Menu
in , , ,

UENYEJI KOMBE LA DUNIA QATAR

Mpasuko kisiasa na kisheria wanukia

 
Uamuzi wa kubadili majira au uenyeji wa Kombe la Dunia 2022 kutoka Qatar au la unatarajiwa kusababisha mpasuko mkubwa.

Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa mapema mwezi ujao utasababisha mpasuko kisiasa na kisheria lakini pia wazo la kuondosha kabisa mashindano hayo Qatar limeanza kuchukuliwa kama chuki dhidi ya Uarabu.

Qatar imepangwa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, lakini wadau wengi wanaeleza wasiwasi wao kutokana na hali ya hewa, kwani jotoridi katika majira ya kiangazi hupanda hadi nyuzi zaidi ya 50 za sentigredi.

Suala hili limezua mjadala ambao unahusisha siasa na michezo, ambapo tayari Rais wa Fifa, Sepp Blatter ameshasema wanachama wanane wa Ulaya walitumia siasa katika uamuzi wa kuipendelea Qatar.

Kati ya wanachama 24 wa Kamati ya Utendaji ya Fifa, 14 waliunga mkono kombe kuchezwa Qatar, na wanane kati yao wanatoka Ulaya.

Leo hii wadau kadhaa wameanza kusema ilikuwa makosa kupanga mashindano hayo kufanyika Qatar, lakini taifa hilo dogo kijiografia la Mashariki ya Kati linashikilia kwamba limekidhi vigezo vyote vya kuandaa mashindano hayo.

Oktoba 4 na 5 mwaka huu patafanyika kikao kizito cha kamati ya utendaji ya shirikisho hilo la soka la kimataifa, kuangalia haja ya kuhamishia mashindano hayo msimu wa baridi ili kutoathiri afya na ufanisi wa wachezaji.
 
 
ARSENE WENGER HATAKI MABADILIKO
 
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger ambaye wachezaji wake na wengine wanaocheza Uingereza wanatarajiwa kushiriki mashindano hayo anasema haoni sababu ya kubadili tarehe.
Wenger ambaye ndiye kocha anayeendelea kufundisha klabu moja kwa muda mrefu kuliko wengine wote Uingereza, anasema Fifa wanatakiwa kusimamia uamuzi wao wa mwanzo.

Wenger anajulikana kwa uhafidhina hivyo kwamba kwa miaka kadhaa ameshikilia falsafa yake ya kutumia wachezaji wadogo na kutotumia fedha nyingi kusajili wachezaji.

Hata hivyo, Wenger ambaye msimu huu amevunja rekodi ya klabu kwa kutumia zaidi ya pauni milioni 40 kusajili mchezaji mmoja, anasema ana hofu juu ya athari ya joto kwa wachezaji na washabiki, lakini anasema uamuzi umeshafikiwa hauwezi kubadilishwa.
 
TEKNOLOJIA YA KUPOOZA HEWA VIPI?
 
Qatar ni taifa la kwanza la Kiislamu na la Mashariki ya Kati kupewa uenyeji wa Kombe la Dunia na linasema lina teknolojia ya kisasa ya kupooza hewa, ambayo katika ngazi ya ukubwa wa mashindano hayo, ni mara ya kwanza kujaribiwa, hivyo ni hatari.

Teknolojia hiyo ambayo hutumiwa katika maeneo madogo madogo inatarajiwa kujaribiwa baada ya Qatar kukamilisha moja ya viwanja tisa vitakavyotumiwa, na hiyo itakuwa 2015/16.
Kuna uwezekano pia wa kufunguliwa masuala ya kisheria kwa ajili ya kutaka shinikizo la kuhamisha michezo hiyo.
 
MSUGUANO WA KISHERIA WANUKIA
 
Kadhalika inaelekea msuguano utapamba moto baina ya Blatter na Mkuu wa Uefa, Michel Platini anayetaka kuchukua nafasi ya Blatter kwenye uchaguzi mkuu wa 2015. Platini anataka mashindano hayo yafanyike majira ya baridi.

