Washambuliaji wanasajiliwa ili kufunga mabao. Lakini zipo timu zinao washambuliaji wanaofunga mabao mengi lakini zinakosa ubingwa. Zipo timu zina washambuliaji wa kawaida lakini zinaibuka na ubingwa au kuwa na rekodi nzuri. Katika timu yoyote inapofunga mabao ya kutosha kusaka ushindi michezoni, safu ya ulinzi inahitajika kulinda lango lao.
Kadiri timu inavyofunga mabao na kulind ndivyo inavyojiwekea nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa. Simba ni miongoni mwa timu zilizofanya usajili wa nguvu msimu huu. Imesajili walinzi wa kati na pembeni; kulia na kushoto. Imesajili viungo wa ulinzi, viungo washambuliajio na washambuliaji pamoja na mawinga. Katika hali hiyo mashabiki wanategemea kuona Simba ikipachika mabao mengi langoni mwa adui. Lakini pia inatarajiwa kuona Simba inazuia lango lake kugeuzwa asusa.
Kimbinu kocha Fadlu David amejitahidi kuhakikisha uchezaji wa pamoja kwa timu katika kuhakikisha wote wanakuwa na mkakati mmoja wa kusaka ubingwa. Msimu huu Simba wameongeza hasira za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu ambao waliupoteza misimu minne iliyopita. Samba fedha wanazo, uongozi upon a zaidi wamejitajidi kulinda nyota wao muhimu. Lakini nini hasa kinachoweza kuwasaidia Simba kuibuka na ubingwa? Kulijibu swali hili tuangalie mchezo wao dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Mchezo huo ulichezwa kwenye uwanja wa KMC Stadium jijini Dar Es Salaam ambapo Simba walikuwa wenyeji wa Coastal Union. Katika mchezo huo Simba walitangulia kupachika mabao 2 ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza. Katika kipindi cha pili Simba waliingia wakiwa na hazina ya mabao mawili mkononi lakini hali ya mambo ilibadilika ghafla tu. Hadi dakika 90 za mchezo zilipokamilishwa matokeo yalikuwa 2-2. Kwamba Coastal Union walifanikiwa kurejesha mabao yote na kulazimisha suluhu.
Hapo ndipo iliposmama hoja yangu ya leo, je Simba inawezaje kufikiria ubingwa ikiwa inageuziwa kibao kirahisi namna hiyo? Jibu la swlai hilo sio la kimfumo pekee bali aina ya wachezaji waliosajiliwa. Kwa kuzingtatia mfumo wa Fadlu David, Simba wanasimama vizuri na mabeki wanne, lakini mpango wa kwanza ni kuhakikisha wanacheza mabeki wawili hadi watatu.
Jukumu la Shomari Kapombe na Mohammed Hussein linakuwa lileile kuhakikisha wanacheza kama mawinga katika nafasi zao, hivyo kuwaacha nyuma Ihrahim Hamza na Chermalone wakisimama kama mabeki wa kati wakisaidiwa na kiungo mkabajai Yusuf Kagoma. Kimbinu Yusuf Kagoma ndiye anawasaidia mabeki wa kati na kusafisha ‘uchafu’ wote unaoletwa na timu pinzani.
Tumeona katika mechi akdhaa wakifanya hivi. Jambo pekee ambalo mwalimu wa Simba anatakiwa kulichukua kama funzo ni namna ya kumsaidia Yusuf Kagoma katika eneo hilo. Timu ya Dadlu David imekuwa na dhana ya ‘attacking mindset’ huku suala la ulinzi likiwa nyuma.
Ukweli ni kwmaba Simba katika mfumo wao wa -3-4-3 au 4-3-3 na 4-1-2—1-1 wanaweza kuziadhibu timu nyingi. Kwamba kama Leonel Ateba ataongoza mashambulizi, basi nyuma yake anaweza kusimama Kibu Dennis au Edwin Balua na Joshua Mutale. Watatu hao wanaweza kupishana kwa mmoja kukaa benchi, huku Ateba akiwa anasaidiwa wawili. Kwa maana hiyo Yusuf Kagoma atahitaji huduma ya Debra Fernandez katika kukamilisha kazi yake.
Vilevile kutokana na uzito wa mechi, mfano za ugenini katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho inabidi mwlaimu aelewe lazima atahitaji kupunguza wawili na hivyo kumtumia mmoja kati ya Kibu, Balu na Mutale. Lengo la kumnyima wapishi wengi Ateba pale mbele ni kuifanya timu iwe na uwezo wa kujilinda.
Kwa maana hiyo Kagoma na Fernandez watahitaji mtu mwingine wa kuvuruga mipango ya adui pale katikati ya dimba. Uamuzi utakuwa kumtumia Fabrice Ngoma au Mzamiru Yassin ili kushirikiana na Fernandez na Kagoma katika ‘Double pivot’. Fernandez atakuwa na uhuru mwingi na kusogea eneo la nambari 10 na hivyo yuyle wa nambari kumi atakuwa amemsogelea zaidi Leonel Ateba na kuliandama lango la adui. Kama timu ikishambuliwa kwa kushtukiza, tayari itakuwa na majembe wawili wa kulinda mabeki yaani Yusuf Kagoma na Ngoma au Yassin. Kazi ya Fernandez itakuwa kusambaza mipira kwa wingi kwa nambari 10 na 9 pamoja na kuachia mafataki makali kuelekea langoni mwa adui.
Kwa saa mipango ya mwalimu Fadlu David lazima izingatie suala la ulinzi ili kuepukana na makosa yaliyofanyika katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Coastal Union walichofanya ni kukuhakikisha kazi ya kiungo mkabaji na mshambuliaji inasambaratishwa na kuwarudisha nyuma zaidi hivyo Simba wakajikuta wamerudishwa nyuma na kuruhusu mabao mawili ya wageni. Ubingwa wa Simba umelalia kwenye uwezo wao wa kujilinda. Kadiri wanavyojilinda nidvyo wnaavyopunguza presha ya kupoteza mchezo kwani washambuliaji wao pale mbele wote wana uwezo wa kupachika mabao. Kwahiyo ukuta wa Simba utaamua ubingwa wao msimu huu.