Menu
in

Uhamisho wa nyota wafuatao hauzuiliki

BW

Tazama vikosi vya timu 5 za juu za EPL utagundua kuwa wapo nyota ambao walitikisa misimu kadhaa iliyopita au wanaendelea kutikisa lakini hawapangwi mfululizo kwenye vikosi vya kwanza. Kwa mfano, mchezaji nyota anaweza kukosekana na timu ikafanya vizuri au ikacheza pasipo kuonesha kuwa lipo pengo la nyota wao aliyekosekana.

Ni hivi ndivyo hali ilivyo katika vikosi vya PSG,Manchester  City, Manchester United, Liverpool, Chelsea au Arsenal. Mchezaji anaweza kuonekana ni muhimu kikosini lakini makocha wamejitahidi kuhakikisha vikosi vyao vinamudu kucheza pasipo kumtegemea staa wao.

Makala haya nachambua mwenendo wa wachezaji ambao ni nyota katika timu zao lakini upo uwezekano mkubwa wa kuuzwa na uhamisho wao hauzuiliki ifikapo Januari 2022 au usajili wa majira ya kiangazi yaani Juni,Julai na Agosti.

RAHEEM STERLING (Manchester City)

Winga huyu alihamia hapo akitokea Liverpool. Alikuwa mchezaji wa mwanzo aliyetumika kuunda zama mpya za Manchester City. Alisajiliwa akiwa kinda na kuzua gumzo kwanini aliondoka kwa wafalme wa mataji Liverpool. Nafasi yake kule Liverpool ilichukuliwa na Jordan Ibe kinda aliyetabiriwa kufanya vizuri kumzidi, lakini haijatokea hadi leo.

Kuanzia msimu uliopita kumekuwa na hali ya kupungua dakika za kuchezeshwa nyota huyo. Mara kadhaa ameanzia benchi katika mechi muhimu na kubwa. Mbele yake wapo mawinga wingine Bernardo Silva na Riyaz Mahrez ambao wamekuwa chachu ya ushindi wa kikosi cha Pep Guardiola.

Ingawaje kocha huyo amedai Raheem Sterling hauzwi, ni kauli inayofanana na wakati alipokuwa na Sergio Kun Aguero. Mahrez amepatiwa nafasi kubwa zaidi, na ndio chanzo cha Bernardo Silva kutaka kuondoka klabu hapo.

Hata hivyo hilo halikutokea na Bernardo amesalia klabuni. Lakini hali inaonesha maisha ya Raheem Sterling ndani ya Man City yanazidi kuyoyo, huku kukiwa na chipukizi mwingine Phil Foden ambaye anatarajiwa kuongezewa mkataba.

Sterling anawindwa na klabu ya Barcelona ambao wana nia ya kumsajili kwa mkopo ifikapo Januari 2022. Barca wamewahi kujaribu kumsajili ny9ta huyo katika maira ta kiangazi lakini bado wana matumaini atapatikana. Kwa vile nafasi yake kikosi cha Pep Guardiola inazidi kufifia itakuwa rahisi nyota huyo kuamua kuondoka.

PAUL POGBA (Manchester United)

Kabla ya ujio wa Cristiano Ronaldo ilionekana wazi Paul Pogba ndiye mchezaji nyota zaidi katika kikosi cha kocha Ole Gunnar Solskjaer. Ronaldo ni kama ametibua ufalme wa Pogba ambaye mwenendo wake umehusishwa na kuhama Old Traford mara kadhaa.

Zinedine Zidane akiwa kocha wa Real Madrid alihusishwa na usajili wa nyota huyo. Taarifa za vyombo vya habari zilisema kuwa Zidane alipokuwa kocha klabuni hapo alitaka Pogba asajiliwe. Kwenye mikutano kadhaa na vyombo vya habari Zidane alikiri umahiri wa Pogba na kutamani aje kikosini mwake lakini akabainisha kuwa uamuzi huo upo mikononi mwa klabu.

Ikapita misimu miwili hadi Zidane ameondoka Real Madrid bado Pogba hakusajiliwa. Amehusishwa na PSG lakini waarabu hao wameweka fedha zao kumsajili Lionel Messi. Ni kama hawamhitaji Pogba na anajikuta hana pa kwenda zaidi ya kuhusishwa tena kurejea Juventus.

Pogba hajaongeza mkataba wa kuitumikia Man United, na inavyoonekana wapo tayari kumpoteza nyota huyo. Ole Gunnar ni kama amepata tiba ya kudhibiti usumbufu wa Pogba kwa kusajili nyota zaidi yake yaani Ronaldo.

Pogba ufalme  wake umefifishwa hivyo analo chaguo la kupokea ofay a Man United ambayo ni chini ya matakwa ya mshahara wa pauni 400,000 kwa wiki. Kwa sasa Pogba si mchezaji wa kusema akikosekana kikosini basi Man United itapepesuka, hapana.

