Tangu kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzanua Bara 2020/2021 jumla ya viwanja vitano vya soka vimefungiwa kutumika kwenye mashindano ya Ligi hiyo kutokana na kasoor mbalimbali. Inafahamika kuwa mchezo wa soka ni biashara na burudani. Katika biashara kuna faida na hasara, na burudani pia inazo faida na hasara zake.
Viwanja vingi vya mchezo wa soka vimekuwa na hali ya inayofanana kwa miaka mingi sasa. Hali ya viwanja hivyo imechangia kuwa sababu za kufungiwa mara kwa mara. Hata hivyo matatizo yanaelekea kujirudia rudia na kusababisha adhabu kutolewa kwa viwanja vile vile ambavyo vinalalamikiwa na wadau wa soka. Je kwanini hali hiyo imekuwa ikijirudia?
Mara kadhaa tumearifiwa juu ya ubovu wa viwanja wa mpra wa Kikapu au mpira wa pete. Hata hivyo uchunguzi unaonesha suala hilo limekuwa sugu sasa. Je, ni kwanini hali iwe hivyo? Hayo ndilo swali la kupatiwa majibu kwa maslahi ya maendeleo ya michezo.
Kwa mfano, hivi karibuni Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara imefungia viwanja mbalimbali vya soka. Bodi hiyo ilieleza kuwa uchakavu katika maeneo ya kuchezea,ulinzi na vigezo vyote muhimu kulingana na shirikisho la Soka nchini TFF, Afrika na FIFA.
Viwanja hivyo vimefungiwa kutumika katika mashindano kutokana na kukosa baadhi ya sifa za kikanuni kama zilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 7 inayozungumzia Uwanja na sheria namba moja ya mpira wa miguu inayozungumzia hadhi ya uwanja wa kucheza katika mashindano ya mpira wa miguu.
Kutokana na uamuzi huo Bodi ya Ligi iliamuru timu ya Polisi Tanzania kutumia uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha kwa ajili ya mechi zake za nyumbani katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Uamuzi huo unaenda sambamba na Kamati ya Leseni kufanya ukaguzi wa viwanja vyote vinavyotakiwa kutumika kwenye mashindano ya Ligi.
Baadhi ya viwanja vilivyokumbana na rungu la Bodi; Septemba 11, mwaka huu wa 2020 Bodi ya Ligi Kuu ilifungia uwanja wa Gwambina mkoani Geita kuchezwa mechi zozote za mashindano kutokana na eneo lake la kuchezea kutokidhi viwango vinavyoainishwa. Kutokana na uamuzi huo, Gwambina walishauriwa kutumia uwanja wa Nyamagana au CCM Kirumba vya jijini Mwanza kwa ajili ya mechi zake za nyumbani.
Septemba 13 mwaka huu wa 2020 uwanja wa Karume uliopo mkoani Mara na ambao umekuwa ukitumiwa na timu ya Biashara United kama uwanja wake wa nyumbani
ulifungiwa kutokana na eneo lake la kuchezea na vyumba vya kubadilishia nguo kutokidhi viwango vilivyoainishwa kikanuni. Kutokana na uamuzi huo Biashara United ilielekezwa kutumia uwanja wa Nyamagana au CCM Kirumba.
Bodi ya Ligi wakati inafungia uwanja wa Karume ilitoa siku 21 kwa wahusika kufanya marekebisho yaliyosababisha kufungiwa kwa uwanja huo.
Aidha, Septemba 27, mwaka huu wa 2020 Bodi ya Ligi ilifungia uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro kuchezewa mechi za mashindano ya Ligi hadi marekebisho yatakapofanyika. Sababu za kufungiwa uwanja huo zilitajwa kuwa; ubovu wa eneo la kuchezea (pitch), vyumba vya kubadilishia nguo na sehemu ya kukaa wachezaji wakati mchezo ukiendelea.
Desemba 25, 2019 viwanja vinne vilifungiwa; Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Hivyo basi kufungiwa tena mwaka huu tena viwanja vilevile ni jambo linashangaza. Adhabu ya mwaka jana hadi mwaka huu bado ni za aina ileile. Hata hivyo hakuna mabadiliko.
WAMILIKI WAFANYE NINI?
Taarifa zinasema asilimia kubwa ya umiliki wa viwanja vya michezo nchini ni Chama cha Mapinduzi. Kimsingi wamiliki wanataka mapato ili kuendesha uwanja. Wamiliki wa viwanja vingi ni nchini wanalaizmika kukodisha kwenye sherehe mbalimbali nje ya michezo.
Mara kadhaa tumesikia Chama cha Mapinduzi wakikiri kuelemewa gharama za uendeshaji kwani mapato yatokanayo na mechi mbalimbali hayakidhi mahitaji. Kwamba licha ya vilabu vya soka kukodi viwanja lakini mapato madogo ni chanzo cha hali mbaya ya viwanja hivyo. Ikumbukwe mwaka 2013 jumla ya viwanja 7 vilifungiwa kutokana na sababu zinazofanana na sasa.
Hatua ya kwanza ya kuchukua kwa wamiliki wa viwanja hivyo ni kuendesha kwa ubia na wawekezaji wengine ambao watakubali kuvitengeneza. Au wamiliki wa viwanja kuamua kuachana navyo hivyo kuviuza kwa wamiliki wapya ambao watakuwa na uwezo wa kuvikarabati na kuvifanya kuwa vya kisasa.
Njia nyingine ni kwa Halmashauri za Wilaya na Manispaa kukabidhiwa viwanja hivyo kama mnunuzi atakayemiliki kuendesha shughuli ambazo zitakuwa chanzo cha mapato ya ndani ya maeneo husika. Kwamba serikali inaweza kuchukua kwa maana ya kununua viwnaja hivyo kutoka Chama cha Mapinduzi na kuvimiliki. Inawezekana sina uthibitisho kisayansi lakini kwa maoni yangu viwanja hivi vinatakiwa kuuzwa kwa wamiliki wengine ama Chama cha Mapinduzi kiongeze uwekezaji kwa kuhakikisha vinakuwa na ubora.
ADHABU YA WAKAGUZI NI IPI?
Kabla ya Ligi kuanza Kamati ya Leseni ya Bodi ya Ligi Kuu inakagua viwanja vyote vinavyopaswa kutumika msimu mzima na kuidhinisha vile ambavyo vinakidhi matakwa ya kikanuni. Mathalani suala la vyumba vya kubadilisha nguo au maeneo ya kukaa wachezaji ni mambo ya msingi ambayo Kamati inatakiwa kuyazingatia. Ni kwanini wanaidhinisha viwanja ambavyo havina sifa? Je, nini adhabu ya wajumbe wa Kamati ya Leseni katika hali hii? Kama hatutachukua kwa pande zote, tatizo la ubovu wa viwanja litaendelea kututafuna.