ILIKUWA ni majira ya saa 12 na nusu kasoro dakika chache jioni kwa saa za Afrika Mashariki, Alhamisi ya Oktoba 31,2013 wakati uwanja mkubwa na wa kisasa wa michezo kuliko yote Afrika ya Mashariki na ya Kati, usio na jina, uliopo eneo la Chang’ombe jijini Dar es Salaam, Tanzania ulipopewa adhabu usiyostahili na mashabiki kadhaa wahuni wa Simba Sports Club. Labda kosa la uwanja huu lililosababisha adhabu hiyo ni kukosa jina, jambo ambalo isingeweza kulifanya wenyewe!
Ni hivi; uwanja huu unaitwa uwanja wa Taifa (National Stadium) badala ya uwanja wa Benjamin William Mkapa, Jakaya Mrisho Kikwete, Mzizima, Hussein Tindwa, Adolph Rishard, Peter Tino, Kinjekitile Ngwale, Kilimanjaro, Tanzanite,Muungano, Ujamaa, Kujitegemea nk. Uwanja wa Taifa, unazungumzia taifa gani wakati duniani kuna mataifa 195? Uwanja huo kuwepo tu Tanzania hakutoi tafsiri ya kwamba taifa hilo ni Tanzania kwani nchini Tanzania tuna uwanja wa Samora, barabara za Mandela, Sam Nujoma, Mwai Kibaki, Barack Obama na mitaa ya Nkrumah, Azikiwe na kadhalika ambao si Watanzania! Hebu tuondoke hapa twende kwenye mada.
Jioni ya tarehe iliyotajwa hapo juu kulikuwa na pambano kali la soka lililovuta hisia kubwa baina ya Simba ya jijini Dar es Salaam na Kagera Sugar ya Bukoba. Hisia kubwa ilitokana na ukweli kwamba kama Simba ingeshinda ingelingana pointi na waliokuwa wanaoongoza ligi wakati huo ambao ni Azam F.C ya Dar es Salaam na Mbeya City ya Mbeya waliokuwa na pointi 23 wakati huo. Kagera nao walihitaji pointi tatu ili wafike poiti 19 wasogelee kilele.
Simba walipata bao dakika ya 45 ya mchezo likifungwa na Amiss Tambwe likiwa bao lake la tisa msimu huu wake wa kwanza kwenye ligi kuu ya nchi ya Tanzania akitokea Vital’O ya Burundi. Kwenye dakika ya mwisho kabisa ya mchezo, Kagera walipata penalti iliyowekwa kambani na mchezaji wa zamani wa Simba, beki Salum Kanoni, na mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1.
Tukio la penalti ya dakika ya mwisho ndilo liliwakera baadhi ya mashabiki wa klabu ya Simba waliong’oa viti vya uwanja wetu wa kisasa na kuvirusha ovyo kufanya uharibifu usiomithilika na usiohalalishwa hata kama mwamuzi alikosea. Hapa kuna kitu kinachoitwa umbali wa matukio (remoteness of events); tukio la mwamuzi kutoa penalti dhidi ya Simba liko mbali mno na mali za umma ndani ya uwanja wa Taifa. Viti hivyo havikuhusu uzembe wa wachezaji wa Simba kuruhusu mpira uchezewe kwenye eneo lao kwenye dakika za mwisho za mchezo na wala havikumhusu mwamuzi aliyefanya uamuzi wa kuwakera mashabiki wa Simba. Ni tukio la hujuma lisilo na chembe ya umantiki.
Adhabu mara zote kwa tukio kama hilo huwa hazitolewi kwa klabu za mashabiki wahuni kama hao. Wanapokatwa pesa za kugharamia matengenezo ya uharibifu ni sawa na kupewa jukumu la kurudisha hali iliyoharibiwa. Kwa nini wasirudishe hali iliyoharibiwa na watu wao? Baada ya kurudisha hali hiyo ndipo adhabu ingetolewa na adhabu hiyo iwe na maumivu fulani kwa klabu na kwa mashabiki ambao kutokana na maumivu hayo wenyewe kwa wenyewe watadhibitiana.
Ukitoa adhabu ya timu kucheza mechi kadhaa bila mashabiki,hilo halitekelezeki kwa sababu, kwa mazingira ya Tanzania, mashabiki hao wataingia kama si mashabiki wa timu hiyo inayoadhibiwa. Kwa hiyo, inafaa klabu hiyo iadhibiwe kwa kulipa faini kubwa baada ya kulipa gharama za matengenezo ya uharibifu. Zaidi ya hayo, timu hiyo ifungiwe mechi mbili au tatu kutumia uwanja wa mji wao kwa kuelekezwa umbali mrefu kwa mfano kilometa zitakazotajwa zisipungue ambazo zitawalazimisha wakachezee Tabora, Shinyanga au Mwanza huku gharama zozote za ziada za timu pinzani kuzifuata huko walipe wao.
Kitendo cha timu yao kupelekwa mbali wakifanya uharibifu, kitawafanya mashabiki wenyewe kwa wenyewe kukemeana mwenzao akiharibu mali ya uwanja au akifanya kitendo chochote cha kustahili adhabu ya hivyo huku klabu nayo ikiwatumia viongozi wa matawi kuwasihi mashabiki wasifanye vitendo vya kustahili adhabu za kuziumiza klabu wazipendazo. Lakini kwa nini mpaka tufike huko? Kwa nini tusiwe na busara za sisi wenyewe kuwa wastaarabu na kuacha ujinga huo?
Tunalaani kwa nguvu zote uhuni uliofanywa na mashabiki wa Simba wa kuharibu mali ya umma kwenye uwanja wetu mkubwa na wa kisasa uliokosa jina, uwanja wa Taifa, sijui taifa lipi!