Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage amesema kikosi chake kiko tayari kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Zambia itakayochezwa keshokutwa (Ijumaa) jijini Lusaka.
Akizungumza kwenye hafla ya kuiaga timu hiyo iliyofanyika leo (Februari 12 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF jijini Dar es Salaam, Kocha Kaijage amesema wachezaji wake wako vizuri, ingawa hakuwa tayari kutoa ahadi kuhusu matokeo.
“Vijana wako vizuri, lakini sitaki kutoa ahadi. Watanzania watuombee, watuunge mkono ili tuweze kufanya vizuri,” amesema Kocha Kaijage katika hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi.
Twiga Stars inaondoka na kikosi cha wachezaji 19 na benchi la ufundi lenye watu watano kwa ndege ya Fastjet kwa ajili ya mechi hiyo itakayooanza saa 9 kamili kwa saa za Zambia. Msafara wa timu hiyo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho chini ya nahodha Sophia Mwasikili ni Amina Ali, Anastazia Katunzi, Asha Rashid, Donisia Minja, Esther Chabruma, Etoe Mlenzi, Everine Sekikubo, Fatuma Issa, Fatuma Makusanya, Fatuma Mwisendi, Fatuma Omari, Happiness Mwaipata, Maimuna Mkane, Mwapewa Mtumwa, Sherida Boniface, Therese Yona, Vumilia Maarifa na Zena Said.
Wakati huo huo, timu ya Azam imeondoka leo alfajiri (Februari 12 mwaka huu) kwenda Beira, Msumbiji kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi Ferroviario da Beira itakayochezwa Jumamosi. Msafara wa timu hiyo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, James Mhagama.
Naye mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Nassib Ramadhan ataongoza msafara wa timu ya Yanga inayoondoka kesho mchana kwenda Comoro kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Komorozine itakayochezwa Jumamosi.
MECHI YA MBEYA CITY, MTIBWA YAINGIZA MIL 25
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Mbeya City na Mtibwa Sugar iliyochezwa Februari 9 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya imeingiza sh. 25,602,000.
Watazamaji 8,534 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyomalizika kwa wenyeji Mbeya City kuibuka na ushindi wa mabao 2-1. Kiingilio katika mechi hiyo kilikuwa sh. 3,000.
Mgawanyo wa mapato ulikuwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 3,905,389.83, gharama za kuchapa tiketi sh. 489,500 wakati kila klabu ilipata sh. 6,256,097.05.
Uwanja sh. 3,181,066.52, gharama za mechi sh. 1,908,639.91, Bodi ya Ligi sh. 1,908,639.91, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 954,319.96 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA) sh. 742,248.86.