Ronaldo, Salah na Modric
WAMEFIKA. Ndivyo unavyoweza kusema juu ya utafutwaji wa mchezaji bora wa Ulaya.
Kama ilivyotarajiwa, Cristiano Ronaldo ameingia kwenye orodha hiyo ya wachezaji watatu bora ambapo mmoja ataibuka kidedea.
Ikumbukwe kwamba Ronaldo aliwabeba sana Real Madrid hadi kutwaa ubingwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), akiwamaliza Liverpool ambao nyota wao pia, Mohamed Salah amechaguliwa.
Luka Modric wa Real Madrid anafunga orodha hii, na ni wazi kwamba mchango wake mkubwa na wa aina yake katika kuwabeba Croatia kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi hadi fainali walipopoteza kwa Ufaransa ni sehemu kubwa mno ya mafanikio yake.
Kimsingi wachezaji wote watatu walicheza fainali ya UCL jijini Kiev, Ukraine msimu uliopita, ambapo Modric na Ronaldo walimzidi nguvu Salah na wenzake wa Liverpool, lakini Salah akiumia na kuondoka mchezoni mapema.
Wote pia wamepeperusha bendera za nchi zao kwenye fainali za Urusi, lakini wakati Modric aking’aa, Salah na Misri yake walitoka mapema katika awamu ya kwanza walau Ronaldo akasogea sogea lakini hakuweza kufika fainali tofauti na ilivyokuwa kwenye Euro ya nchini Ufaransa ambapo walitwaa ubingwa.
Ronaldo sasa ameshaondoka Real, akifanya kazi na Bibi Kizee wa Torino wakati wawili waliobaki wapo katika klabu zile zile, na wamekuwa pia wakidhaniwa kwamba wanaweza kuchaguliwa katika kuwania uchezaji bora wa dunia.
Modric, mchezaji mahiri wa kiungo na washambuliaji wawili hao wanaojua fika kuzifumania nyavu, walichaguliwa na jopo la makocha 80 na wanahabari 55, ambapo mshindi atapatiwa tuzo hiyo wakati wa kupanga makundi kwa ajili ya UCL Agosti 30 huko Monaco, Ufaransa.
=-=