Louis anakwenda kuimarisha klabu ya Simba eneo la pembeni kulia na nyuma ya washambuliaji…
UAMUZI wa uongozi wa klabu ya Simba kumreejsha nyota wake wa zamani Louis Miquissone unapaswa kupongezwa. Winga huyo machachari raia wa Msumbiji ana kila sababu ya kurudi Simba. Timu ambayo ipo katika nafasi nzuri kwa ubora barani Afrika. Timu ambayo inafanya kila juhudi kuwika na kutetemesha vigogo pamoja na kutafuta mataji ya soka Afrika.
Katika mashindano mawili waliyoshiriki Simba, wamefikia ngazi ya robo fainali; Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho. Jitihada za Simba kuyasaka mataji ya CAF kila msimu ni kivutio ambacho kinafaa kumrejesha mchezaji yeyote aliyeondoka. Bahati nzuri ni kwamba Louis Miquissone aliuzwa kwenda Al Ahly baada ya kuonesha umwamba wake kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar Es Salaam alipowatungua bao tamu zaidi.
Nyota huyu anakumbukwa kwa mengi na mashabiki wa Simba. Anakumbukwa na wapinzani wa Simba namna alivyowatia machungu kutokana na kiwango chake, mabao yake, ubora wake na namna alivyo mchezaji wa kitimu. Ana kipaji binafsi lakini pia anajua kucheza kitimu.
Akiwa Simba alishirikiana vizuri na kwa ustadi wa hali ya juu na Cletous Chota Chama na kutengeneza kombinenga kali. Kombinenga hiyo haikuwa hatari kwa Ligi Kuu pekee, bali kwenye mashindano ya CAF pia ilikuwa gumzo. Ni sababu hiyo wakubwa wenye fedha waliwasajili nyota hawa wawili, Louis na Cletous; Ni Al Ahly na RS Berkane.
Naam, sasa nyota wote wawili wapo klabuni. Kwa namna ama nyingine Louis anakwenda kuimarisha klabu ya Simba eneo la pembeni kulia na nyuma ya washambuliaji. Ni mchezaji mzuri kuunganisha eneo la kiungo na washambuliaji. Ni mpishi mzuri na mfungaji wa mabao.
Kumrejesha Louis umefanyika uamuzi bora, kwani unaimarisha kikosi,kuwavuta mashabiki wake, kuongeza msisimko ndani ya timu na Ligi Kuu. Ni nyota ambaye amekuwa akiwavutia wengi, wakubwa kwa wadogo, mabibi na mabwana.
Louis ni mchezaji ambaye kasi yake huwa kielelezo cha ubora wa Ligi Kuu kukaribisha wachezaji wenye viwango vikubwa. Kuondoka kwake Al Ahly ni wakati mwafaka, na kwamba ushindani uliopo kwenye timu ile ni mkubwa hasa ukiwa na baadhi ya wachezaji wanaotoka Ligi za Ulaya kuja kukipiga kwa mabingwa hao wa Afrik,a wakiwa na uzoefu na wasifu mkubwa kuliko Miquissone.
Kama alivyowahi kusema Mbwana Samatta, mchezaji anayenunuliwa kwa fedha nyingi hulazimika kupangwa kila mechi ili kuhalalisha bei aliyonunuliwa. Mchezaji huyo bila kujali mengine, anatumika kama kielelezo na kuhalalisha bei yake.
Kwa hiyo Louis asingeweza kupenya mbele ya Percy Tau mwenye uzoefu wa Ligi Kuu England, na akiwa analipwa fedha nyingi zaidi ndani ya kikosi cha Al Ahly. Licha uwezo wake, pia angeweza kupisha nyota wengine, lakini fedha anayolipwa lazima ihalalishe kupangwa kila mechi.
Ujio wa Louis Miquissone unaweza kuinua ari ya timu, kuongeza kasi na ushindani mkali katika safu ya ushambuliaji. Inakwenda kuwaimarisha akina Kibu Dennis, Peter Banda na Cletous Chama mwenyewe pamoja na Jean Beleke anayetarajiwa kuongoza safu hiyo.
Kwa vile Simba wamekuwa wakifunga mabao mengi na kutokea kila upande, ni wazi Louis Miquissone analeta mabao mengine kwenye kapu la Simba. Uimara na ubora wa wachezaji unatokana na wanaoshindana nao. Mchezaji anayekalia benchi kwa sababu ya kuzidiwa na mwenzake anayepangwa kikosi cha kwanza, maana yake Yule aliyepo benchi apewe maua yake kwani ndiye anachangia kuimarika na kuoneshwa ubora kwa mwenzake. Ushindani wanaotoa ndiyo matokeo ya ubora wa wachezaji wengine kikosini.
Tunapaswa kukiri kuwa hata wachezaji wa nje kutamani kurudi kucheza Ligi Kuu ni kutokana na mapenzi yao kwa mashabiki na namna wanavyoishi. Ni wazi tamaa yao kurudi kucheza Ligi Kuu ni ishara ya kuamini ndipo mahali walipotengeneza majina yao kisoka na wangependa kupatumia ili waweze kukua zaidi. Wanaamini ndipo mahali ambapo wanaweza kutupamia ‘kutoboa’, kwa maana ya kuonwa na ksuajiliwa na timu kubwa kwa vile macho ya timu hizo yapo Ligi Kuu.
Mashabiki fulani wa soka wa Zambia waliwahi kuniambia kuwa Ligi Kuu mwanzoni ilikuwa na fedha nyingi lakini haikuwa imepiga hatua. Kwa sasa wamebadili kauli tangu Cletous Chama aliposajiliwa moja kwa moja na RS Berkane na Louis Miquissone kwenda Al Ahly, wanasema Ligi Kuu ni eneo jingine lenye fursa kwa wachezaji si Afrika mashariki pekee bali Afrika na kwamba ni mahali wanapoweza kupatumia kuonwa na timu kubwa. Fursa ya mashindano ya kimataifa imezileta timu kubwa kupambana na timu za Ligi Kuu hivyo kuona umwamba wake na kuamua kuwasajili nyota wao.
Kwahiyo Ligi Kuu inapomkaribisha Louis Miquissone maana yake inakwenda wengi wanatarajia ufalme ule alioutengeneza utarudi tena. Kwa hakika ana deni kubwa kwa mashabiki wenye matumaini naye. Ama kuna mwana Simba ambaye hapendi kushuhudia utamu wa miguu ya Louis Miquissone? Wacha Ligi Kuu ianze.