Menu
in , , , ,

Ubora wa kipa Ali Salim uko eneo gani?

Tanzania Sports

MASHABIKI wa soka wameshuhudia nchi yao ikizalisha makipa mahiri sana na waliopata kutamba Ligi Kuu Tanzania. Wapo makipa wageni waliokuja kucheza Ligi Kuu Tanzania wakaonesha uwezo wao na wengine wakaachwa. Tanzania imepata kuwa na makipa wakali kama Mambosasa, Mohammed Mwameja, Rifat Said, Juma Kaseja, Shabani Dihile,Aishi Manula, na wengineo. Mjadala mkubwa umekuwa ukitawala miongoni mwa mashabiki na vyombo vya habari kuhusiana na nafasi ya golikipa wa Taifa Stars na klabu ya Simba, Ali Salim.

Je ana uwezo wa kutumia miguu yake kwa ufasaha?

Nafasi ya golikipa imebadilika kwa kiasi kikubwa. Makocha wa sasa wamekuwa na mfumo ambao unawalazimisha makipa kuwa ndiyo mabeki wa kwanza wa kati. Katika mfumo wa mabeki watatu, golikipa anategemewa kusogea mbele kutoka eneo lake hadi yadi 38 pale timu inaandaa mpango wa mashambulizi. Golikipa mwenye uwezo wa kutumia miguu huwa anatakiwa kushiriki kucheza eneo la nyuma ya namba tano ili kutengeneza ‘V’ inayounda shambulizi.

Kwa kawaida shambulizi hilo linakuwa kwa muundo wa namba nne kucheza kuelekea kushoto, na namba tano kucheza kulekea kulia, kisha namba sita anashuka eneo ambalo linamkutanisha na golikipa. Kwa maana kipa anatakiwa kuwa zaidi ya kukaa golini awe na uwezo wa kucheza kwa kutumia miguu yake. kwahiyo makipa wa sasa hawategemewi kupangua mashuti pekee wakiwa langoni bali kushiriki mchezo wenyewe kwa muda wote wa dakika 90.

Ali Salim si golikipa mwenye uwezo wa kutumia miguu yake kwa ufasaha. Uwezo wake wa kukokota mpira si mkubwa na kama jambo ambalo makocha wanatakiwa kufanya kazi ni eneo hili na anaweza kuiga mengi kutoka kwa Mousaa Camara anayetamba langoni katika klabu ya Simba au Aishi Manula. Ali Salim sio kipa wa kwanza kufundishwa matumizi sahihi ya miguu, tumewahi kuona hata Ulaya, golikipa wa Real Madrid, Thibous Courtois alikuwa na uwezo mdogo sana wa kucheza kwa miguu yake. Makocha wa Real Madrid ndiyo waliombadilisha kipa huyu ambaye sasa anaweza kukukota mpira na kutoa pasi vizuri katika ‘build up’.

Kama tukilingtanisha makipa watatu Ali Salim, Metacha Mnata na Abudtwalib Msheri, utaona Ali Salim na Msheri wanayo nafuu fulani kuliko Metacha. Inafahamika Metacha Mnata sio mahiri katika matumizi ya miguu yake hivyo naye anaachwa na soko la kisasa. Msheri ni kwa sababu hapati mechi nyingi za kumwimarisha lakini si kipa wa kubezwa.

Je uwezo wa kufanya uamuzi langoni unaridhisha?

Ali Salim anakabiliwa na changamoto ya kufanya uamuzi kwenye michezo mbalimbli anayopangwa iwe katika lango la Simba au Taifa Stars. Uwezo wake wa kufanya maamuzi umekuwa hafifu ndio chanzo kutokua kwa kiwango chake sasa. Ni kipa ambaye anatakiwa kulelewa na kutunzwa ili aweze kufika kwenye hali ya kuwa na uwezo mkubwa. Kwa mfano, yapo matukio kadhaa ameonesha anao uwezo wa kudhibiti michomo ya timu pinzani na hili alilifanya zaidi chini ya kocha Robertinho kabla hajatimuliwa.

Tangu wakati ule Ali Salim hakuwa mchezaji mwenye kiwango kikubwa na umahiri bali matukio pekee ambayo ni kupangua penalti na michomo ya mbali ndiyo yamekuwa gumzo kuliko uwezo wa jumla wa kufanya maamuzi. Lazima kuangalia utimamu wake katika kufanya maamuzi kila anapopangwa langoni ili kukua.

Je anao uwezo wa kucheza krosi?

