Hali si shwari Manchester City na itakuwa ngumu kutetea ubingwa wao.
City wamepoteza mechi muhimu, tena dhidi ya mahasimu wao wa Jiji la Manchester, nao ni Manchester United baada ya kukubali kufungwa 4-2 Jumapili hii.
Kocha wa City, Manuel Pellegrini amesema kwamba anabeba lawama kwa hali yote ya kushuka kiwango kwa timu yake na kupoteza mechi kadhaa msimu huu.
Kwa kupoteza mechi hiyo huku vinara Chelsea wakishinda 1-0 dhidi ya QPR wameacha pengo la pointi 13 baina yao na vinara wa Stamford Bridge, huku wakishika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.
City sasa wamebakiwa na pointi zao 61, Man United wakiwa na 65, Arsenal 66 na Chelsea 73. Pamoja na kupata ushindi mwembamba dhidi ya QPR wanaoelekea kushuka daraja, bado Chelsea wapo pazuri katika kutwaa ubingwa kutokana na kazi kubwa waliyofanya mwanzoni mwa msimu.
Bao la Chelsea lilifungwa na Cesc Fabregas. Beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic alipigwa na kitu kutoka kwa washabiki,
Mabao ya United yalifungwa na Ashley Young, Marouane Fellaini, Juan Mata na Chris Smalling wakati ya City yalitiwa kimiani na Sergio Aguero.
Ukabaji wa City ulionekana kuwa dhaifu na kwa mara nyingine nahodha Vincent Kompany hakuwa na kiwango kinachotakiwa na alitolewa baada ya nusu ya kwanza, nafasi yake ikachukuliwa na Eliaquim Mangala.