UEFA kushukia klabu ‘korofi’
Wachezaji wa klabu za soka barani Ulaya wataadhibiwa ikiwa klabu zao zitakiuka kanuni za haki kuhusu fedha.
Umoja wa Vyama vya Soka la Ulaya (UEFA) unafikiria hata kufikia kusimamisha wachezaji, ikiwa klabu zao zinashindwa kufuata kanuni na taratibu za fedha.
Kuna kitu kilichozoeleka zaidi Ulaya kama FFP (Financial Fair Play), ambapo Rais wa UEFA, Michael Platini anasema kitatumiwa hata kwa vituo vya televisheni.
Hatua hii inakuja wakati zawadi za klabu 23 zilizoshiriki kwenye mashindano mbalimbali kwa 2012-13 zikishikiliwa, kwani uchunguzi dhidi yao unaendelea.
Platini, inavyoelekea, anafanya kile ambacho alipata kusema awali kwamba angefanya, kuhakikisha panakuwapo nidhamu kwenye soka ya Ulaya.
“Kwanza ni kuzuia fedha za zawadi zao (klabu), kitakachofuata ni kuzuia fedha za vituo vya televisheni na baada ya hapo itakuwa kusimamisha wachezaji waliosajiliwa ndani ya dirisha la mwaka mmoja nyuma.
“Mwisho kabisa UEFA itatoa adhabu kali zaidi, pengine kuzifuta baadhi ya klabu zilizotia hasara (nje ya viwango vilivyokubaliwa) kwenye mashindano ya Ulaya,” ndizo habari za ndani ya UEFA zinavyosema.
Asubuhi ya Jumanne wiki hii, chombo hicho kinachosimamia soka ya Ulaya, kilibainisha juu ya matakwa mapya ya awali ya FFP.
Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo, ni kwamba klabu zote zinazoshiriki kwenye mashindano yanayosimamiwa na UEFA lazima zitoe taarifa kuhusu hali yao ya kifedha, ikiwa ni pamoja na madeni yasiyolipwa hadi Juni 30 mwaka huu.
Chombo cha Uchunguzi na Udhibiti wa Fedha za Klabu (CFC) kilicho chini ya UEFA kimeshakutana na kutoka na orodha ya mashauri 23.
Katika hayo, klabu husika zinadaiwa na ama klabu nyingine, waajiriwa wake, mamlaka au mashirika ya kodi na mamlaka nyinginezo, jambo ambalo ni doa.
Uchunguzi dhidi ya klabu hizo unaendelea, ambapo zenyewe zimetakiwa kuwasilisha taarifa iliyohuishwa kuhusu hali zao ifikapo mwisho wa mwezi huu wa Septemba.
Katika hali hiyo, UEFA imeamua kuzuia fedha za zawadi hadi hapo malipo yote yaliyolimbikizwa yaliyobainiwa na wapelelezi yatakapolipwa au CFC kutoa uamuzi tofauti.
CFC inaongozwa na mtu mzito, Waziri Mkuu wa zamani wa Ubelgiji, Jean-Luc Dehaene. Waziri mkuu huyo mstaafu ndiye aliyebainisha klabu zilizolimbikiza malipo.
Moja ya hizo ni Atletico Madrid, ile iliyoikung’uta Chelsea mabao 4-1 katika mchezo wa Super Cup wa UEFA majuzi. Ipo pia klabu nyingine ya Hispania, Malaga.
Klabu nyingine zilizoangukia kwenye tuhuma hizo za kashfa ya madeni ni FK Borac Banja Luka, FK Sarajevo na FK Zeljeznicar, zote za Bosnia & Herzegovina.
Nyingine katika kikaango hicho ni PFC CSKA Sofia ya Bulgaria, HNK Hajduk Split na NK Osijek, zote za Croatia.
Nyingine ni Maccabi Netanya ya Israel, FK Shkendija 79 ya Macedonia, Floriana FC ya Malta, FK Buducnost Podgorica na FK Rudar Pjevlja, zote za Montenegro.
Nyingine zinazokabiliana na makucha ya UEFA katika hili ni Ruch Chorzow ya Poland, Sporting Clube de Portugal ya Ureno, Dinamo Bucharest,
FC Rapid Bucharest na FC Vaslui za Romania.
Zaidi zinazotakiwa kuchomoa kwenye kadhia hii ni
Rubin Kazan ya Urusi, FK Partizan na FK Vojvodina za Serbia na Eskisehirspor na Fenerbahce za Uturuki.
Katika orodha hiyo hakuna klabu ya Uingereza iliyo kwenye uchunguzi. Hata hivyo, tayari klabu za Ligi Kuu ya England (EPL) zilishajadili suala hilo, zikitaka kuwa na kibano chao zenyewe kuhusu FFP.
Wadau wengi waliweka uzito, wakitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya klabu zitakazoshindwa kuheshimu kanuni za fedha, lakini pia wakataka kuweka kiwango cha mwisho cha juu cha mishahara.
Itakuwa juu ya klabu zenyewe kuamua mfumo uendeje na adhabu gani zitolewe. England ina klabu saba katika michuano ya Ulaya.
Inadaiwa kwamba, klabu zinataka kuunganisha nguvu, ili kutoruhusu wachezaji na mawakala wao kujipatia nyongeza kubwa kupindukia za mishahara.
Vigezo vya mishahara ni baadhi ya vinavyofuatwa na vituo vya televisheni katika kutoza fedha za kurusha matangazo ya michuano moja kwa moja katika sehemu mbalimbali za dunia.
Hata hivyo, kama ilivyotarajiwa, klabu tayari zimegawanyika kwenye makundi mawili, katika suala la kuweka ukomo wa juu wa mishahara.
Hili linakuja wakati pamekuwa na mishahara mikubwa ya kutisha kwa wiki kwa baadhi ya wachezaji, huku klabu nyingine bado zikifikiria kuwasajili nyota zaidi kwa kuvunja rekodi ya mishahara iliyopo.
Manchester City ni moja ya klabu zinazodaiwa kutopenda kuwekwa ukomo wa kiwango cha mshahara kwa mchezaji, wakati upande wa pili inatajwa klabu ya West Ham inayotaka kuwekwa ukomo.