Menu
in , , ,

Tusipokuwa makini tutapoteza vipaji vyetu

Tanzania Sports

MALAIKA Mihambo ni mwanamichezo wa Ujerumani mwenye asili ya Zanzibar. Sababu za yeye kuwa raia wa Ujerumani sote tunaweza kukiri kuwa aina ya michezo anayoshiriki haina kipaumbele kikubwa kwenye nchi yetu ya Tanzania. Katika sekta ya michezo Tanzania, mchezo wa soka ni namba moja, kisha inafuatia mingine kama vile Masumbwi, kikapu, volleyball, mpiura wa pete na kadhalika. 

Malaika Mihambo ni miongoni mwa nyota ambao wamelikimbia Taifa hili sababu ya kukosekana maendeleo ya mchezo wa kuruka juu (high jump), kuruka chini (long jump) pamoja na riadha kwa ujumla wake. mafanikio machache yaliyopo kwenye michezo hiyo yanaweza kuwafanya watanzania wenye vipaji kuhamia nchi nyingine kubwa na zenye maendeleo zaidi kama ilivyokuwa kwa Ujerumani. 

Pengine hali hii imezikumba nchi nyingi za Afrika kwani wapo wana michezo wanaoabadili uraia sababu ya nchi wanazotoka kuwa na nafasi finyu za kushiriki au kuwaendeleza. Chukulia mashindano ya Olimpiki unakuta baadhi ya mataifa ya Afrika hayana hata washiriki wa mchezo wa kurusha mikuki, tufe na kadhalika. 

Katika mazingira hayo unaona bayana wachezaji wenye vipaji wanachukua mwelekeo wa kwenda nchi nyingine. Katika nchi za Afrika magharibi kumekuwa na mvutano mkali linapofika suala la vipaji vya soka kwani baadhi ya wachezaji wanachukuliwa na mataifa ya Ulaya, Asia, Amerika na wimbi hili huenda likaendelezwa sababu ahadi za fedha pamoja maendeleo binafsi ya wachezaji.

Mchezo wa soka upande wa wanawake unakua kwa kasi nchini Tanzania. Timu za  Ligi Kuu zinamiliki timu za wanawake ambao wametengenezewa ligi yao, Women Premier League. Katika ligi ya wanawake baadhi ya wachezaji wanatoka nje ya nchi katika ukanda wa Afrika mashariki ambao wamesajiliwa na kukuza ligi hiyo. 

Hata hivyo kwenye Ligi ya wanawake kuna wachezaji wamenunuliwa kwenda nchi za kigeni na hivyo kuwakilisha bendera ya Tanzania. Wapo wachezaji wa kulipwa wanawake wanaotoka Tanzania kama vile Julietha Singano anayekipiga huko Mexico kwenye klabu ya FC Juarez, Aisha Masaka anayekipiga katika klabu ya Brighton ya England kwa kuwataja wachache. Wachezaji hawa wanawake wamepata nafasi haraka kucheza soka la kulipwa huko Ulaya na amerika sababu ya uhaba wa vipaji vya wanawake kwenye mchezo huo. 

Nimekumbuka suala la wachezaji wanawake baada ya kuona kikosi cha timu ya Taifa ya England chini ya miaka 23. Kwenye kikosi chao kuna mchezaji mwenye asili ya Tanzania, anaitwa Malaika Meena. Mchezaji huyu amekuwa akizungumzwa kwa muda mrefu na mashabiki wa soka la wanawake. Wadau wa soka la wanawake wamekuwa wakifuatilia maendeleo ya wachezaji hao na kubaini kuwa Tanzania kuna vipaji vingi ambavyo vingeweza kutamba hapa Ulaya. Hata hivyo isivyo bahati Malaika Meena anakuwa mchezaji wa timu hiyo kwa sababu amezaliwa hapa England. 

Kama ilivyokuwa kwa wajina wake Malaika Mihambo, sasa Malaika Meena amejichaguliwa kuchezea nchi ya England katika umri mdogo tu wa miaka 23. Katika mazingira haya mdau wa maendeleo ya soka la nyumbani Tanzania lazima atajiuliza swali, imekuwa mamlaka zinazohusika hazikuona kipaji cha Malaika Meena? 

Ama ilikuwa hadi Malaika Meena ajipendekeze kwenye mamlaka za soka la wanawake Tanzania ndipo apewe kipaumbele? Je mamlaka za soka Tanzania hazikuweza kumfikia mchezjai huyo kumshawishi kuvaa jezi za timu ya Taifa ya wanawake ya Tanzania? 

Kwa mfano ukitembelea katika kurasa za mitandao ya kijamii ya shirikisho la soka Tanzania, TFF unakutana na sifa nyingi zimeelezwa kuhusu Malaika Meena. Lakini ghafla unapoona jina lake linawakilisha nchi ya England lazima ujiulize kimetokea kitu gani? Mamlaka zinazohusika, namaanisha TFF ni wakati sasa kukubali hakuna mchezaji atakayejieleta ikiwa wenyewe hatufanyi juhudi zozote kumfuatilia. 

Napenda kutoa rai kwa mamlaka zinazohusika kwamba kadiri tunavyoshindwa kuchukua hatua za kuwaweka sawa ama kuwaingiza kwenye mipango yetu kwa kuzungumza nao na kukubaliana ndivyo tunavyoporwa wachezaji wenye vipaji na Mataifa makubwa. Malaika Meena hakuwa mchezaji wa kuikacha Tanzania. Kwenye kikosi cha Twiga Stars tungeweza kumtumia vyema kama nyenzo ya kuangaza vipaji vilivyopo nchini. Hata hivyo kwa sababu ambazo hadi sasa hazieleweki mchezaji huyo ametuacha. Mamlaka zinazohusika zinatakiwa kuangalia kwa makini suala hili kwa makini sana.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version