Menu
in , , ,

UARGENTINA NI TATIZO KWA MESSI

“Messi si ahame nchi tu”.

Mchambuzi mmoja mashuhuri wa michezo wa hapa nyumbani aliandika maneno hayo kwenye ukurasa wake wa Facebook baada ya Argentina kupoteza mchezo wa fainali dhidi ya Chile kwenye michuano ya Copa America mapema mwezi huu kwa mikwaju ya penalti. Messi ahame Nchi.

Ripoti za hivi karibuni zinaonyesha mshahara wa Messi na malipo yake mengine kutokana na mikataba yake binafsi humuingizia takriban paundi milioni 1 kwa wiki. Hizo ni zaidi ya shilingi bilioni 3 za kitanzania. Pesa zote hizo anazotia mfukoni kila Jumamosi hazijatosha kumnunulia Messi furaha.

Ameshinda makombe matatu (treble) akiwa na klabu yake ya Barcelona msimu uliomalizika. Makombe ambayo pia hayajafanikiwa kumpa Messi furaha anayostahili. Shida yake ni moja. Ni uargentina.

Uargentina wake unamzuia Messi asiwe na furaha inayotegemewa kwa nafasi aliyo nayo kwenye ulimwengu wa soka. Hapati heshima anayostahili Argentina kwa sababu eti Argentina imeshindwa kutwaa mataji makubwa ya Kombe la Dunia na Copa America.

Hivi Messi anacheza peke yake?! Kwenye michuano ya Copa America iliyomalizika hivi punde Messi alishinda tuzo ya ‘Man of the match’ kwenye michezo minne kati ya sita aliyocheza. Namna alivyozihadaa ngome za wapinzani kwenye michezo yote ndio ilikuwa sababu ya ushindi wa Argentina mbaka kufanikiwa kutinga fainali.

Hakuonyesha ubinafsi akajaribu kuwatengenezea wenzie nafasi za kufunga jambo ambalo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Kiwango alichokionyesha kwenye michuano hiyo kilitosha kabisa kuipa Argentina ubingwa. Haikuwa bahati yake na Argentina wakapoteza mchezo wa fainali dhidi ya wenyeji Chile.

Akapewa tuzo ya mchezaji bora wa michuano na akaikataa.

Kilichofuata ni mashambulizi ya maneno dhidi ya Lionel Messi. Mchango wake ukaonekana si kitu eti kwa kuwa hawakushinda taji. Ni peke yake aliyebezwa na kutukanwa kati ya wachezaji wote wa Argentina.

Wakasahau ni yeye pekee kati ya wachezaji wa Argentina aliyefanikiwa kufunga kwenye mikwaju ya penalti kwenye mchezo wa fainali. Gonzalo Higuain na Ever Banega walikosa penalti. Awali Higuain alikosa pia bao la wazi.

Wachezaji wenzie walimuangusha Messi. Bado mashambulizi yalionekana kumstahili zaidi Messi pekee.

Waargentina wenyewe wakamshmbulia Messi eti kwa kushindwa kuliletea taifa Copa America. Mbaka watu mashuhuri anaowaheshimu kama Diego Mardaona wakamshambulia kwa maneno. Ni ukosefu wa heshima kwa Messi. Tatizo ni Uargentina.

Christiano Ronaldo hakuwahi pia kushinda kombe lolote na timu ya taifa ya Ureno. Hakuwahi hata kuifikisha Ureno fainali ya kombe la Dunia. Mbona anaheshimiwa na kutukuzwa na wareno? Jijini Madeira nchini Ureno alikozaliwa Ronaldo kumejengwa sanamu yake Disemba mwaka jana.

Sanamu hii inaheshimiwa kama ishara ya heshima ya wareno kwa Ronaldo. Zlatan Ibrahimovic pia ana heshima ya kutosha nchini kwake Sweden pamoja na kushindwa angalau kuipeleka Sweden kwenye fainali za kombe la dunia mwaka jana.

Hakupokea mashambulizi yoyote. Argentina imeshindwa kuonyesha heshima kwa Messi. Sanamu yake iliyojengwa pamoja na sanamu za Maradona na Batistusta hivi karibuni jijini Buenos Aires nchini Aregentina imekatwa vidole viwili na watu wasiojulikana. Heshima ya Messi ipo kwenye nchi nyingine zikiwemo Marekani na Uingereza.

Jijini New York kuna sanamu ya Messi inayopewa heshima kubwa na hakuna aliyeikata vidole. Hata London ipo sanamu ya Messi. Waingereza hawakuikata vidole.

Inaonyeha umarekani ama uingereza ungefaa kuwa utaifa wa Messi. Ila huu uargentina umekuwa chanzo cha kumkosesha furaha katika kipindi hiki. Nashindwa kufikiri namna ambavyo Messi angetukuzwa kama angekuwa muingereza. Uargentina ni tatizo kwa Messi.

cassimbendera@gmail.com

Written by Kassim

Exit mobile version