Menu
in , ,

TUNATEMBEA KWENYE GIZA AMBALO FEISAL “FEI” MTOTO LIMEMTIA UPOFU

Tanzania Sports

Hii ndiyo dunia ambayo tumeamua kuishi na kuamini ni dunia sahihi ambayo inaweza kutufikisha sehemu ambayo ni kubwa.

Dunia yenye giza kubwa, giza ambalo limetutia upofu, upofu ambao unatufanya tufanye vitu visivyokuwa na manufaa kwetu sisi.

Ndiyo maana tulimchagua Clement Sanga kama mwenyekiti wa bodi ya ligi wakati tunajua ni makamu mwenyekiti wa Yanga. Hatukuliona hili mwanzoni tumekuja kuliona wakati ambao tayari yupo kwenye majukumu yake.

Hii ni kwa sababu tulifanya uchaguzi wa viongozi wetu tukiwa gizani, hatukupata nafasi ya kujua ni yupi sahihi na yupi siyo sahihi katika maendeleo yetu ya mpira.

Maamuzi yetu mabovu yanatokana na giza zito lililopo mbele ya macho yetu, ndiyo maana tuliamua kulikataa kombe la Kagame Cup na kuamua kucheza mechi zenye hadhi ya Ndondo Cup.

Hatukuona umuhimu wa kuipa timu mechi za ushindani kwa ajili ya mechi za mashindano ya CAF.

Kwetu sisi tuliona ni sawa kwa sababu wakati tunaamua hakukuwepo taa la kuondoa giza kwenye akili zetu.

Akili ambazo hazifikirii maendeleo katika mpira wetu ila zinafikiria maendeleo katika matumbo yetu.

Ndiyo maana macho, masikio na akili zetu huwa zinasimama ipasavyo kipindi cha usajili kwa sababu wengi wanajua kuwa ndiyo wakati wa matumbo yao kunufaika na siyo timu kunufaika.

Ndicho kipindi ambacho utaona ujinga ambao hugeuka maajabu makubwa ambayo ni kawaida tu kwetu sisi kwenye ardhi hii ya Nyerere kutokea.

Utashangaa kipi kuona mchezaji anasajiliwa na timu zaidi ya moja kwa wakati mmoja? Hakuna cha ajabu kwa sababu kila uchwao jambo hili hutokea.

Na kila likitokea hakuna anayeona aibu kuwa hili jambo halitakiwi kurudiwa tena na cha ajabu kipindi kingine cha usajili utasikia ajabu hili.

Tena wengi wao hufurahia jambo hili kwa sababu tumbo huwa limejaa pesa za ujanja janja.

Ujanja ambao unawapelekea mpaka wachezaji husika kutokuwa na wasimamizi au mawakala sahihi.

Kitu ambacho hupelekea wachezaji binafsi kusimamia usajili wao kama wao hadi mwisho wakisaidiwa na watu ambao wao giza ndiyo sehemu sahihi ya kuishi.

Hawataki mwanga na hawana shida kabisa ya mwanga wowote kwa sababu giza kwao ni barabara zuri la kutengeneza maendeleo ya tumbo lao na siyo maendeleo ya mpira wetu.

Ni kitu cha kawaida kwetu sisi kushusha thamani ya mwanga na kuamini kuwa giza tunalotumia litatuongoza mpaka sehemu kubwa ya maendeleo ya mpira wetu.

Bado tuna safari ndefu sana bro kwenye kila kitu ndiyo maana jana sikushangaa kuona 
Singida wamesaini mkataba wa moja kwa moja  mchezaji mwenye mkataba na timu nyingine (JKU) kabla ya kununua mkataba wake wa awali kutoka kwenye timu ambayo ilikuwa inammiliki awali.

Mchezaji akakubali kupiga picha za utambulisho akiwa na jezi za timu nyingne (Singida) wakati anajua mkataba wake na timu yake (JKU) bado haujanunuliwa/kuvunjwa.

Timu nyingine (Yanga) inaibuka na “kumaliza” taratibu za usajili  masaa machache baada ya picha za utambulisho za timu nyingne(singida) kusambazwa.

Yote haya yamefanyika siku moja tena na mchezaji mmoja, mchezaji ambaye hana wasimamizi wa kumfikisha mbali.

Wasimamizi wa kumuongoza kipi anapaswa kufanya sahihi katika maendeleo ya maisha yake na kipi ambacho hapaswi kufanya katika maendeleo ya maisha yake ya mpira.

Anatembea kwenye giza bila kuona mbele, haoni anapokanyaga ndiyo maana hatua zake za mafanikio zimetawaliwa na upofu.

Atafikaje anapotamani kufika bila kuwa na kiongozi kwenye giza hili ambalo tunaishi na kulifurahia bila hofu?

Kuna umuhimu mkubwa kwa wachezaji wetu kujitambua na kuwa na wasimamizi wazuri wenye maono makubwa ya vipaji vyao kuliko kuwa na wasimamizi ambao wanajali matumbo yao binafsi na kusahau maono ya mchezaji na mwisho wa siku kipaji cha mchezaji huangamia bila kufika sehemu ambayo ni kubwa.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version