Awali ni awali tu na la kuvunda halina ubani; Juventus wamewavua ubingwa wa Ulaya Real Madrid.
Katika mechi ya mkondo wa pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) iliyopigwa nyumbani kwa Madrid, Santiago Bernabeu, vijana wa Carlo Ancelotti wameshindwa kuwadhibiti Wataliano.
Wakiwa na deni la bao moja kutokana na kufungwa 2-1 kwenye mechi ya mkondo wa kwanza, mabingwa hao wa zamani wa Ulaya walianza mechi kwa kujiamini.
Hata hivyo, Juve walioonekana kutaka kukombia klabu za Italia kwa kuwa chini katika Ulaya hawakukubali, na hata bao la penati la Cristiano Ronaldo la dakika ya 23 lilisawazishwa dakika ya 57 na Alvaro Morata.
Juventus, au kama wanavyojulikana kama bibi kizee wa Torino, watakuwa wanaingia fainali ya kwanza tangu 2003 na watakabiliana na Barcelona Juni 6 jijini Berlin kwenye fainali.
Ancelotti sasa ana wakati mgumu, kwa sababu inaelekea wazi kwamba atakosa kikombe cha maana, kwani katika Ligi Kuu ya Hispania yupo nyuma ya Barca kwa pointi nne, wote wakiwa wamebakisha mechi mbili.
Amezuiwa kuwa kwenye eneo la benchi la ufundi kwa mechi hizo, baada ya kuwakebehi waamuzi wa mechi iliyopita ya La Liga kwa kuwapigia makofi baada ya mechi.
Barca, wapinzani wakubwa wa Madrid wanaweza kutwaa makombe matatu makubwa, kwani licha ya uwaniaji wao wa kombe la UCL, wamefika fainali ya Kombe la Mfalme na wanatarajia kutwaa ubingwa wa Hispania.
Real Madrid watajiuliza sana, kwa sababu Morata ni mchezaji wao waliyemuuza Juve msimu uliopita na kazi yake imeyeyusha ndoto za timu za Hispania kukutana kwenye fainali, ambayo kwao huuita ‘El Clasico’.
Penati ya Real kwenye mechi ya Jumatano hii ilitokana na Giorgio Chiellini, yule aliyeng’atwa na Luis Suarez wa Barcelona, kumchezea vibaya Ronaldo.
Matokeo ya mechi yangeweza kuwa mengine kama wachezaji wa Real, Gareth Bale na James Rodriguez na wengineo wangefanikiwa kwenye fursa walizopata.
Juventus wamefika hatua hiyo baada ya kuwatoa Monaco kwenye hatua ya robo fainali wakati Barca waliwaondosha Paris Saint-Germain.
Hali hii inampa wakati mzuri kocha wa Barca, Luis Enrique, ambaye hata hivyo tetesi zinaonesha kwamba anaweza kuondoka huku Ancelotti aliyeeleza matumaini ya kubaki Madrid sasa akiwa katika kiti moto.