ya kufanya walivyotaka , kulewa na kulala usiku sana.

Hapa Uingereza mambo yalibadilika alipoingia Arsene Wenger wa Arsenal, mwaka 1996 akaleta sera ya ulaji bora wa vyakula, kutokunywa pombe na kulala mapema. Wenger alikuwa akitokea Japan alikojifunza nidhamu ya michezo ambayo inaoanisha masuala ya afya na taaluma.

Leo mchezaji akionekana anafanya jambo lisilo la kawaida kama mwanamichezo husutwa na vyombo vya habari. Baadhi ya tabia au vitendo hivi ni kama kuvuta sigara (Jack Wilshere wa Arsenal), malaya au wanawake wengi (Wayne Rooney na Ashley Cole), kukaa katika vilabu vya usiku kucha (mshambuliaji Raheem Sterling wa Liverpool karibuni) nk.

Mbali ya sababu ya kiafya na michezo ni biashara. Miaka michache iliyopita mchezaji wa Golf, Tiger Woods alipata shida sana ilipodaiwa alikuwa na wanawake wengi wakati ana mke. Makampuni mengi ya kitajiri yalianza kuondoa jina lake katika baadhi ya matangazo aliyoyafanya. Ilimbidi ajirudi na kuomba msamaha ingawa hakukubaliana na kila shtaka au dai lililosemwa.

Wachezaji wa Yanga walikatwa mshahara lakini kwa wachezaji maarufu dunia ya Kizungu ni zaidi ya kukatwa mshahara. Vipato vingine vile vile huathirika na kupungua. Makampuni huyatumia majina ya wachezaji kuuza bidhaa.

Ndiyo maana wiki jana kocha Harry Redknapp wa timu ya QPR (Queen Park Rangers) alisisitiza kusiwepo na hafla ya Krismasi kwa wachezaji kutokana na woga kwamba mabaya wataharibu. Kawaida sehemu za kazi nchi zinazofuata sherehe za Krismasi hufanya tafrija siku chache kabla ya sikuu ya Krismasi.

Harry Redknapp alinukuliwa na gazeti la Evening Standard akihimiza lazima wachezaji kuwa makini.
Akasisitiza, “Mtu yeyote anaweza kukupiga picha ukiwa katika hafla umepepesa macho halafu wapambe wadai ulikuwa umelewa.”

Kuna msemo wa Kiingereza usemao usikutwe na suruali magotini. Msemo una maana mtu mashuhuri ana wajibu mkubwa mbali ya taaluma yake. Ndiyo maana Harry Redknapp na Arsene Wenger huwa na fimbo mkononi kuwataka wachezaji wao wasizembee nje ya viwanja.

Bila shaka tatizo lililowafika wachezaji wa Yanga si geni kwa vijana. Kijana ni mtu anayeanza maisha, asiye bado na majukumu ya watoto nk. Watoto wanaokua nao huwaangalia wachezaji kama watu wa mfano. Hii ni kutokana na maisha yao yalivyo, utajiri na vivutio vya runinga na vyombo vya habari. Ndiyo sababu umaarufu na taaluma vina uzito wake.

Kinyume na miaka hamsini iliyopita leo umaarufu na taaluma vinashika nafasi ya familia, dini na maadili mengine muhimu ya kijamii.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version