*Man U wapata majeruhi mwingine
Mataifa ya Ulaya yameshauriwa kuunganisha nguvu kugomea fainali zijazo za Kombe la Dunia ili iwe shinikizo kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kufanya mageuzi makubwa ndani mwake.
Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Soka (FA) cha england, David Bernstein amekishauri chama hicho kushawishi vyama vingine barani Ulaya kuwashinikiza akina Sepp Blatter wanaoendesha shirikisho hilo kiimla kwa harufu ya rushwa wabadilike.
Bernstein amesema England pekee hawawezi kutia ushawishi kwa kujitoa au kutishia, hivyo ni vyema wakashawishi nchi nyingine, akisema fainali za Kombe al Dunia zitadhoofika sana iwapo Ulaya haitashiriki, hivyo Fifa wanaweza kusalimu amri.
Ushauri huo unakuja wakati kukiwa na kukinzana kwa ripoti juu ya uwapo wa matumizi ya mlungula katika kuwania uenyeji wa michuano ya 2022 inayofanyika Qatar majira ya joto wakati kinaonekana ni kitu kisichowezekana.
Kadhalika Fifa iliishambulia FA kwa maelezo kwamba watu wake walijiongoza vibaya katika kuwania kuandaa fainali hizo. Fainali zinazofuata zinafanyika nchini Urusi, ambapo pia kutokana na ubabe wa Rais Vladimir Putin, pamekuwapo kelele za kutaka kususia.
“Ningekuwa FA kwa sasa, ningechukua kila jitihada kushawishi mataifa mengine yaliyo ndani ya Uefa kutishia kugoma na nina hakika tungefanikiwa. Katika baadhi ya hatua unatakiwa kutumia vitendo na si kuzungumza tu,” akasema Bernstein aliyeondoka madarakani kutokana na kufikisha miaka 70.
Akasema angetaka Blatter ajiuzulu nafasi yake, lakini akasema kwamba amejiimarisha sana hapo kitini na kwamba ni mjanja, akisema si rahisi kumwondosha madarakani. Blatter aliyekuwa ametangaza akimaliza ngwe yake atastaafu, amesema anagombea tena, kwa madai kwamba kuna kazi hajazimaliza.
Bernstein amesema Fifa inajiendesha kidikteta, akisema utawala huo unamkumbusha ule wa zamani wa Sovieti, akisema uadilifu katika soka sasa umeshuka kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya sampuli ya uongozi wa shirikisho hilo.
Akaongeza kwamba kuichagua Qatar kuwa wenyeji 2022 ni moja ya maamuzi mabovu na ya kustaajabisha zaidi katika historia ya soka. Baadhi ya nchi zilizotaka kuandaa na zikapigwa kumbo ni England yenyewe, Marekani, Australia, Korea Kusini, Japan.
DALEY BLIND WA UNITED AUMIA GOTI
Katika tukio jingine, Manchester United wameendelea kupata mapigo kwa wachezaji wake kuumia, safari hii akiwa kiungo mpya, Daley Blind ambaye ameumia goti.
Blind aliumia dakika ya 20 na kuondoka uwanjani akichechemea wakati akiiwakilisha Uholanzi kwenye mechi ya kufuzu kwa michuano ya Euro 2016 dhidi ya Latvia, ambapo timu yake ilishinda kwa 6-0.
Kocha wa Uholanzi, Guus Hiddink amesema ana wasiwasi kwamba ameumia vibaya, mchezaji mwenyewe ameandika kwamba anafurahia kuliwakilisha taifa lake katika mechi 25, amesikitishwa sana kuumia lakini anaamini atarudi mwenye nguvu zaidi.
Huyu ni mchezaji wa tatu kwa United kuumia katika mapumziko haya ya mechi za Ligi Kuu ya England, wa kwanza akiwa kipa David De Gea aliyeteguka kidole cha mkono wa kulia akichezea Hispania Ijumaa wakati Michael Carrick alijitoa kwenye kikosi cha England kutokana na maumivu.