TIMU ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars Timu ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, inatarajia kucheza mechi ya kirafiki na wenzao wa Botswana kwa ajili ya kujiandaa na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake zitakazofanyika Afrika Kusini kuanzia Oktoba 31. Akizungumza jana, Kocha wa Twiga, Boniface Mkwasa, alisema kuwa Botswana ndio wamewaomba kucheza nao na kwamba hadi sasa, wanaendelea kukamilisha taratibu za kuhakikisha kuwa wanaitumia vyema fursa hiyo ya kujipima kabla ya kwenda kwenye michuano nchini Afrika Kusini. Mkwasa alisema kuwa mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Jumatatu (Oktoba 25) na kama hakutakuwa na mabadiliko, timu yao itaondoka nchini Jumapili ikiwa na wachezaji 20. Twiga wataanza michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya saba kwa kushuka dimbani Oktoba 31 na kucheza dhidi ya wenyeji ‘Banyana Banyana’. Timu nyingine katika kundi la Twiga ni Mali na Nigeria, ambao wana rekodi ya kutisha ya kutwaa ubingwa mara tano kati ya mara sita tangu kuanza kufanyika kwa michuano hiyo mwaka 1998. CHANZO: NIPASHE