Na wala haonekani kuzivutia timu nyingi kufanya naye biashara. Wataalamu wa kandanda wanasema tatizo la kwanza la Pogba ni wakala wake mwenye utata mwingi, Mino Raiola. Ni mojawapo ya sababu inayochangia vilabu vingi kumnyamazia kiungo huyo mwenye kipaji kikubwa na umri wa miaka 28.  

LIONEL MESSI (PSG)

Uwezekano wa mshambuliaji wa PSG Lionel Messi kudumu klabuni hapo zaidi ya mkataba wake wake utakaomalizika mwaka 2023 ni vigumu. PSG hawaonekani kuwa hatari mbele ya timu pinzani licha ya kuwa na safau kali ya ushambuliaji inayoundwa na Messi,Neymar na Mbappe.

Mbele ya Club Brugge ya Ubelgiji, Messi,Neymar na Mbappe walionekana kuwa wachezaji wa daraja la chini. Na zaidi wachezaji wenzake wa PSG hasa safu ya kiungo ni kama walikuwa hawaelewi wachezeje wakiwa na staa huyo.

Video mbalimbali zinaonesha wachezaji wa PSG hata kufungua na kuomba nafasi ni tatizo kubwa, ambalo lilichangia kumnyima Messi nafasi ya kufurukuta. Ukiacha Neymar anayemwelewa staa huyo, bado PSG hawajui namna gani watamtumia Messi hivyo timu nzima inaonekana kuwa dhaifu.

Michael Owen mchambuzi wa soka amekiri hilo wakati akielezea mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya PSG na Club Brugge ambapo badala ya timu kuwa imara inaonekana kukosa maarifa ya pamoja hivyo kila mchezaji kucheza kivyake.

Taarifa kutoka Argentina zinabainisha kuwa Messi huenda akaelekea kucheza Ligi Kuu Marekani maarufu kama MSL mara baada ya mkataba wake kumalizika ifikapo mwaka 2023. Lakini uhamisho wa nyota huyo kabla ya kumalizika mkataba wake ni mkubwa kwa sababu PSG watataka kuvuna kitita cha fedha za mauzo yake.

HARRY KANE na ANTONIO RUDIGER

Ingekuwa kwenye uwanja wa masumbwi basi tungesema hili ni pambano kali za uzani wa juu. Iko hivi Tottenham Hotspurs  walifanya jaribio la kumsajili beki kisiki wa Chelsea, Antonio Rudiger bila mafanikio.

Chelsea nao walijibu mapigo kwa kutaka kumsajili mshambuliaji wa Tottenham Hotspurs, Harry Kane bila mafanikio. Wote wamebaki katika klabu zao lakini uhamisho wa nyota hao wawili unaelekea kutozuilika.

Harry Kane aliyekiongoza kikosi cha England kufika fainali ya Euro 2020 alitaka kuhama klabuni hapo huku timu za Chelsea,Man United,Real Madrid na Man City zikihusishwa na uhamisho huo.

Hata hivyo staa huyo alibaki Spurs lakini muda unayoyoma, haonekani kubaki hapo tena kuanzia uhamisho wa Januari 2022 au majira ya kiangazi Juni,Julai na Agosti.

Harry Kane amekuwa mchezaji mkubwa wa Spurs lakini amekosa mataji ya kuongeza wasifu wake katika kandanda kitu ambacho kinamnyima raha hivyo kutamani kuondoka klabuni hapo. Kubaki kwake kumetajwa ni sababu ya masharti aliyotoa kwa Spurs.

ALEXANDRE LACAZETTE (Arsenal)

Mshambuliaji huyu hana namba ya kudumu Arsenal huku mkataba wake ukielekea ukingoni. Mikel Arteta ni kama haamini katika uwezo wa Mfaransa huyo kiasi kwamba amekuwa mchezaji wa homa za vipindi; anaweza kupangwa mechi tatu mfululizo kisha akawekwa benchi zaidi.

Arteta licha ya kutokuwa na washambuliaji wa daraja la juu kama Harry Kane bado ameshindwa kumtumia ipasavyo Lacazette mwenye umri wa miaka 30 kwa sasa. Kwa umri huo anaelekea ukingoni.

DECLAN RICE (West Ham)

Ni dhahiri waponda nyundo hao wameshikilia dhahabu isiyo yao. kiungo Declan Rice ni mchezaji wa mzuri na amepandisha hadhi yake hasa katika fainali za Euro 2020 zilizochezwa mwaka huu. Rice akiwa na Kalvin Philip walikuwa injini ya kikosi cha England kilichofika fainali.

Man United wanawinda sahihi ya Rice, naye amegoma kuongeza mkataba mwingine West Ham. Kwa sasa ana umri wa miaka 26 na uhamisho wake kwenda Old Traford unaonekana hauzuiliki kwa sababu West Ham hawawezi kumzuia tena licha ya kukataa dau la pauni milioni 100 katika dirisha la usajili lililopita. Nao Manchester United wamepania kumsajili nyota huyo kuchukua nafasi ya Fred ambaye hajakidhi malengo ya kusajiliwa kwake.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version