*Ureno walala kwa Albania, Ireland washinda
*Mali pungufu wawaadhibu Malawi 2-0 Afcon
Ujerumani wameamka baada ya kuwa wamechapwa na Argentina kwenye mechi ya kirafiki, na sasa wamewafunga Scotland kwa tabu 2-1 kwenye mechi ya kwanza ya kufuzu kwa fainali za Euro 2016.
Thomas Muller ndiye alifunga mabao yote mawili moja katika dakika ya 18 na la pili dakika ya 70, ikiwa ni baada ya Ikechi Anya kuwasawazishia Waskochi kunako dakika ya 66 na kipindi cha kwanza Scotland walipata bahati lakini wakatumia vibaya.
Ulinzi dhaifu ulimruhusu Muller kucheka na nyavu na katika dakika za mwisho Scotland walipata pigo jingine kwa mchezaji wao, Charlie Mulgrew kutolewa nje baada ya kupewa kadi ya pili ya njano.
Mchezaji wa Sunderland, Steven Fletcher alikuwa amesema kabla ya mechi kwamba wangejitahidi kuwafunga Wajerumani, hasa baada ya kuona udhaifu wao mbele ya Argentina, na kweli alipoingia kipindi cha pili ndiye alitoa pasi murua kwa Anya aliyemtungua Manuel Neur.
Wenyeji Ujerumani walitawala mchezo huo kwa asilimia 69.
Katika mechi nyingine za kufuzu kwa Euro 2016 Georgia wakicheza nyumbani walichapwa 2-1 na Jamhuri ya Ireland, Hungary nao wakatandikwa idadi hiyo hiyo ya mabao na Ireland Kaskazini wakati Gibraltar wakichezea kichapo cha 7-0.
Matokeo mengine ni Visiwa vya Faroe kufungwa 3-1 na Finland, Ugiriki kuchomoza na ushindi wa 1-0 dhidi ya Romania, Denmark kuwafunga Armania 2-1 na Ureno kulala 1-0 mbele ya Albania.
MALI WAWAADHIBU MALAWI
Mechi ya kiporo ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) imemalizika kwa Mali kuwafunga Malawi 2-0.
Mali walicheza wachezaji 10 katika sehemu ya mchezo huo ulioahirishwa majuzi kwa sababu ya mvua kubwa, kwani kipa wao, Mamadou Samassa alipewa kadi nyekundu, lakini hiyo haikuwazuia kuwashinda Malawi 2-0 walio kwenye kundi B.
Samassa anayecheza nchini Ufaransa alitolewa nje kipindi cha pili mara baada ya Bakary Sacko anayechezea Wolverhampton Wanderers ya Uingereza kuwafungia Eagles. Mchezaji mwingine anayekipiga Ufaransa, Cheick Tidiane Diabate aliwahakikishia wenyeji ushindi kwa bao la pili dakika za lala salama.
Bao lake limewaweka Mali katika nafasi ya kwanza kwenye kundi lao, kwa tofauti ya bao moja dhidi ya Algeria waliowafunga Ethiopia 2-1 jijini Addis Ababa Jumamosi hii. Malawi wanawakaribisha Ethiopia Jumatano hii kwenye mchezo wa pili wakati Mali watakumbana na Algeria.