Eneo hilo lina matatizo mengi. Ali Salim katika video kadhaa za michezo amekuwa na tatizo ya kucheza krosi na kufanya mahesabu mazuri (timing) ya eneo hatari ambalo linafikiwa na washambuliaji wa timu pinzani. Ali Salim si golikipa mzuri katika kupangua krosi iwe kutoka upande wa kulia au kushoto. Maeneo yote hayo yanatokana na ile hali ambayo wataalamu wa elimu wanasema wapo watu wanaojifunza jambo kwa njia ngumu (sio waelewa wa haraka) na wapo wale wepesi ambao wanaelewa haraka. Ali Salim sio mjuvi kugundua madhara ya krosi zinazoelekezwa langoni mwake na hili linamnyima nafasi ya kuwa mahiri kama walivyo wengine. Kutokana na hilo amekuwa akishindwa kurukia krosi na mara nyingi hutazama kwa macho.

Je anaweza kunusa hatari langoni?

Mathalani katika kikosi cha Simba kwa sasa labda Moussa Camara aumie au kocha aamue kumpimzisha kisha ampange Ali Salim, lakini ukweli ni kwamba anazidiwa kwa mbali sana na golikipa huyo mgeni. Tazama namna Moussa Camara alivyonusa hatari za Ahli Tripoli na alilazimika kujitosa katikati ya msitu wa Waarabu hao na kuokoa au kunyakua mipira aliohisia ni hatari. Moussa ameonesha mara kadhaa kwanini Simba wameweka pesa kwake, ananusa hatari na kuifanya kazi, kitu ambacho kwa Ali Salim hakipo. Hakuna matukio ambayo amejitokeza na kuruka katikati ya msitu wa washambuliaji wa timu pinzani, badala yake amesubiri matukio (moments) pekee ambazo zimeigharimu timu yake. Ni sababu hii hata Aishi Manula anamwacha mbali sana kiuwezo.

Je kasi yake ikoje?

Wapo makipa wenye kasi, mfano Aishi Manula. Kipa huyu anapokimbilia mpira katika eneo analopunguza hatari anayo kasi. Moussa Camara,Djiqui Diara, au Mohammed Mustafa wa Azam wamekuwa na kasi katika kukimbilia mipira au kupokea basi kutoka kwa mabeki wao. Ama pale timu inapoanzisha mpira kuanzia nyuma wanao uwezo wa kujiweka sawa kiufundi kucheza kitimu kwa miguu yao ili kutengeneza mashambulizi kuelekea lango la adui. Ali Salim hana kasi hiyo na si kipa wa kujipanga kifundi kuweza kucheza kitimu. Yeye ni aina ya makipa wa kizamani wanaokuwa langoni kusubiri kuokoa michomo na hatari kadhaa. Nje hapo hana kasi,

Je ni lazima kipa wa Yanga,Simba apangwe Taifa Stars?

Taifa Stars imetoka kubugizwa mabao mawili ya jioni na Jmahuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ukiangalia mchezo wenyewe, uamuzi wa benchi la ufundi na mpango wao wa kupambana na DRC unaona dhahiri makosa madogo madogo yameigharimu timu yetu. Miongoni mwa hilo ni kuamini kipa anayekalia benchi Simba au Yanga ndiye mahiri zaidi huku ikiwaona wengine ni nyongeza tu.

Kwa mfano tumeshuhudia kipa chaguo la tatu au la pili la Simba na Yanga anapewa jukumu la kusimama langoni mwa Taif Stars bila kuzingatia uwezo. Timu za Ligi Kuu zinao makipa wazawa wengine wenye uwezo kumzidi Ali Salim na imemwahi kutokea kuwa golikipa namba moja wa Taifa Stars ambaye hakuwa akicheza Simba wala Yanga.

Shaban Dihile alikuwa kipa wa JKT Ruvu akawa chaguo namba moja la kocha Marcio Maximo. Maximo hakuingia kwenye mtego wa kuchukua kipa namba tatu au mbili wa Simba au Yanga. Pia hakuangalia kucheza kwake Simba au Yanga pekee bali vigezo vya uwezo wa kipa wa kucheza Taifa Stars. Labda faida aliyonayo Ali Salim ni kufundishwa na makocha wa viwango vya juu na kumpa fursa ya kukaa lango la Taifa Stars. Kinyume cha hapo sio kipa wa kumtishwa kazi ambayo hawezi kuimudu na uwezo wake pamoja na kipaji ni vidogo.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version