UKUBALI au ukatae kiwango cha Ligi Kuu Tanzania imepanda na kwa mujibu wa wataalamu wa soka ambao wamekuwa wakitoa takwimu za Ligi wameita kuwa ni namba nne kwa Afrika. Kati ya vita ambayo waendeshaji, wadhamini, wachezaji na makocha pamoja na wadau wanapaswa kuielewa ni hii ya kiuchumi. TANZANIASPORTS inachambua kwa kina juu ya vita vya kiuchumi vinavyoinyemelea Ligi Kuu Tanzania kutoka kwa ligi shindani na matajiri wenye pesa kutoka nje. Makala haya yanafichua namna vita vya kiuchumi vinavyoweza kuathiri Ligi yetu pia.
KAULI YA RAIS TFF
Kuelekea mwishoni mwa mwaka 2024, Rais wa shirikisho la soka nchini, TFF, Wallace Karia alitoa kauli nyeti na yenye kuwakumbusha wamiliki wa vilabu, wadhamini na wadau kuwa suala la vita vya kiuchumi kwa timu zetu na ligi yetu ni muhimu na linapaswa kuimarishwa. Wallace Karia alikaririwa akisema, “Naomba pia klabu ziimarishe vitengo vya fedha sitaki kuona soka letu likiingia dosari kwa utakatishaji fedha. Nimekuwa nikihudhuria mikutano mbalimbali ya CAF na FIFA na kuna baadhi ya viongozi wenzangu wa Mataifa mengine hawahudhurii mikutano hiyo ukiuliza kwanini unaambiwa ameshikiliwa na Polisi kuhusu matumizi mabaya au kupokea fedha bila ya taarifa sahihi za fedha hizo. Na inaonekana watu wengi wanaingia kwenye soka ili kuficha shughuli zao, ingawaje sisi hatupo huko mara kadhaa serikali imekuwa ikifanya ukaguzi na kutukuta wasafi lakini ili tuwe salama zaidi lazima vitengo vya fedha viimarishwe kinachoingia na kutoka kionekane,”
Kwa kuzingatia muktadha huo, Karia alikuwa anasisitiza suala la fedha chafu kwenye mchezo wa soka. Lakini vile hoja hiyo inakwenda kwenye vilabu vyetu katika vita ya kiuchumi. Kwa mfano Rais Karia anaposema “vitengo vya fedha viimarishwe” maana yake pia klabu zinatakiwa kuondokana na hali mbaya ya kifedha ambayo inachangia timu kufanya vibaya. Ni kwamba kila klabu inatakiwa kubuni mikakati na mbinu za kupata fedha zaidi ili kuimarisha vikosi na Ligi yetu. Kimsingi suala la fedha kwa klabu limekuwa mfupa mgumu bila kujali hoja ya utakatishaji. Baadhi ya klabu zinakabiliwa na uwezo mdogo wa kulipa fedha za mishahara, uendeshaji wa timu, na shughuli nyinginezo. Ama baadhi zimekuwa zikilipa fedha ndogo hali ambayo inasababisha wachezaji kuvunja mikataba ama kucheza muda mfupi na kuondoka baada ya kubaini matatizo ya kifedha. Matatizo ya kifedha kwa klabu yamekuwa jambo linaloumiza vichwa mashirikisho mengi ya soka Afrika. Changamoto hii ndiyo sababu naungana na Rais Karia ni muhimu kuimarisha vitengo hivi ili viweze kuendana na ubora wa Ligi kwa kuhakikisha vinakuwa na vyanzo halali vya mapato ambayo yanaipa thamani timu katika Ligi.
