Argentina inatazwa sana, na hii ni kwa sababu imebeba mtu mmoja ambaye kwa sasa ndiye kioo cha mpira wa Argentina na duniani kwa ujumla.
Kuna magwiji wengi wamepita, kuna mengi wameyafanya na kuna vingi wameshinda na mwisho wa siku wakabakiza alama ambazo huwa tunazikumbuka kila uchwao.
Jua la leo linamaana kubwa sana katika maisha ya soka ya Lionel Messi. Ana miaka 30 mpaka sasa hivi, miaka ambayo inampa muda mchache wa kuendelea kuutumikia mpira na timu ya taifa kwa ujumla.
Timu ambayo hajawahi kushinda nayo kitu chochote tangu aanze kuitumikia. Huu ndiyo mtihani mkubwa unaotia hasira kwa Lionel Messi.
Anaonekana kwa sasa ni gwiji kama alivyokuwa gwiji wa nchi hiyo Diego Maradona, lakini kinachowatofautisha ni kushinda taji na timu ya taifa.
Mwenzake aliwahi kufanikiwa kuiongoza Argentina mwaka 1986 leo hii kila jicho linamwangalia Lionel Messi. Yeye ndiye anayeonekana mkombozi katika nyakati hizi ambazo Argentina wanapitia.
Kuna madhara hasi kwa Lionel Messi kuonekana kama ndiye mtu pekee mwenye nguvu kubwa ya kuibeba Argentina?
Hapana shaka kwa sababu timu itamwegemea yeye na kama ikimwegemea yeye na ikitokea akabanwa basi timu haitokuwa na njia mbadala wa kupata matokeo katika mechi ya leo.
Safu ya kiungo ya Ufaransa ndiyo uti wa mgongo wa timu ya taifa ya Ufaransa?
Ukiangalia mabingwa wa kombe la dunia la mwaka 2010 (Hispania) na 2014 (Ujerumani) walikuwa imara zaidi katika eneo la kiungo. Hali hii ipo katika kikosi cha Ufaransa msimu huu kwa sababu ina viungo wa kiwango cha juu kama Kante, Tolliso, Matuidi, Pogba.
Kipi wakifanye Ufaransa ili Lionel Messi asing’are katika mchezo wa leo?
Mara nyingi Lionel Messi hushuka chini katikati kuchukua mipira na kukimbia nayo kuelekea mbele.
Kitu ambacho Ufaransa wanaweza kufanya ni wao kumtumia Kante kumfanya Lionel Messi kutokuwa huru anapokuwa anarudi eneo la katikati.
Kipi wakifanye Argentina waweze kushinda hii mechi?
Kwenye mechi dhidi ya Nigeria , Lionel Messi alionekana kama mtu ambaye hana mzigo mkubwa sana ndani ya timu. Timu ilicheza kwa pamoja, Argentina hawakuwa na lengo moja la kumtengenezea nafasi pekee Lionel Messi.
Kitu hiki wanatakiwa kukifanya kwenye mechi ya leo na Ever Banega kusimama katika eneo la kiungo cha kati ili kutengeneza nafasi za magoli.
Higuain na Di Maria watakuwa na msaada katika mechi hii ya leo?
Di Maria kasi yake imepungua sana ukilinganisha na kipindi cha nyuma vivo hivo kwa Higuain. Hivo kumwanzisha Aguero katika eneo la mbele na kumwanzisha Dyabala eneo la kushoto pembeni kutakuwa na nafasi kubwa kwa Argentina kushinda.
Kwanini nasema hivi? Kwanza Argentina watakuwa na wachezaji wengi ambao wanauwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi kuanzia eneo la katikati ya uwanja mpaka mbele ya uwanja ( Banega, Messi, Dyabala na Aguero).
Safu ya ulinzi ya Argentina vs Safu ya ushambuliaji ya Ufaransa.
Safu ya ulinzi ya Argentina mekuwa inaruhusu magoli mengi hii ni tofauti na safu ya ulinzi ya Ufaransa. Safu ya ulinzi ya Argentina haijafanikiwa kupata clean sheet katika michezo mitatu ya kombe la dunia huku ikifungwa magoli matano mpaka sasa hivi. Inakutana na safu ya ushambuliaji yenye wachezaji ambao ni nyota kama Griezmann , Mbaape.
Utofauti wa umri kati ya wachezaji wa Ufaransa na Argentina unaweza ukaamua mechi hii kwa kiwango gani?
Wachezaji wa Argentina wana wastani wa umri mkubwa ukilinganisha na wachezaji wa Ufaransa hivo hii itakuwa inatoa tafasri moja kuwa wachezaji wa Ufaransa watakuwa na pace (kasi) kubwa kuzidi wachezaji wa Argentina na hii itakuwa na faida kwao kuliko kwa Argentina.