Menu
in , , ,

Uchaguzi wa TFF: Nini sababu ya mizengwe?

WAKATI tarehe ya uchaguzi wa TFF, Oktoba 26,2013, ikizidi kusogea, mizengwe haijauachia mchakato wa uchaguzi huo. Kuna watu waliondolewa kwenye kugombea nafasi za urais na ujumbe. Swali la msingi sana tunalopaswa kujiuliza ni kwamba mizengwe hii ni ya kulinda hadhi na maendeleo ya mchezo wa soka nchini au ni chuki tu miongoni mwa wadau wa soka wa Tanzania ama kuwaogopa watu fulani wasiwemo kwenye uongozi wa soka nchini kutokana na misimamo yao isiyoyumba kuhusu madudu kwenye uendeshaji na utawala wetu wa soka?

Mambo mawili yanatia mashaka kuhusu mizengwe hiyo; kwanza, sababu za kuzuia watu fulani kugombe uongozi kuwa mbali na soka ya uwanjani na pili kutojulikana ukomo wa muda wa tuhuma za wazuiwa hao kwa siku za usoni ili wakati huo waweze kugombea uongozi wa soka nchini.

Siku hizi kuna silaha moja kubwa ya kuwaengua watu kwenye kugombea uongozi wa soka Tanzania. Silaha hiyo ni ya kukosa uzoefu wa uongozi wa soka. Huu ni uongozi na si uchezaji soka. Hivi mtu kama kaongoza taasisi kubwa kama kitivo cha chuo cha elimu ya juu kinachotoa wasomi wa digrii, anapenda na anajua soka, huyu unamuondoaje kugombea uongozi wa soka dhidi ya yule aliyeongoza Yanga na Simba kwa kushindwa kuzipa mafanikio? Chukua mfano wa Profesa Sospeter Muhongo. Alicheza soka mkoani Mara kwa mafanikio akiwa mlinzi na anaongoza wizara nyeti na ngumu ya nishati na madini lakini akiomba uongozi TFF ataambiwa hana uzoefu! Imekaaje hii? Uzoefu huu ni wa kuongoza soka au wa kutengeneza fitna za soka?

Mawazo mapya na mipango mipya ya kisoka vitapatikana vipi namna hii Tanzania kama kuna juhudi za wazi za kufanya soka iongozwe na watu wale wale walioshindwa huku mwanya ukizibwa kwa wenye mawazo mapya kuingia uongozini? Tazama kichekesho hiki; kuna mgombea mmoja wa uwakilishi wa kanda ya Dar es Salaam, Shaffih Dauda, mwanahabari mwajiriwa wa Clouds FM alizuiwa kugombea eti kwa sababu alichapisha kwenye blog anayomiliki barua toka Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) kwenda TFF ya maelekezo ya nini cha kufanywa baada ya mchakato wa awali wa uchaguzi kuvurugika kwa sababu hizi za mizengwe mizengwe. Barua hiyo ambayo haikuwa ya siri iliyomponza Dauda ilitoa maagizo yafuatayo:-

1. Kuunda vyombo sahihi (Kamati ya Maadili itakayokuwa na vyombo viwili ambavyo ni cha kutoa maamuzi ya awali na cha rufaa) ambavyo mamlaka yake yatakuwa ni kushughulikia masuala ya ukiukwaji wa maadili;

1. 2. Kufanya mabadiliko ya katiba kwa kuzingatia uundwaji wa vyombo hivyo;
1. 3. Kuanza upya kwa mchakato wa uchaguzi wa Kamati ya Utendaji kwa kufungua milango kwa wagombea ambao walishachukua fomu na wagombea wapya:

4. Shughuli hiyo ikamilike ifikapo tarehe 30 Oktoba 2013.
M Maswali hapa ni mawili; kwanza, kitu gani kilichowakera sana TFF kwa kuchapishwa kwenye blog barua hiyo isiyo ya siri ambayo maudhui yake yalishawekwa hadharani na TFF wenyewe kwa wananchi kupitia vyombo vya habari? Pili, huyo mwanahabari Shaffih Dauda alitakiwaje awajibike kwa TFF badala ya kwa wasomaji wa habari zake wakati yeye alifanya aliyoyafanya akiwa si kiongozi wa TFF bali mtoa habari? Jibu hapa ni moja tu kwamba Dauda anaogopwa kwa sababu ni mkosoaji. Tutaendeleaje namna hii kwa kuwaogopa wafichua madudu?

Unaweza kupumbazwa kwamba maamuzi ya kuwaengua wagombea fulani fulani ni maamuzi huru yanayofanywa na vyombo huru vya TFF visivyoingiliwa kama Kamati ya Maadili na kamati zake mbili za rufani.Hakuna kitu hapo.Majuzi Kamati ya Rufani ya TFF inayoongozwa na Mwanasheria Jesse Mguto iliwarudisha kwenye kugombea watu saba waliondolewa kugombea nafasi mbalimbali kwa sababu tofauti tofauti. Watu hao ni Richard Rukambura,Omar Abdulkadir,Wilfred Kidau, Riziki Majala,Kamanga Tambwe,Nazarius Kilungeja na Shaffih Dauda.

Bila aibu TFF imetoa kauli ya kuonesha kutoridhika na maamuzi hayo na kamati yake ya utendaji inafikiria kukata rufani dhidi ya uamuzi huo wa chombo huru! Vyombo hivyo vinakuwaje huru kama TFF inayapokea kwa furaha maamuzi ya kuengua wagombea lakini ikiyachukia maamuzi ya watu hao kupewa nafasi ya kugombea? Uchaguzi una kamati zake, inakuwaje kamati ya utendaji ya TFF ichukue upande kwenye masuala ya uchaguzi?

Hebu tubadilike jamani. Tuache yeyote mwenye uwezo wa kuongoza soka yetu aongoze ili mradi tu awe na sifa za kufanya hivyo na asiwe na kashfa kubwa za kimaadili na za kiwango chochote zinazohusiana na mchezo wa soka. Tutafakari hayo huku tukijiuliza nini sababu za mizengwe ya uchaguzi na nini faida zake kwa soka yetu?

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version