Historia inaniambia Chelsea inabahati sana na makocha wa Italy, wamekuwa na uwezo mkubwa wa kuifundisha Chelsea katika mafanikio makubwa.
Imekuwa desturi kwa kila kocha wa Italy kila anapokanyaga katika nyasi za Stamford Bridge lazima aweke furaha kubwa katika nyuso za mashabiki wengi wa Chelsea.
Ukurasa wa kwanza wa historia hii unaanza kumtaja Gianluca Vialli, inawezekana ndiye kocha aliyekuwa na mafanikio makubwa kwa kipindi kifupi alichowahi kukaa Chelsea. Miaka miwili pekee ilitosha kwa Gianluca Vialli kuipa Chelsea vikombe vitano.
Vikombe ambavyo viliipa nafasi Chelsea kuamini tena kupitia mbinu za Kiitaliano. Wengi tulishangaa timu ilipokabidhiwa mikononi mwa Claudio Ranieri, kocha ambaye hakushinda chochote lakini alikuwa mshindani wa kweli.
Kurasa za historia ya mpira wa miguu zinamtambua kama kocha ambaye aliwahi kufika fainali ya kombe la chama cha soka England (FA Cup), nusu fainali ya klabu bingwa barani ulaya na mshindi wa pili kwenye kampeni za ubingwa wa ligi kuu ya England katika msimu wa mwaka 2003-2004 na ndiye kocha ambaye alifanikiwa kuwatengeneza waliokuja kuwa magwiji makubwa wa Chelsea yani John Terry na Frank Lampard.
Magwiji ambao walifanikiwa kumtumkia Carlo Ancelotti katika utawala wake pale darajani. Utawala ambao ulikuwa na mafaniko makubwa kwa sababu alifanikiwa kubeba vikombe vitatu, vikombe ambavyo vilitengeneza furaha kubwa kwa mashabiki wa Chelsea.
Chelsea ilikuwa moja ya timu tishio chini ya mikono Carlo Ancelotti, ila kama ambavyo waswahili walivyowahi kusema kuwa hakuna kinachodumu milele, ndivyo ilivyokuwa kwa safari ya Carlo Ancelotti.
Haikuwa safari ya muda mrefu sana, miaka miwili pekee ilitosha kuweka alama zake pale darajani. Muda wake uliisha na nafasi ya muda wa Roberto Di Matteo kukaa kama kocha wa muda ulifika.
Kocha ambaye aliipa Chelsea kombe la klabu bingwa barani ulaya. Kitu ambacho ni kikubwa na kilikuwa kinatokea kwa mara ya kwanza na mpaka sasa hivi hakijawahi kutokea katika nyasi za Stamford Bridge. Pamoja na kuwapa Kombe la chama cha England (FA) na kombe la klabu bingwa barani ulaya lakini hakupewa nafasi ya muda mrefu katika kikosi cha Chelsea.
Hakuna aliyekuwa anamwamini kwa kiasi kikubwa na wengi waliyachukulia mafanikio yake kama bahati na yalikuja kwa bahati na hakuna uwezo mkubwa wa kimbinu uliotumika katika akili yake kuhakikisha Chelsea ikisimama mahali pakuu.
Mahali ambapo Antonio Conte alifanikiwa kusimama. Ndiye kocha mwenye asilimia kubwa ya ushindi pale Chelsea. Sera zake za kiitaliano ziliiwezesha Chelsea iwe sehemu inayoogopekwa.
Aliamini kupitia Catenaccio akaupa nafasi mfumo wa kutumia mabeki watatu wa kati. Mfumo uliompa nafasi ya kutengeneza timu inayoshambulia na kujilinda katika uwiano mkubwa kitu ambacho kilimwezesha yeye achukue makombe mawili ndani ya miaka miwili.
Huyu ndiye alitoa nafasi ya ukurasa wa kocha mwingine kutoka Italy kuja Stamford brigde. Maurizio Sarri, rafiki mkubwa wa sigara ambaye mpaka sasa mikono yake haijawahi kushinda taji lolote kama kocha lakini Chelsea wamemwamini na kumpa nafasi.
Anatengeneza historia ya kocha mwingine kutoka Italy kuifundisha Chelsea. Chelsea imekuwa na damu nzuri na makocha wanaotoka katika hii nchi, damu ambayo ni kama kiunzi kwa Maurizzio Sarri.
Kila mtu anasubiri kutazama hatua ambazo atatumia kuruka kiunzi hiki. Je atafanikiwa kutembelea kwenye nyayo za watangulizi wake kutoka Italy?
Kuna mengi ambayo watu wengi wanayasubiri kutoka kwake. Aliweza kuifanya Napoli icheze mpira wa kuvutia na mpira wa ushindani. Anakuja sehemu ambayo hakuna utamaduni wa kucheza aina hii ya mpira wa kuvutia.
Sehemu ambayo kwao wao mataji ndiyo suala la msingi kuliko mpira wa kuvutia kama ambao alifanikiwa kuuwekeza katika timu ya Napoli, ndipo hapo ugumu wa jibu la swali linalohoji uwezekano wa yeye kupitia njia ya mafanikio ya wenzake kutoka Italy unapoanzia.