Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania ya umri chini ya miaka 20 inaanzia moja kwa moja raundi ya kwanza Kanda ya Afrika kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Canada.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana (Agosti 18 mwaka huu) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Tanzania imepangiwa kucheza na Msumbiji ambapo mechi ya kwanza itachezwa Dar es Salaam kati ya Oktoba 25, 26 au 27 mwaka huu.
Mechi ya marudiano itachezwa wiki mbili baadaye nchini Msumbiji. Mechi hiyo inatakiwa kuchezwa kati ya Novemba 8,9 au 10 mwaka huu. Iwapo itafanikiwa kuitoa Msumbiji itacheza raundi ya pili na mshindi wa mechi kati ya Botswana na Afrika Kusini.
Raundi ya Tatu ambayo ndiyo ya mwisho, mechi zake za kwanza zitachezwa kati ya Januari 10, 11 au 12 mwakani wakati zile za marudiano zitakuwa kati ya Januari 24,25 au 26 mwakani.
Sudan Kusini na Uganda ndizo timu pekee kwa Kanda ya Afrika zinazoanzia raundi ya mchujo ambapo katika mechi ya kwanza zitapambana kati ya Septemba 13,14 au 15 mwaka huu na kurudiana kati ya Septemba 27, 28 au 29 mwaka huu.
Nchi 17 za Afrika zimeingia kwenye michuano hiyo. Nchi hizo ni Afrika Kusini, Botswana, Burkina Faso, Equatorial Guinea, Ghana, Guinea Bissau, Ivory Coast, Misri, Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Sudan Kusini, Tanzania, Tunisia, Uganda na Zambia.