Mkuu wa Chama cha Soka cha Australia, Frank Lowy, ambaye nchi yake ilishindwa na Qatar katika dau la kuandaa kombe hilo, anaonya juu ya kuhamisha tarehe za mashindano, akisema ni sawa na kubadiloi kanuni baada ya mchezo kumalizika.

Low anaapa kufungua shauri la kisheria ili kudai kurejeshewa fedha za walipa kodi wa Australia zilizopotezwa, kwani itadhihirisha kwamba Qatar haikuwa na uwezo wala sifa za kuandaa mashindano hayo majira ya joto.

Kuna uwezekano wa wadhamini wa Fifa na watangazaji walionunua haki za matangazo kwa mabilioni ya dola kufungua kesi kutaka kurejeshewa fedha zao.

Kituo cha Televisheni cha Fox na kituo cha Telemundo kinachotangaza Kihispaniola walilipa dola bilioni moja kwa ajili ya haki za televisheni za Marekani, kiasi ambacho ni kikubwa kuliko ambacho wangelipa Bodi ya Ligi ya Taifa ya Soka ya Marekani (NFL).
 
SIASA NAYO INACHANGIA HAYA?
 
Kana kwamba yote yaliyoainishwa awali hayatoshi, madai ya Rais Blatter kwamba wajumbe wanane wa Ulaya walitumia siasa kuipa haki Qatar yanawasha moto.

Blatter anadai palikuwa na shinikizo la kisiasa, vinginevyo uamuzi tofauti ungefikiwa na wajumbe wa kamati ya utendaji, na 2022 Kombe la Dunia lingefanyika nchi tofauti kabisa.

Mtoto wa Platini ni mwanasheria wa kampuni ya michezo inayomilikiwa na Serikali ya Qatar – Qatar Sports Investments (QSI), ambapo Platini alikuwa mjumbe wa kwanza kusema aliipigia kura Qatar ili iandae mashindano hayo.

Hata hivyo, Platini anakanusha madai kwamba alifikia uamuzi huo kutokana na shinikizo au ushawishi wa kisiasa.

Hata hivyo, wengi wanaamini Platini alishawishiwa kwa namna fulani katika dili la pande tatu, wakati Nicolas Sarkozy akiwa Rais wa Ufaransa, ambaye ni rafiki mkubwa wa Emir wa zamani wa Qatar, Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani. Platini ni Mfaransa.

Katika dili hilo, QSI iliinunua klabu ya Paris St. Germain (PSG), ambayo Sarkozy ni mdau mkubwa kwa sharti la QSI kuingia na kuwekeza zaidi kimichezo nchini Ufaransa.

Hapo hapo, mtandao wa Kituo cha Televisheni cha Serikali ya Qatar cha Al Jazeera kingepewa haki ya kurusha Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) huku Ufaransa ikitia shinikizo Qatar iwe mwenyeji. Dili hilo lilifanyika Ikulu ya Elysée jijini Paris.

Alipohojiwa wakati huo, Balozi wa Qatar nchini Ufaransa, Mohamed Al Kuwari, alisema walikuwa na maslahi ya kuwekeza Ufaransa, kuwa na ubia na kusonga maeneo mengine kama Afrika na Asia na kuwa na ushirika na kampuni kama Total, Vinci na Veolia.

Hadi sasa uenyeji wa Kombe la Dunia haujaipa Qatar hadhi iliyotarajia, kwa sababu sasa inazungukwa na kashfa hizo za kupanga uenyeji na sasa si ajabu msuguano wa kisheria ukawavurugia zaidi.

Wafanyakazi wengi nchini Qatar, kwa asilimia 94 ni wa kigeni na pia ni taifa lenye wakazi wengi wasiokuwa raia.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version