Menu
in ,

TUMSOME , TUMWANDIKE NA KUMWELEWA SIMBU

Mashindano ya dunia ya riadha yamemalizika na kutuachia kitabu chenye fundisho kubwa kwetu.

Kitabu ambacho wengi wamekifunika na kukitelekeza kwa muda na wachache bado wanaendelea kukisoma taratibu.

Ndivyo tulivyo wanadamu, wengi huhamasika kwa muda kutokana na furaha ya muda lakini jambo likipita hatulichukulii maanani tena.

Na ndiyo maana huwa ni vigumu kwetu sisi kutengeneza mkondo wa mafanikio ya muda mrefu.

Simbu alikuja, tuko naye na mwisho wa siku atapita na kutuacha wapweke tena bila sehemu ya kujishikiza .

Kwenye kitabu chake cha mafanikio kuna swali katuuliza, tumeandaa mipango gani ya kuwapata kina Simbu wengine katika mfumo ulio bora zaidi ya mfumo aliopatikana yeye?

Ni Clinic ngapi ambazo zimepangwa kufanyika kwa mafanikio makubwa kwa ajili ya kupata watu sahihi ambao watakuja kuweka utawala wa riadha ?

Kitabu cha Simbu kinatuonesha dhahiri kuwa riadha ndiyo kitambaa sahihi cha kutufuta machozi wana michezo kama kukiwekwa uwekezaji wenye tija.

Hivi nini maana ya michezo ni biashara ?

Kwenye kitabu cha mafaninikio ya Simbu kimeelezea kwa kifupi sana kupitia DSTV.

Lakini kitabu kimetuachia na mwanga wa kutuonesha ni kipi ambacho tunatakiwa kufanya.

Ni wapi wafanyabiashara wanatakiwa kuwekeza ili wafike mbali kimataifa na bidhaa zao.

Simbu katuonesha riadha inafuatiliwa kwa kiasi kikubwa na watu wengi duniani na kuna uwezekano mkubwa wa kupenya kwenye riadha.

Kama kuna uwezekano wa kufanya vizuri kwenye riadha basi wafanyabishara wanatakiwa kuwa na imani na riadha.

Waamini riadha ni sehemu sahihi ya kutangaza bidhaa zao ili ziweze kufakia watu wengi .

Mfanyabiashara huwekeza sehemu ambayo anaona kuna faida.

Simbu ashatuonesha kwenye riadha kuna faida. Kuna haja ya kusita kutangaza bidhaa yako kupitia riadha ?

Miguu yote miwili inatakiwa kuingizwa kwenye uwekezaji wa riadha, ni moja ya sehemu ya mistari iliyopo kwenye kitabu cha Simbu.

Mistari ambayo inaniachia swali ambalo halina jibu kichwani mwangu.

Kuna mashindano maalumu ya kitaifa yanaandaliwa na RT? Kama yapo kwanini hayana mwamko mkubwa ?

Hatuwezi tegemea kupata wanariadha bora kwa kushushwa tu kama hatuna mashindano makubwa ya kitaifa na clinic bora za kutafuta wanariadha wa baadaye.

Kuna haja ya RT kuongea na wafanyabiashara wadhamini mashindano yao hasa hasa kipindi hiki ambacho kila mtu anaona kuna mwanga kwenye riadha.

Ni kipindi sahihi kwa mashindano makubwa nchini kama Kilimanjaro marathon yaanze kuendeshwa katika kiwango cha kimataifa.

Hakuna ongezeko la wadhamini katika mashindano haya. Ni mashindano ambayo kila uchwao hayashirikishi wana riadha wakubwa wa kimataifa. Na watu wengi huyatumia kama mazoezi na siyo mashindano.

Uwekezaji mkubwa unahitajika, kuanzia kwenye matangazo mpaka uendeshwaji.

Ni wakati sahihi kuwa na matangazo ya moja kwa moja ya mashindano haya ili yawafikie wengi na kujikuza zaidi.

Ni wakati sahihi sisi mashabiki wa michezo tuhamasike zaidi na riadha pia.

Tumeitenga sana riadha, ila riadha imekataa kututenga.

Simbu akiwa na mtangazaji wa EFM, Maulid Kitenge, aliyeambatana na timu ya Tanzania kwenye mashindano ya dunia jijini London.

Imezidi kutubeba kila tunapoonekana kuanguka, inazidi kutufuta machozi kila tunapoonekana tunalia.

Tusimkimbie mfariji wetu, tumkumbatie na kuambatana naye pamoja, na hiki ndicho kilichopo kwenye kitabu cha Simbu. Haina budi ya kumsoma, kumwandika na kumwelewa Simbu.

Yapo mengi ya kumwelewa Simbu, mimi nimwelewa sana kwenye mstari aliosema wakati tunafikiria kuzalisha wanariadha wapya tusisahau pia kufikiria kuzalisha makocha wa kuwafundisha wana riadha hawa.

Tuna idadi ndogo ya wazalishaji wa wanariadha ndiyo maana tuna wana riadha wachache sana ambao tunawapeleka kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Tumefikiria kuwa na timu nyingi za vijana angalau kila kanda ? Na tukawaandalia mashindano ya kanda angalau mara mbili kwa nwaka ?

Kipi ambacho kinaleta ugumu wa kuandaa mashindano makubwa ya riadha duniani angalau hata yale yanayoshirikisha vijana ? Swali hili lipo kwenye kitabu cha Simbu likiwauliza RT na Serikali.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version