Menu
in ,

UCHAMBUZI WA MAKUNDI YA AFCON.

Tanzania Sports

GROUP A

GABON.

Hawa ndiyo wenyeji wa mashindano haya. Unaweza mwangalia Pierre-
Emerick Aubameyang katika jicho la maendeleo zaidi.

Lakini kuna vitu ambavyo vinatia shaka kwa Gabon.

Cha kwanza wamemteua kocha wao mwezi mmoja kabla ya mashindano. Na
kibaya zaidi ametoka kwenye mpira wa China na hajawahi kufundisha soka
la Africa.

Hii inaweza ikampa ugumu kwa namna mbili, moja ugeni wa kikosi wa
kikosi ambacho amekabidhiwa mwezi mmoja uliopita, pili ugeni wa soka
la Africa pia inaweza ikawa kikwazo kwake.

Gabon kwenye mechi 13 zilizopita ameshinda mechi 2.Hii inaonesha
wanapitia wakati mgumu sana katika kupata matokeo.

Mwaka 2013 hawakufuzu kwenda mashindano ya Afcon lakini mwaka 2015
walifuzu na wakaishia hatua ya makundi.

Mara ya mwisho kuandaa mashindano haya waliishia robo fainali. Mwaka
huu pia Uwenyeji unaweza ukawabeba ukiachana na mchango mkubwa wa
Pierre-Emerick Aubameyang. Wana nafasi kubwa ya kufuzu kwenye hatua
ya makundi.

CAMEROON

Sahau kizazi cha kina Eto’o , kuna kizazi kipya kinatengenezwa muda
huu kwenye nchi ya Cameroon.

Wamefuzu kwenye michuano hii bila kupoteza hata mchezo mmoja kutoka
kwenye kundi lililokuwa gumu lenye timu za Afrika kusini, Mauritania
na Gambia.

Kitu kikubwa ambacho kitawateteresha na kuwafanya wasifike mbali
kwenye mashindano haya ni kuwakosa nyota wake kama Matip ( Liverpool),
Nyom ( Westbrom), Onana( Ajax), Assembe ( Nancy).

BURKINAFASO.

2010, 2012 na Mwaka 2015 walikomea Kwenye hatua ya makundi ya mashindano haya.

Mwaka 2013 waliishia nafasi ya pili. Kitu kikubwa ni kurejea kwa kocha
wao Paulo Duarte ambaye walikuwa naye kuanzia mwaka 2008-2012.

Burkinafaso walikuwa hawakosi kushiriki michuano hii kwa sababu timu
yao ilikuwa imejengwa na Paulo. Kurejea kwao kutakuwa msaada mkubwa
sana kwao kwa sababu siyo mgeni wa timu hii.

GUINEA BISSAU.

Wamefuzu kwa mara ya kwanza, habari kubwa kwao siyo kufuzu kwa mara ya
kwanza ila habari kubwa ni kundi ambalo walikuwepo mpaka wakafuzu
michuano hii.

Congo ni wanarobo fainali wa mashindano yaliyopita, wakati Zambia
walikuwa mabingwa wa mwaka 2012 lakini waliweza fuzu mbele yao. Kwangu
mimi Guinea Bissau ndiyo itakuwa Suprise package katika mashindano
haya.

KUNDI B.

ALGERIA.

Hili ndilo kundi gumu kwangu na bingwa wa michuano hii atatoka kwenye
group hili.

Algeria wanavipaji vingi sana kama kina Mahrez, Slimani ( wote
wametoka Leicester city) .Brahimi( Fc Porto), Bentaleb ( Schalke 04).
Hiki ndicho kizazi cha dhahabu kwao. Mashindano yaliyopita waliishia
robo fainali.

TUNISIA.

Kwenye mashindano 7 wamefika robo fainali mara 5.

Uwepo wa Algeria kwenye group hili unatengeza mechi nzuri sana dhidi
ya Tunisia na hii ni kwa sababu timu zote zimetoka Africa Kaskazini.
Siku zote timu za Africa Kaskazini zinapokutana huwa kuna upinzani
mkubwa.

