Ni Barcelona
*RUFAA YA CHELSEA YAKWAMA*
Mabingwa wa Hispania na Ulaya, Barcelona wameanza vyema msimu kwa kutwaa taji la Uefa Super Cup, linaloandaliwa na Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) kwa kukutanisha mabingwa wa Ulaya na wale wa Ligi ya Europa.
Ilikuwa mechi kali, yenye mvuto na wingi wa mabao, ikijumuisha timu kutoka nchi moja, huku mechi yenyewe ikipigwa Tbilisi, Georgia.
Lilikuwa bao la Pedro, mshambuliaji wa Barca anayewania kuhamia Manchester United kabla ya dirisha la usajili kufungwa, lililowazamisha Sevilla, ushindi wa Barca ukiwa ni 5-4 na ulipatikana katika muda wa ziada, baada ya kutoshana nguvu katika dakika 90 za kawaida.
Pedro aliingia katika dakika ya 93 na kuionesha dunia umuhimu wake. Sevilla waliwahangaisha Barcelona katika muda wote wa mchezo, tofauti na ilivyotarajiwa na wengi kwamba wangepata ushindi wa mteremko.
Barcelona walishangilia kwa nguvu ushindi huo, ambapo yawezekana hii ikawa mechi ya mwisho kwa Pedro kuwa nao.
Hata hivyo, beki wa kulia wa Barca, Dani Alves aliyetaka kuhama kisha akabadili mawazo, amemsihi Pedro abaki naye Camp Nou, akimwambia kuna uwezekano akaenda kuharibu soka yake Man United.
RUFAA YA CHELSEA YAKWAMA
Katika hatua nyingine, Chama cha Soka (FA) cha England kimetupilia mbali rufaa ya kipa wa Chelsea, Thibaut Courtois, iliyokuwa ikipinga kadi nyekundu ya moja kwa moja aliyopewa wakati wa mechi dhidi ya Swansea.
Chelsea walijaribu kukata rufaa ili mchezaji huyo apate nafasi wikiendi hii kwenye mechi ngumu ya Ligi Kuu dhidi ya Manchester City.
Courtois alipewa kadi hiyo baada ya kumwangusha Bafetimbi Gomis. Walikwenda sare ya 2-2. Itabidi kipa namba mbili, Asmir Begovic akae golini, akiwa amesajiliwa kiangazi hiki kutoka Stoke.