Ukiachana na mchezo wa mpira wa miguu ambao kwangu mimi naamini ndio unaoongoza kwa kufuatiliwa zaidi na kupendwa hapa Tanzania, naweza kusema pia masumbwi ni mchezo wa pili unaopendwa zaidi na umekuwa moja ya michezo inayokua kwa kasi Tanzania.
Masumbwi ni moja kati ya mchezo ambao pia umechangia si tu kuinua vipaji vya vijana bali pia kutoa fursa za ajira na kujenga maisha bora kwao jambo ambalo linafanya linafanya mchezo huu kuwa moja ya nyenzo muhimu za maendeleo ya vijana nchini.
Tanzania ina historia ya muda mrefu kwenye mchezo wa ngumi. Mwanzo wa mchezo huu nchini ulianza wakati wa ukoloni lakini ulipata umaarufu zaidi katika miaka ya 1960 baada ya uhuru. Ngumi zilipendwa na watu wengi na klabu za michezo za mtaani zikaanza kusimama, zikijikita katika kuibua vipaji vya vijana. Pamoja na changamoto zilizokuwepo wachezaji wa ngumi walizidi kuibuka na kuwakilisha nchi kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa kama Michezo ya Jumuiya ya Madola pamoja na Olimpiki.
Ukizungumzia mchezo huu wa ngumi kuna majina ambayo huwezi kuacha kuyataja kama Francis Cheka, Hassan Mwakinyo, Twaha Kiduku na Karim Mandonga majina ambayo yamekuwa yakivuma si tu ndani ya nchi bali hata nje ya mipaka ya Tanzania. Hawa wamefanikiwa kutokana na msaada wa klabu na makocha wa ndani ambao wanajitahidi kukuza vipaji vya ngumi.
Michezo kwa ujumla imekuwa nyenzo muhimu ya kutoa ajira kwa vijana na mchezo wa ngumi hauko nyuma katika hili. Kwa hali ya uchumi isiyokuwa thabiti kwa vijana wengi,mchezo wa ngumi umekua ukitoa fursa muhimu za kujiendeleza kimaisha kupitia mashindano mbalimbali ambayo yamekua yakiandaliwa na wadau wa ngumi, mikataba ya kibiashara na udhamini wa makampuni mbalimbali ambayo yamekua yakiendeleza chachu ya mafanikio ya mchezo huu.
Tumekua tukishuhudia wachezaji wa ngumi ambao wamekua wakishiriki mashindano ya ndani na nje ya nchi ambayo hutoa zawadi kubwa za pesa. Mashindano haya ni kama vile ngumi za ridhaa (amateur) na zile za kulipwa (professional). Kwa mfano, wachezaji kama Twaha Kiduku,Francis Cheka na Hassan Mwakinyo wamejipatia kipato kizuri kupitia mapambano ya kulipwa ndani na nje ya Tanzania.
Makampuni ya michezo, maduka ya vifaa vya michezo, na makampuni ya mawasiliano yamekuwa yakidhamini wachezaji wa ngumi kama njia ya kutangaza bidhaa zao. Kwa vijana, kupata udhamini huu kunawawezesha kujipatia kipato cha ziada. Udhamini huu unaweza kuwa wa kifedha au kuwapa vifaa vinavyosaidia mafunzo na mashindano.
Ingawa mchezo wa ngumi unatoa ajira kwa vijana lakini changamoto kadhaa zinakabili ukuaji wake. Changamoto hizi ni pamoja na ukosefu wa miundombinu bora, ukosefu wa vifaa vya kisasa vya mazoezi, na ukosefu wa udhamini wa kutosha kwa wachezaji wa ndani. Aidha, kukosekana kwa mfumo mzuri wa kuwaendeleza wachezaji wa ridhaa kuelekea kwenye ngumi za kulipwa kunarudisha nyuma jitihada za kuendeleza mchezo huu nchini.
Kama ilivyo katika mchezo wa mpira wa miguu basi na katika mchezo huu wa masumbwi hapa Tanzania kuwa na uwekezaji wa kutosha kwenye miundombinu ya michezo, elimu kwa makocha, na ushirikiano mzuri kati ya sekta binafsi na serikali, michezo ya ngumi inaweza kutoa ajira nyingi zaidi kwa vijana na hivyo kuboresha maisha yao.
Mchezo wa ngumi nchini Tanzania una nafasi kubwa ya kuleta maendeleo kwa vijana, si tu kupitia uboreshaji wa vipaji bali pia kutoa fursa za ajira. Ikiwa changamoto zinazokabili mchezo huu zitashughulikiwa ipasavyo, ngumi inaweza kuwa chanzo muhimu cha ajira na maendeleo kwa vijana wa Tanzania. Kukuza mchezo huu kunahitaji juhudi za pamoja kati ya serikali, sekta binafsi, na jamii kwa ujumla ili kufungua milango zaidi ya mafanikio kwa vijana nchini.
ReplyForward |