*Waondoa nuksi ya penati
Uholanzi wamevuka kitisho cha mikwaju ya penati kwa mafanikio, wakiwatoa Costa Rica 4-3.
Baada ya dakika 90 kumalizika bila mshindi, dakika 30 za ziada pia hazikuzaa bao lolote hivyo wakaingia kwenye mikwaju ya penati wakiwa suluhu.
Costa Rica walikuwa wakisifika kwa penati, na washabiki wake walishangilia dakika 120 zilipomalizika wakidhani kwamba wangewatoa Wadachi ambao ni mara ya kwanza kushinda katika changamoto ya penati kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Kocha Louis van Gaal alimtoa kipa JasperCillessen dakika za mwisho kabisa na kumwingiza Tim Kruul wa Newcastle United aliyeamini angewasaidia kwenye penati.
Kruul alipangua penati mbili; ya Bryan Ruiz na ya Michael Umaña huku Uholanzi wakifunga nne na kumaliza mchezo.
Nahodha Robin van Persie alitangulia kufunga ya kwake, kisha Arjen Robben na Wesley Sneider kabla ya mkongwe Dirk Kuyt kukwamisha fataki la chini chini wavuni hivyo kutosha kuwatoa Costa Rica.
Katika mchezo kwa ujumla Uholanzi walitawala, wakishambulia na kukosa mabao zaidi ya matatu ya wazi, baadhi ya mipira ikiokolewa na kipa Keylor Navas ambaye katika fainali hizi aliruhusu mabao mawili tu, ila kwa penati si mzuri. Mipira mingine iligonga mwamba.
Van Persie na Sneider walikosa mabao pia, huku Robben kama kawaida akisumbua ngome ya adui na kupata faida ya mipira ya adhabu baada ya mwamuzi kuridhika alikwatuliwa mara kadhaa, huku wachezaji wa Costa Rica wakitoa ishara za yeye kujiangusha.
Kwa ujumla Uholanzi walionekana kukosa bahati katika dakika zote 120, huku Costa Rica wakijihami zaidi na kushindwa kufanya mashambulizi ya maana hadi mpachika mabao wao, Joe Campbell wa Arsenal alipopelekwa benchi.
Sasa Uholanzi watachuana na Argentina Jumatano hii, ambao katika mchezo wa awali Jumamosi hii waliwafunga Ubelgiji kwa bao moja la dakika ya nane la Gonzalo Higuain.
Nusu fainali ya kwanza itakuwa Jumanne, baina ya Brazil na Ujerumani.
Brazil waliwatoa Colombia kwa mabao 2-1 kwa tabu Ijumaa wakati Ujerumani waliwazidi nguvu Wafaransa kwa bao 1-0 Ijumaa hiyo hiyo, balo lililofungwa na Mats Hummels.