Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) imewasili Dar es Salaam leo tayari kwa
mechi ya kwanza ya mchujo kusaka tiketi ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji
wa Ligi ya Ndani (CHAN) kati yake na Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa
Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
The Cranes inayofundishwa na Mserbia Sredojvic Micho imetua Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 5.30 asubuhi kwa ndege ya Air
Uganda, na imefikia hoteli ya Sapphire.
Timu hiyo leo (Julai 11 mwaka huu) itafanya mazoezi saa 9 alasiri kwenye
Uwanja wa Karume, wakati kesho saa 9 alasiri itafanya mazoezi Uwanja wa
Taifa, kabla ya kuipisha Taifa Stars itakayoanza mazoezi saa 10 kamili
jioni.
Taifa Stars inayofundishwa na Mdenmark Kim Poulsen, na kudhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager, leo kwa mujibu wa program yake haitakuwa na
mazoezi.
Wachezaji wanaounda The Cranes ni makipa Ismail Watenga, Kimera Ali na
Muwonge Hamza. Mabeki ni Guma Dennis, Kasaaga Richard, Kawooya Fahad,
Kisalita Ayub, Magombe Hakim, Malinga Richard, Mukisa Yusuf, Savio Kabugo
na Wadada Nicholas.
Viungo ni Ali Feni, Birungi Michael, Frank Kalanda, Hassan Wasswa, Kyeyune
Said, Majwega Brian, Mpande Joseph, Muganga Ronald, Ntege Ivan, Owen
Kasule, wakati washambuliaji ni Edema Patrick, Herman Wasswa na Tonny Odur.
*TENGA KUZUNGUMZA NA WAANDISHI KESHO*
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga atakuwa
na mkutano na waandishi wa habari. Mkutano huo utafanyika kesho (Julai 12
mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye hoteli ya Tansoma.
Kutokana na mkutano huo, sasa mkutano kati ya makocha wa Taifa Stars na The
Cranes uliokuwa ufanyike saa 5 asubuhi ofisi za TFF nao umehamishiwa hoteli
ya Tansoma. Mkutano huo pia utahusisha manahodha wa timu zote mbili.
*WAJUMBE MKUTANO MKUU MAALUMU KUWASILI KESHO*
Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) utakaofanyika Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) wanawasili jijini Dar es
Salaam kesho (Julai 12 mwaka huu).
Mkutano huo wa marekebisho ya Katiba utakuwa chini ya uenyekiti wa Rais wa
TFF, Leodegar Tenga na utafanyika ukumbi wa NSSF Waterfront kuanzia saa 3
kamili asubuhi. Wajumbe wote wa mkutano huo watafikia hoteli ya Travertine.
Pia mkutano huo utahudhuriwa na wageni mbalimbali waalikwa wakiwemo kutoka
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na Chama cha Mpira wa
Miguu Zanzibar (ZFA).
* *
*MECHI YA STAND, KIMONDO NAYO KUPIGWA JUMAPILI*
Mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kati ya Stand United
FC ya Shinyanga na Kimondo SC ya Mbeya iliyokuwa ichezwe Jumamosi (Julai 13
mwaka huu) imesogezwa mbele kwa siku moja.
Timu hizo sasa zitacheza Jumapili (Julai 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa
Kambarage mjini Shinyanga. Kimondo ilishinda bao 1-0 mechi ya kwanza
iliyochezwa Julai 6 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi nyingine ya ligi hiyo itakuwa kati ya Friends Rangers ya Dar es
Salaam na Polisi Jamii ya Mara, na itafanyika kwenye Uwanja wa Azam ulioko
Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Mwamuzi wa mechi hiyo ni Hans
Mabena kutoka Tanga.