Menu
in , , ,

Tumpe maua yake Kibu Dennis

Kibu Dennis

Hali hiyo ipo pia kwa Kibu Dennis ambaye uchezaji wake wa kasi, nguvu na kujituma kumempa nafasi ya kuonekana kwenye kikosi cha Simba mara kwa mara….

Tumefuzu mashindano ywa AFCON kwa namna yake. Jitihada, nguvu, maarifa na mkakati wa kuacha kuremba remba ulivisaidia Taifa Stars kupiga hatua mbele zaidi ya majirani zake Uganda maarufu kama The Cranes. Kati ya wachezaji wengi waliotoa mchango tangu mwanzoni mwa kampeni za kufuzu napenda kumchambua Kibu Dennsi. Ni supastaa wa mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu na washiriki pekee wa African Football League (AFL), Simba. Kibu Dennis ana hitsoria tofauti na nyota wengi walioko kwenye kikosi cha timu ya taifa. Ni mchezaji ambaye hata uchezaji wake unajitambulisha. 

KIBU DENNIS KAMA PAWASA

TANZANIASPORTS linafahamu kuwa nyota huyo wa Kitanzania anacheza soka la kufa na kupona, ni aina ya uchezaji uliowahi kuonekana kwa beki mahiri wa Simba, Boniface Pawasa. Katika ukuta mgumu wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Boniface Pawasa na Victor Costa walitengeneza kombinenga ya hatari ambayo iliwababaisha hata Zamalek ambao walichanganyikiwa siku walipotupwa nje ya mashindano ya CAF. 

Kulingana na uchunguzi wa TANZANIASPORTS, sifa kubwa ya Boniface Pawasa ilikuwa ni kujituma na kucheza kwa nguvu zote kuanzia dakika ya mwanzo hadi filimbi ya mwisho. Uchezaji wa ‘hapa kazi tu’ ndiyo uliokuwa unampa nafasi Pawasa kuwa nyota kwenye kikosi cha Simba. Pawasa akawa panga pangua, lakini alizidiwa kwa mbali kwa kipaji na mshirika wake Victor Costa. 

Hali hiyo ipo pia kwa Kibu Dennis ambaye uchezaji wake wa kasi, nguvu na kujituma kumempa nafasi ya kuonekana kwenye kikosi cha Simba mara kwa mara akipambana na nyota wa kigeni. Haikuwa rahisi kwa nyota wa Senegal Pape Sakho kumpokonya namba Kibu Dennis. Haikuwa rahisi kwa kwa Mmalawi Peter Banda kumpokonya namba Kibu Dennis. 

Aina ya uchezaji wake wa nguvu-kazi na kasi vinampa nafasi ya kupangwa mara kwa mara kulingana na mifumo. Pengine Kibu Dennis ni mchezaji wa mifumo ambayo anampa wasaa mzuri kocha wake kuongeza kasi ya timu dhidi ya wapinzani tofauti. Hiki ndicho kilichopo kwa Kibu Dennis na ndicho kinachochangia awe tofauti na wengine.

GUMZO LA URAIA 

Wakati Kibu Dennis aliposajiliwa na Simba liliibuka tatizo la uraia wake. Katika kipindi ambacho alicheza Ligi Kuu akiwa Mbeya City haikujulikana kama hakuwa raia halali wa Tanzania. Lakini maisha yake tangu utotoni akiwa na miaka 10 inasemekana ameishi Tanzania hadi alipoonekana Ligi Kuu. Simba walimsajili nyota huyo kutokana na umahiri wake si kwa sababu alitokea DRC au ingekuwa kwingineko. Ili aweze kucheza ilibidi sheria zitumike kumpa uraia wa Tanzania mahali ambako ni nyumbani kwake. 

Na sasa Kibu Dennis ametoa mchango mkubwa kwenye kikosi cha Simba na timu ya Taifa. Mchango mkubwa wa Kibu Dennis ulionekana nchini Algeria ambako aliongoza safu ya ushambuliaji akiwa na chipukizi wa Yanga, Clement Mzize. Nyota hawa walisaidiwa na mkongwe Simon Msuva, ambapo walimkosa nahodha wao Mbwana Samatta wa klabu ya POK. 

Tanzania Sports

Kibu Dennis anapokuwa uwanjani anampa nafuu kocha kwenye kusaidia ulinzi. Ni winga, mshambuliaji na kiungo mshambuliaji ambaye anaweza kurudi nyuma kusaidia ulinzi. Mbio na kasi ni silaha muhimu sana kwa Taifa Stars. Kibu Dennis ni mchezaji ambaye anatumikia mfumo wa soka na anawajibika bila kuchoka. Hii ni sehemu muhimu, na ambayo bila shaka mamlaka za Tanzania zilishauriwa vizuri kuhusu kumpa uraia nyota huyo bila kusita sita. Waliopondekeza, waliopokea na waliotekeleza uamuzi wa kumpa uraia Kibu Dennis wapongezwe kwa usikivu na bila shaka kocha Kim Poulsen anao mchango wake. Heko kwa TFF.

SI VIPAJI VYA AJIBU, ATHUMAN

Kibu Dennis anajituma sana, ana nguvu na kasi kubwa, lakini hana kipaji kikubwa kama Yusu Athuman au Ibrahim Ajibu. Hilo ni sawa na lilivyokuwepo wakati wa Boniface Pawasa na Victor Costa. Ni wazi nyota hao wawili walikuwa na vitu adimu na tofauti. Victor Costa alikuwa mahiri na kipaji kikubwa, angeweza kutuliza mpira kwa madoido na kupiga chenga kwenye boksi la eneo la hatari kisha ukashindwa kumpokonya mpira. Wakati mwingine ninapomtazama Kalilou Koulibaly huwa namfikiria Victor Costa, ubabe, kipaji,kujiamini na maarifa wamejaaliwa. 

Yusuf Athuman alikuwa nyota wa Yanga na hivi karibuni ameripotiwa kwenda barani Ulaya ambako ameshasajiliwa. Kijana huyo ukimtazama anavyopokea mpira,kutoa pasi, mikimbio na maamuzi anayofanya unamwona kabisa ana kipaji kikubwa cha kandanda lakini hana ile ‘spirit’ ya Kibu Dennsi. Hali kadhalika Ibrahim Ajibu ana kipaji kikubwa sana lakini anakabiliwa na tabia za uvivu,uzembe na kutojituma. Wakati mwingine Ibrahim Ajibu hunikumbusha tabia za uzembe na uvivu za Mario Balotelli. Ni nyota wenye vipaji vikubwa lakini hawana tabia za Kibu Dennis au Boniface Pawasa. 

Hadi tulipo sasa ni dhahiri Kibu Dennis anatakiwa kupewa maua yake. Kibu apewe maua yake kwa uchezaji wa aina yake ambao hata Yanga wanamtambua kwa kombora kali alilowatandika kwenye mechi za Ligi Kuu. Ari, nguvu, kasi, kujituma muda wote wa mchezo ndizo siri za nyota huyu. Akianza ndivyo anavyomaliza, hii itawafanya makocha wengi watamani kuwa naye kikosini. Kamwe hakuna kocha anayependa wachezaji wavivu,wazembe na wasiojituma kwenye kikosi chake. Ukibisha angalia ugomvi mpya wa kocha wa Manchester United, Erik Ten Hag na nyota wake Jadon Sancho.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version