Menu
in , ,

Tumkabidhi rasmi Rashford jezi namba 10

Tanzania Sports

Wakati Wayne Rooney anatangaza kutoendelea kucheza akiwa na jezi ya Manchester United, wengi hapa England tuliona kama utani.

Tuliona ni kitu ambacho kimetokea kwa muda mfupi sana, yani kilikuwa kimewahi sana. Tuligemea kuendelea kumuona Wayne Rooney kwa muda mrefu zaidi.

Miaka 31 pekee ilikuwa miaka michache sana kwake yeye kuiacha Manchester United. Klabu ambayo ameitumikia tangu akiwa na miaka 18.

Klabu ambayo alitumia muda wake mwingi wa kucheza mpira akiwa nayo. Alifanya mengi sana ya kukumbukwa akiwa na Manchester United.

Alifunga sana, tena magoli ambayo yalikuwa yamebeba hisia kubwa sana kipindi tulipokuwa tunayatzama. Ni nani ambaye hakusisimka mpaka unywele kwenye goli alilofunga dhidi ya Manchester City kwa Bicycle Kick?.

Midomo ilibaki wazi, tulijisahau kwa sekunde kadhaa, baadaye tukaja kukumbuka baadaye kuwa tunatakiwa kushangalia lile goli.

Ni aina ya magoli ambayo hufungwa na kukaa kwenye nyavu za ubongo wa mwanadamu. Magoli yale ni nadra sana kukaa kwenye nyavu za goli.

Hubaki kuwa kumbukumbu kubwa sana ndiyo maana hukaa kwenye nyavu za ubongo wa mwanadamu.

Hiki ndicho kilichotufanya tumkumbuke Wayne Rooney. Mchezaji ambaye alikuwa na uwezo wa kufunga kila aina ya magoli.

Goli lipi hajafunga?, magoli ya mbali?, magoli ambayo watangazaji wengi wa mechi walikuwa wanayapenda sana kuyatangaza.

Kulikuwa na burudani mbili ambazo tulikuwa tunazipata. Macho yangu yalikuwa yanaburudika kila nikitazama aina hiyo ya magoli.

Lakini sikio langu lilikuwa linaburudika zaidi kila nilipokuwa nasikia Charles Hillary akisimulia aina hiyo ya magoli ya Wayne Rooney.

Huyu ndiye nyota mkubwa wa klabu ya Manchester United. Wamepita wengi sana. Najua dunia itawakumbuka kina Sir. Bobby Charlton.

Na dunia ingetamani kuendelea kumuona Cristiano Ronaldo akiendelea kuitumikia kwa muda mrefu Manchester United.

Wengi wanaamini rekodi nyingi sana. Na angemfanya Wayne Rooney asifike sehemu ambayo aliifikia kipindi akiwa Manchester United.

Ndiye mfungaji bora wa wakati wote wa Manchester United. Huyu ndiye nembo kubwa kwa Manchester United kwa sasa.

Alikuwa mchezaji wa ajabu sana. Hakuwa na kipaji cha kutisha kama vipaji ambavyo huzaliwa Brazil.

Hakuwa na uwezo mkubwa wa kuburudisha kama kina George Best. Lakini alikuwa na nguvu kubwa ya kufanya chochote akiwa amepewa jukumu lolote.

Jukumu gani ambalo alipewa na akaacha kulitimiza? Alitumikishwa ipasavyo na yeye akatumikia ipasavyo bila kinyongo chochote.

Alipotakiwa kucheza nyuma ya mshambuliaji alifanya hivo bila kinyongo na alicheza kwa kiwango kikubwa sana.

Alipotakiwa kucheza kama mshambuliaji wa mwisho alifanya hivo , hata aliporudishwa kucheza kama kiungo wa juu alicheza.

Tabasamu lake halikuisha moyoni kila alipokuwa anatakiwa kucheza namba yoyote. Ni ngumu kuamini kuwa huyu binadamu alicheza kama kiungo wa chini.

Na alifanikiwa kutimiza majukumu yake vizuri sana. Na timu ikashinda. Kwa kifupi huyu alikuwa punda wa makocha wengi waliopita pale Manchester United.

Alex Ferguson alimtuma atakavyo, na yeye alitimiza alichokuwa anatumwa. Baya David Moyes alimtumikisha sana.

Hata alipokuwa Louis Van Gaal alikuwa tayari kufanya naye kazi ndiyo maana hata alipokuwa anapewa nafasi ya kucheza kama kiungo alifanya hivo.

Alifanya hivo pia hata kipindi cha Jose Mourinho. Yeye kwake mpira ulikuwa kazi kubwa kuzidi kazi zote duniani. Alikuwa tayari kucheza hata kila kipindi ambacho angehitajika.

Wakati was zamani kidogo kila tulipokuwa tunamuona mchezaji kavaa jezi namba 10 tulijua kabisa huyu ni mchezaji hatari zaidi.

Ni jezi ambayo ilikuwa imebeba maana ya neno “kipaji”. Ilikuwa ni ngumu kukuta mchezaji mwenye jezi namba 10 akiwa hategemewi kwenye timu.

Wayne Rooney alikuwa tegemeo kubwa kwenye timu. Alihubiri vizuri injili ya jezi namba 10. Alizidi kutukumbusha kuwa mchezaji kwenye jezi namba 10 anatakiwa awe tegemeo kubwa kwenye timu.

Ndiyo maana alipoondoka katika klabu ya Manchester United wengi tulisubiri kuona ni nani ambaye angeweza kupewa hiyo jezi.

Ni nano ambaye angeweza kuwa mchezaji tegemeo baada ya Wayne Rooney kuondoka. Marcus Rashford mgongo wake ulipata baraka zote.

Alivaa rasmi jezi namba kumi ya Manchester United. Kipindi cha Jose Mourinho hakuonekana kama mchezaji ambaye angeweza kuwa tegemeo katika kikosi cha Manchester United.

Kuanzia benchi kwake kilikuwa kitu cha kawaida. Wengi walikuwa hawajaridhishwa na kitendo cha jezi namba 10 kupewa mchezaji ambaye hutokea benchi.

Lakini kwa sasa ni tofauti, Marcus Rashford ni tegemeo katika kikosi cha Manchester United. Dalili za yeye kujitengenezea ufalme wake zinaonekana. Ufalme ambao unatuachia swali kama ni wakati sahihi kumkabidhi Rashford jezi.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version