Kwenye michezo 13 iliyopita Tunisia wameshindwa mechi moja tu, hii
inaonesha ni timu ambayo ni mshindi.

SENEGAL.

Kipi unakumbuka kuhusu Senegal? Mimi kila ikitajwa Senegal jina la
nchi ya Uturuki huwa linakuja kwenye kichwa changu.

Wanarobo fainali wa kombe la dunia mwaka 2002 . Unakumbuka kizazi cha
kina Alhaji Diouf?

Tayari kizazi hicho kimeshakufa, na muda huu kuna kizazi cha kina Mane
( Liverpool ), Kouyate( Westham), Diame.

Hawajawahi kushinda kombe hili. Wanakikosi kizuri sana Msimu huu. Kazi
kubwa kwao ni kufuzu kundi hili, walifanikiwa kufuzu wana nafasi kubwa
ya kwenda mbali.

ZIMBABWE

Wamefuzu kwa mara ya pili. Tayari bundi limeshaanza kuingia kwao.

Wachezaji walianza kugomea baada ya kucheleweshewa malipo yao na kudai
pesa za motisha.

Hii kwa kiasi kikubwa kinaweza kuwatoa kwenye mchezo na ikizingatia
wapo group gumu inaweza ikawa ngumu kwao kupita.

GROUP C.

IVORY COST.

Kuna vitu vingi sana vimebadilika sana kwenye kikosi cha Ivory Cost.
Kizazi cha dhahabu cha kina Drogba, Toure kimeshapita. Kocha wao
Herve Renard ameshaondoka pia.

Herve Renard alikuwa mtu muhimu sana katika kuunganisha vipaji vya
timu ya taifa ndiyo maana aliisaidia kuchukua ubingwa wa mwaka 2015.

Imefika fainali 3 katika mashindano 6 yaliyopita. Huwezi ipuuza hata
kama kuna mabadiliko.

MOROCCO.

Herve Renard alishinda kombe hili akiwa na Zambia na Ivory Cost. Sifa
kubwa ya Renard ni kuunganisha vipaji kwenye timu na kutengeneza timu
imara ya ubingwa.

Ndiyo maana katika michezo 13 iliyopita Morocco hajafungwa hata mechi moja.
Tayari Renard ameshatengeneza timu imara. Naipa nafasi kubwa sana
Morocco katika mashindano haya.

DR CONGO.

Mashindano yaliyopita walikuwa washindi watatu. Mashindano haya
wanaingia bila ya nyota wao Bolasie. Mtihani mkubwa walionao ni
kumfunga mmoja kati ya Morroco au Ivory Cost.
TOGO.
Mashindano yaliyopita hawakuwepo.

Hawana kikosi imara cha kutisha, wamekuwa hawana mwendelezo mzuri wa
kiwango chao.

GROUP D.

GHANA.

Pamoja na wakati mgumu wanaopitia, wamecheza mechi 5 bila ushindi.

Ila wanakikosi kizuri cha wachezaji kama kina Jordan na Andre Ayew.

Mashindano yaliyopita waliishia nafasi ya nne.Watamkosa Asmoah Gyan
mwanzoni mwa mashindano haya.

MISRI.

Kufa kwa kikosi bora kilichochukua kombe mwaka 2006, 2008 na 2010.
Taratibu Misri imeanza kuwekeza kwa vijana.

Mohamed Salah anarudi tena baada ya kukaa nje Kwa muda wa wiki tatu.

MALI.

Mashindano yaliyopita walikomea hatua ya makundi. Mashindano ya mwaka
2012 na 2013 waliishia nafasi 3.Kikosi chao hakijabadilika sana,
nawapa nafasi kubwa kwenye mashindano haya. Ni Suprise package yangu
nyingine.

UGANDA.

Walishiriki mara ya mwisho Mwaka 1978.Ni fahari ya Africa Mashariki kwa sasa.

Tuzo ya timu bora ya Africa inaweza ikaongeza morali kwenye kikosi chao.

Lakini kwangu mimi siwapi nafasi kubwa ya kufika mbali.

Na Martin Kiyumbi.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version