Na Israel Saria
HIVI karibuni Chama cha soka nchini Kenya (FKF) kilikubali klabu yake ya Gor Mahia kucheza mechi za mashindano ya CAF katika viwanja vya Tanzania. Uamuzi wa kuhamisha mechi za Gor Mahia kwenda nyumbani Tanzania umetokana na hali mbaya ya viwanja vya Kenya. Shirikisho la Soka Afrika (CAF) liliwaambia FKF kuwa viwanja vingi vya Kenya havijakidhi vigezo vya kuruhusu kutumika kwenye mashindano ya CAF ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho. Uamuzi huo umekuja wakati Kenya ni miongoni mwa nchi zilizoomba kuandaa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Maombi ya Kenya yanashirikiana na nchi mbili za Uganda na Tanzania, ambapo kwa pamoja zimeomba kuandaa AFCON ya mwaka 2027. Wakati Kenya ikiambiwa viwanja vyake havina vigezo, hali ya Uganda nayo haikuwa nzuri kwani ililazimika kucheza baadhi ya mechi za nyumbani katika viwanja vya ugenini. Kwa mfano mchezo wa kuwania kufuzu AFCON 2023 dhidi ya Tanzania ulilazimika kufanyika nchini Misri.
Vilevile timu ya Taifa ya wanawake ya Uganda ililazimika kutumia uwanja mmoja huko nchini Rwanda ili kucheza na wageni wao timu ya Taifa ya wanawake ya Rwanda. Ukitazama nchi zote tatu zilikuwa zinasifika kwa viwanja vizuri. Mfano Tanzania inaweza kutegemea viwanja sita vya kuandaa mashindano hayo, Uwanja wa Benjamin Mkapa (Dar es salaam), Uwanja wa Uhuru(Dar es salaam), Uwanja wa Azam Complex(Dar es salaam), uwanja wa Sheikh Amri Abeid (Arusha), Uwanja wa CCM Kirumba (Mwanza) na uwanja wa Amaan (Zanzibar). Kati ya viwanja hivi, ni Sheikh Amri Abeid pekee ambao unaweza kuhitaji ukarabati mkubwa ili kukidhi vigezo vya CAF. Ni suala la serikali na wamiliki wa CCM kutoa kipaumbele kwa jiji la Kimataifa kama Arusha kuwa makazi ya michezo pia.
Majirani zetu Kenya walisifika kwa viwanja vizuri kama Nyayo na Moi Kasarani. Viwanja hivi vilikuwa vinajaza maelfu ya mashabiki na walikuwa na kila sababu ya kujivunia uzuri wa viwanja vyao. Hata hivyo hali ya mambo ya uwanja wa Nyayo na Moi Kasarani ni mbaya hadi CAF kufika mahali kutangaza havifai kuwa mwenyeji wa mashindano yao. Nchini Uganda uwanja wa Nakivubo ulikuwa umebeba sifa nyingi zamani. Lakini Uganda ya sasa inakabiliwa na tatizo la viwanja ndiyo sababu hata CAF imesema hawana sifa ya kutumia katika mashindano yao. Ni kweli kwamba kulikuwa na ukarabati katika uwanja wao mkuu na tegemeo wa Taifa, lakini bado kuna hali ya uchache wa viwanja katika nchi hiyo.
SABABU NI NINI?
Hivi viwanja wanaharibu kutoka na mikutano ya siasa, gwaride,kuegesha magari na kuvifanya kama vile kumbi za mikutano. Viwanja vinapotumika kwenye matukio mengine ya sherehe vinasababisha kuharibu, na hakuna teknolojia ya kuthibiti uchakavu wa viwanja kama unaotayarishwa kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu. Kwamba uongozi wa Real Madrid imepanga kutumia uwanja wao kama chanzo cha mapato kwa kukaribisha sherehe na matukio mengine kufanyika uwanjani hapo, lakini wanaanda mbinu ya kuzuia kuharibika eneo la kuchezea.
Nhcini Tanzania uwanja wa Benjamin Mkapa umesababisha matatizo kadhaa ikiwemo viongozi wake kuondolewa kwenye nafasi zao kwa kile kile kilichoitwa ubovu. Uwanja huo ulikuwa unategemea jenereta moja kwa kipindi kirefu hali ambayo umeme ulikuwa uanzimika mara kwa mara. Pia uwanja huo ulianza kuchakataa katika eneo la kuchezea kiasi kwamba CAF walieleza huenda ukakosa vigezo vya kutumika katika mashindano yao. Hii ina maana matumizi makubwa ya viwanja hivi hayawekewi bejati ya kukarabati. Bajeti ya kukarabati viwanja hivi hazitumiki ipasavyo vinginevyo visingeharaibika. Mfano uwanja wa Benjamin Mkapa una unalipwa kila mechi kama sehemu ya kuupa thamani na malipo ya matunzo.
NINI KINAWEZA KUFANYIKA?
Hatua ya kwanza ni kupunguza matukio ya kisiasa, mikutano, kugeuza kuwa maegesho na mambo yote yanayosababisha viwanja kuharibika. Vile kutumia bajeti yake ipasavyo ikiwemo kukarabati vyoo ambavyo vingi vinakuwa vichafu, kukarabati kumbi za mikutano na majukwaa ya viwanja.
Ili kupata nafasi ya kuwa mwenyeji wa AFCON lazima uwe na viwanja vyenye uhakika. Viwanja ambavyo unavitunza vizuri. Viwanja ambavyo vina hali zote za usalama kuanzia eneo la kuhezea, vyoo, kumbi na maizngira bora ya ulinzi. Tatizo sisi waswahili kutunza kitu na kukiendeleza tuna changamoto kubwa, hilo ni miongoni mwa sababu itakayopeperusha ndoto za Kenya, Tanzania na Uganda kuandaa michuano ya AFCON. Nchi ambazo zina utulivu mkubwa kuliko Angola iliyowahi kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe pamoja na uasi hadi mwaka 2010 ikaandaa AFCON mwaka huo, lakini Afrika mashiriki inashindwa kwa sababu ndogo tu; kutunza viwanja vyake vya soka.