*Argentina ushindi mwembamba
*Uswisi wawazidi nguvu Ecuador
Fainali za Kombe bado zimendelea kutoa washindi, ambapo hadi Jumapili hii hakuna timu zilizokwenda suluhu wala sare.
Kwa mara ya kwanza teknolojia ya goli ilitumika kwenye mechi baina ya Ufaransa na Honduras, ambapo Ufaransa waliwafunga Honduras 3-0, lakini bao moja likazusha wasiwasi kwani kipa aliondosha mpira ukiwa tu ndio umevuka mstari.
Awali skrini kubwa uwanjani ilionesha kwamba si bao lakini mara moja ikaandika kuwa ni bao huku mwamuzi naye akapata alama kwenye saa yake mkononi na kuashiria mpira upelekwe kati.
Huo ulikuwa ushindi wa kwanza kwa Les Bleus tangu fainali za 2006, kwa sababu mwaka 2010 hawakupata ushindi hata mmoja na walitolewa kwenye hatua za makundi baada ya kuonesha utovu wa nidhamu kwa kugomea mazoezi.
Mabao ya Ufaransa yalifungwa na mshambuliaji wa Real Madrid, Karim Benzema aliyecheka na nyavu mara mbili wakati jingine liliwekwa kimiani na Noel Valladares.
ARGENTINA WATOKA NA USHINDI MWEMBAMBA
Argentina walilinda hadhi yao kwa kupata ushindi 2-1 dhidi ya Bosnia-Hercegovina, ambapo mchezaji matata duniani, Lionel Messi alipachika bao zuri.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Argentina kushinda, kwani Bosnia walipambana kiume lakini wakakosa bahati huku mlinzi wao Sead Kolasinac akijifunga katika harakati za kuokoa mpira wa adhabu wa Messi.
Baada ya hapo Messi aligongeana vyema na Gonzalo Higuain, wakwababaisha walinzi wawili kisha Messi akatundika mpira wavuni na kuandika bao la pili. Dakika sita kabla ya mechi kumalizika, Bosnia walipata bao kupitia kwa Vedad Ibisevic.
Macho yote yalikuwa kwa Messi, mchezaji aliyepata kuwa bora duniani mara nne, na mechi ilipigwa katika dimba maarufu duniani la Maracana lililo jijini Rio. Messi hakupata kufanya vizuri sana kwenye michuano hii, kwani bao lake la jana ni la pili katika dakika 623 alizocheza mechi hizi, maana bao lake la mwisho kabla ya hili la Jumapili alilifunga Juni 16, 2006 dhidi ya Serbia & Montenegro.
USWISI WAWAZIDI NGUVU ECUADOR
Uswisi waliendeleza wimbi la timu kutotoka sare, kwani wakiwa sare 1-1 na Ecuador, walitupia bao la ushindi katika dakika ya tatu ya muda wa ziada na kuwapatia pointi tatu muhimu.
Akitokea benchi, Haris Seferovic alifunga bao hilo muhimu katika mechi ya kwanza ya Kundi E. alinasa mpira wa chini chini wa Ricardo Rodriguez na kuamsha shangwe kwa washabiki, ikizingatiwa kwamba Uswisi ndio walikuwa wametangulia kufungwa.
Hata bao la kusawazisha lilifungwa na mchezaji aliyetokea benchi, Admir Mehmedi aliyefunga kwa kichwa. Ecuador walipata bao lao kupitia kwa Enner Valencia mapema katika dakika ya 22.