KUCHUKULIWA KWA SEAD RAMOVIC
Yanga walimchukua Sead Ramovic kutoka klabu ya TX Galaxy ya Afrika kusini, lakini ameishia kutumikia klabu hiyo kwa muda wa siku 82 tu. Kocha huyo aliitumikia Yanga katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa na baadhi ya mechi za Ligi Kuu Tanzania. Hata hivyo akiwa katika kibarua hicho alipokea ofa nono kutoka kwa klabu ya Belouzdad ya Algeria ambao waliweka mezani kwake kiasi cha Dola 40,000 kama mshahara wake wa mwezi. Katika mazingira hayo Sead Ramovic hakuwa na namna nyingine zaidi ya kuomba kuondoka katika klabu ya Yanga ambayo ilikuwa inamlipa kiasi cha Dola 15,000 kwa mwezi. Kama mfanyakazi yeyote yule asingeliacha ofa hiyo. Katika mazingira haya, unaona dhahiri hii ni vita ya kiuchumi ambayo inaanza kupamba moto dhidi ya Ligi Kuu Tanzania. Kwamba ina makocha ambao wanaweza kupewa fursa na ofa nono katika klabu za ligi ya Juu ya Tanzania. Aidha, tunarudi palepale kuwa vitengo vya fedha vikiimarishwa maana yake mapato ya klabu yakua na malipo yake kwa wachezaji, makocha na wataalamu wengine yakuwa juu zaidi. Na kwahiyo ofa kutoka kwa timu za zilizopo kwenye Ligi kubwa zaidi ya Tanzania hazitaweza kuwababaisha.
OFA YA FADLU DAVIS
Simba hawawezi kusema hawajui kilichotokea, lakini katika hali halisi kocha wao Fadlu Davids anawindwa na miamba ya soka kutoka nchini Morocco. Klabu ya FAR Rabat ni timu ambayo inataka saini ya Fadlu Davids ingawaje ofa yao haijawekwa wazi na vyanzo vyangu vya taarifa. Hata hivyo kocha wa Simba amebainisha wazi kuwa hana mpango wa kuondoka Simba kwani ana mkataba na malengo ya kukamilisha aliyokubaliana na uongozi wake. inaelezwa pia viongozi wa Simba wamekataa ofa nyingine ya usajili ya Kibu Dennis kwa sababu ambazo zipo wazi, kwamba wapo kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho hivyo si busara kumruhusu staa wao kuondoka klabuni hapo. Hii ni dhahiri kuwa timu kubwa zimeona utaalamu uliopo kwenye Ligi Kuu Tanzania unapawa kunyakuliwa na kupelekwa kwao kwa nguvu ya fedha., ni nguvu za kiuchumi ndizo zinazowahamisha wachezaji na makocha kutoka Ligi moja kwenda nyingine. Vita hii ni yetu sote, tupambane.
NGUVU YA FEDHA
Kimsingi timu nyingi kutoka nchi za Kiarabu zimeongeza nguvu ya kuitupia jicho Ligi Kuu Tanzania. Mathalani usajili wa mshambuliaji Suleiman Mwalimu ‘Gomez’ kwenda klabu ya Waydad inayofundishwa na aliyekuwa kocha wa Mamelodi Sundowns, Rhulani Mokwema, unaonesha namna vilabu hivyo vinavyojizatiti kwa kuweka fedha mezani. Kimsingi hii ni vita ambayo inapaswa kutumika kama nyenzo ya kuimarisha nguvu ya soka la Tanzania badala ya kuidhoofisha. Klabu zinatakiwa kujiandaa kuuza wachezaji wao pale wanapohitajika nje endapo wameridhishwa na dau au hawana cha kupoteza zaidi ya kutumia malipo ya fedha hizo kuimarisha timu. Vita vya kiuchumi binakuja kuleta neema na balaa kwa Ligi Kuu. Neema inayokuja ni klabu kupata malipo mazuri wanayokubaliana na kupata wawakilishi wazuri wa Ligi Kuu ambao watatumika kama nyenzo ya kutafutwa wachezaji wengine zaidi. Wamiliki wa klabu kubwa wanaelewa silaha pekee waliyonayo ni fedha kwahiyo watafanya kila wawezalo kuhakikisha wananunua kila mchezaji mahiri au kocha mwenye viwango ili akatoe ujuzi kwao. Ni vita vya kiuchumi, klabu zijiimarishe kupitia vitengo vyao vya fedha na kukuza mapato ya klabu kutoka vyanzo mbalimbali,