Beki Chris Smalling wa Manchester United ameadhibiwa na klabu yake kutokana na kitendo chake cha kuimba na rafiki zake katikati ya Jiji la Manchester usiku wa manane baada ya kupiga kinywaji.
Smalling ambaye ni majeruhi, alikutwa saa tisa usiku wa kuamkia Jumapili akiimba na wenzake wakiwa katika hali ya ulevi, ikiwa ni baada ya United kuwashinda West Ham United kwa mabao 2-0 jijini London.
Kocha wa Manchester United, David Moyes amekiri kuwapo tukio hilo, akasema wameshamchukulia hatua za kinidhamu na kwamba binafsi alizungumza na kijana huyo, isipokuwa hakutaka kuingia kwa undani juu ya tukio lenyewe.
“Sisi ndio Manchester United na tunafanya kile tunachopenda,” waliimba kilevi Smalling na wenzake, pia wakiruka kwa shida kutokana na mavune ya kileo.
Smalling mwenye umri wa miaka 24 hajacheza tangu Machi 8 walipochuana na West Bromwich Albion, lakini wadau wanaeleza kwamba mwenendo wake huo unaweza kumharibia mambo, hasa wakati huu ambapo Mashetani Wekundu wameshikwa pabaya katika Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Smalling anaonekana kuanza kujenga kiburi na kujiamini sana, kutokana na kwamba mabeki wengi ama wamekuwa wagonjwa, wamepigwa kadi nyekundu au kiwango kinagomba kutokana na umri kuwatupa mkono kama Rio Ferdinand.
Nahodha Nemanja Vidic amekuwa ama majeruhi au nje kwa kadi nyekundu wakati Jonny Evans naye ana majeraha. Jumamosi iliyopita Michael Carrick alilazimika kucheza beki ya kati pamoja na Phil Jones.
Kitendo cha Smalling kinachukuliwa kwamba ni utovu wa nidhamu, kisichokubalika katika soka la kulipwa, ambapo huweza kuimbwa wimbo kama huo wakati timu ama imetwaa ubingwa au ipo juu kabisa kwenye msimamo wa ligi, tofauti na sasa ambapo Man U wanateseka katika nafasi ya saba na hawana uhakika wa kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.