Menu
in , ,

TUWE MAKINI NA VIPIMO VYA NDIMI ZETU KWA SAMATTA

MS

Ulikuwa usiku wake mzuri kwake, usiku ambao ulikuja na vitu vingi
katika maisha yake. Vitu vingi viliambatana mara baada ya mechi ya
Gent na Genk.

Haikuwa vyombo vya habari vya Tanzania pekee vilivyopamba jina lake,
hata vyombo vya habari ambavyo awali tulizoea kuwasoma kina Messi,
Ronaldo, Sanchez na wachezaji wakubwa barani ulaya vilimwandika Mbwana
Ally Samatta.

Magoli yake mawili yaliyotosha kujenga ukubwa wa Mbwana Samatta wiki
hii, ukubwa ambao alikuwa akiuota awali alipokuwa anauota wakati yupo
mchangani, ukubwa ambao alikuwa akiutamani mpaka akapigana akafika
Simba akiamini kuwa ndipo daraja pekee atakalotumia kwenda kwenye
ukubwa anaouishi kila uchwao.

Kufika TP Mazembe hakukuwa mwisho wa safari yake, pesa za Katumbi
hazikumwaminisha au kumzubaisha kuwa alipo ndipo sehemu aliyokuwa
anaiota kila siku.

Hakuziangalia zile pesa kwa kuridhika, aliamini kuna sehemu sahihi
ambayo ni kubwa ambapo atapata pesa nyingi zaidi ya hizi za Katumbi.
Kila dakika alipigana kutafuta mafanikio yake makubwa akiamini
kutengeneza mafanikio makubwa ndani yake ndipo atakapokuwa
anatengeneza furaha yake.

Furaha yake aliijenga kwa kufunga, Kwanini asiwe mtu mwenye furaha
kuchaguliwa kwenye kikosi bora cha juma la Europa?

Maana kubwa ya vyote hivi ni kwamba kila kitu kinawezekana katika
maisha kama ukitia bidii kwenye jambo lolote unalolifanya, kuna funzo
kubwa sana kwa Samatta kuingia kwenye kikosi bora cha juma cha Europa.
Ni wakati sahihi wa yeye kuona wazi kuwa kila kitu ni hatua katika
maisha, haijalishi unapiga hatua kwa spidi gani lakini cha muhimu ni
hatua zako kuwa za uhakika.

Alianza kuwa kwenye kikosi bora cha Afrika, amefanikiwa kuingia kwenye
kikosi cha juma cha Europa michuano ambayo inawachezaji wazuri kama
Eden Dzeko na wengine wengi.

Kwanini yeye na sisi Watanzania tusijivunie kwa uhakika wa hatua hizi
za Samatta?. Lazima tujivunie, lazima tuandike kwenye magazeti,
mitandano ya kijamii, kuongea kwenye radio, na vituo vyetu vya runinga
huku tukimsifu na kujivunia shujaa wetu.

Ni bahati kumuona Samatta kwa sababu lazima utamsifia kwa wajukuu
zako, kwa hiyo ni lazima tukae kwenye mitandano ya kijamii tukimsifia.

Na tunaenda mbali zaidi mpaka kumjaza sehemu asiyo na haki ili awe na
haki. Hii yote ni kwa sababu ya furaha yetu kubwa juu ya mafanikio
yake.

Kwa wiki hii ni kawaida kukutana na Andiko linaloelezea ufalme wa
Samatta mbele ya Aguero, Rooney, Welbeck kwa sababu tu ya goli mbili
za juzi.

Ni jambo jema sana kumuombea Samatta afike katika daraja la hawa watu
tunaowataja kwa sababu tunapenda maendeleo ya Samatta yeye ndiye
kombe la dunia tulilonalo muda huu kwenye kabati yetu. Lakini umakini
unahitajika kila tunapoamua kuruhusu ndimi zetu tunapomsifia Mbwana
Samatta.

kikawaida sisi binadamu huwa tunasikia kitu kimoja tunapokuwa kuwa
tunaambiwa kwa pamoja. Utofauti wetu unakuja kwenye mapokeo ya vitu
tulivyovisikia. Mapokeo ndiyo hutupa matokeo tofauti kwa kila mtu, na
hii ni kutokana na kuwa hutulingani uwezo wetu wa kutafasiri jambo
tunalolipokea.

Tafasiri ya kitu huua au kujenga malengo ya mtu fulani. Kusema Samatta
kuwa ni zaidi ya Aguero ni kumfanya yeye ajione hapo alipo ndipo
alipofika, hatakiwi tena kupiga hatua ya kusogea zaidi kwa sababu yeye
ni zaidi ya Aguero. Tayari ameshawekwa daraja moja na kina Messi na
Ronaldo kwa sababu hawa ndiyo watu ambao wako juu ya Aguero.

Tunakosea sana kumuonesha Samatta kuwa tayari ameshafika, hii
tunamfanya ashibe kwa harufu ya chakula. Tunatakiwa tumtie njaa Mbwana
Samatta ili atafute chakula kwa hali, nguvu zake zote.

Tunatakiwa tumpongeze huku tukiwa tumekunja nyuso zetu. Hatakiwi kuona
meno yetu tukimchekea kipindi hiki. Makofi pekee yaliyoambatana na
sura zinazomwambia hapo ulipo hutakiwi kuwepo ndivyo vitu sahihi vya
kumsukuma Samatta.

Pamoja na ujinga wao binafsi wa baadhi ya wachezaji wetu wa Tanzania lakini
tumeua wengi sana kwa njia hii ya kuwaonesha hapo walipo wamefika.

Wakati yuko Simba tulimwambia yeye ni Messi, Singano akajiona amefika
muda huu hana uhakika wa namba Azam.

Kuna aina nyingi za kumuunga mkono Samatta, lakini aina hii tunayoenda
nayo tunatakiwa tuwe makini sana na vipimo vya ndimi zetu. Tusirefushe
sana ndimi zetu mpaka tukapata shida kuzirudisha ndani ya mdomo hapo
baadaye.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version