Blatter awageukia Ufaransa, Ujerumani
Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter amedai kwamba siasa zilitumika kabla ya mchakato wa kupata wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2018 na 2022.
Blatter aliyeahidi kuachia ngazi baadaye mwaka huu licha ya kuchaguliwa kwa kipindi cha miaka minne ijayo, amedai kwamba Ufaransa na Ujerumani zilijiingiza kwa nguvu kupitia kwa marais wao.
Anadai kwamba mwaka 2010 rais wa Ufaransa aliyepita, Nicolas Sarkozy na mwenzake wa Ujerumani, Christian Wulff walijaribu kutia ushawishi wao kabla ya Qatar na Urusi kushinda kwenye kura za uenyeji kwa miaka hiyo.
Blatter (79) anasema kwamba haoni tatizo lolote juu ya ukweli kwamba Qatar kuchaguliwa kuwa wenyeji japokuwa hivi sasa vyombo vya dola vya Uswisi vinachunguza mwenendo wa mchakato huo kubaini iwapo mlungula ulitumiwa.
Uamuzi wa Blatter kujiuzulu unatokana na shirikisho hilo kunuka rushwa, ambapo maofisa wake waandamizi saba na wengine wa zamani au wanaohusiana nalo wameshakamatwa na kufunguliwa mashitaka, ambapo wale saba waliodakwa jijini Zurich wanasubiriwa kupelekwa Marekani kupanda kizimbani.
“Kabla ya fainali za Kombe la Dunia kutolewa kwa Urusi na Qatar, viongozi wawili wa kisiasa waliingilia nao ni Sarkozy na Wulff waliojaribu kuwashawishi wapiga kura,” anasema Blatter akiongeza kwamba hata Chama cha Soka cha Ujerumani (DFB) kilipokea maelekezo kwamba wawapigie Qatar kutokana na maslahi ya kiuchumi.
“Zitasame kampuni zote za Kijerumani – Deutsche Bahn (kampuni ya reli) Hochtief (ujenzi) na nyingine nyingi tayari zilikuwa na miradi Qatar kabla ya uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia kutolewa kwa nchi hiyo.
“Hii ndiyo sababu tuna Qatar kama wenyeji wa fainali hizo. Mie nafanya kazi kwa kanuni za uongozi. Iwapo wajumbe wengi zaidi wa kamati ya utendaji wanataka Kombe la Dunia lifanyike Qatar nawajibika kukubaliana nao,” anaongeza.
Rais wa zamani wa DFB, Theo Zwanziger awali anadaiwa kwamba alipata kumwandikia Rais Wulff kumuuliza juu ya uwezekano wa Qatar kuwa mwenyeji, lakini anakana kwamba kulikuwa na ushawishi wowote.
Blatter ameeleza kwamba dhamira yake ipo safi, si mla rushwa na kwamba yeyote anayemwita hivyo anatakiwa kutupwa jela. Majuzi Blatter alitokea na kusema kwamba hajajiuzulu nafasi yake na kwamba anaendelea kuchapa kazi kama kawaida.
Inatarajiwa kwamba atajiuzulu kwenye mkutano maalumu utakaoitishwa baadaye, lakini awali alisema lazima muda wa kutosha utolewe kupata viongozi wazuri. Inadaiwa kwamba ana nia ya kubaki madarakani lakini wiki iliyopita alionywa kwamba asibadili mawazo bali aondoke kupisha wengine