Menu
in ,

TULIMSUBIRI NEYMAR, AKAJA SALAH

Kivuli cha Lionel Messi ndicho kilichomtoa, hakutaka kusimama kwenye
kivuli cha mtu mwingine ilihali kivuli chake kikiwa kimesinyaa.

Mawazo yake na matamanio yake makubwa yalikuwa kujenga Ufalme wake
mwenyewe. Ufalme ambao atapokea heshima kubwa kila sehemu ya dunia.

Aliamini ndani ya Ufalme wake atakuwa huru kufanya maamuzi yoyote
aliyokuwa anayatamani kuyafanya pale Barcelona.

Akazidi kuamini ndani ya Ufalme wake kila mtu atamwabudu na kusujudu
mbele yake, waimbaji wote alitamani wamtungie nyimbo za kumsifu yeye
na kumwabudu yeye kama bwana wa mpira wa miguu.

Mitandao yote ya kijamii alitaka kuiteka ili iwe inamzungumzia yeye
juu ya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, hata mikataba ya kibiashara
na makampuni mbalimbali alitamani aipate yeye.

Neymar
Neymar

Aliona ni muda sahihi kwake yeye kumiliki Ufalme, PSG ikampokea na
yeye akaipokea kama sehemu ya kwake yeye kujenga Ufalme wake.

Taratibu changamoto za Ujenzi zikawa zinaonekana, Edson Cavan kuwepo
pale kama mpigaji rasmi wa penalti ikawa changamoto ya kwanza lakini
haikuwa ngumu kwake alifanikiwa kuiruka.

Siku zikazidi kukimbia, alionesha uwezo wake ambao ulitufanya tuamini
kijana wa kutoka Brazil kaamua kweli kweli kupigania Ufalme wake.

Alionesha njaa ya Ballon D’or, alitumia miguu yake kama silaha
kuwaadhibu makipa na mabeki wa timu pinzani. Nyavu za goli zilikuwa
zinafurahia uwepo wake uwanjani kwa sababu zilijua wakati wowote
zitacheka.

Kuna wakati watu walidhani anaziadhibu timu ambazo zinaonekana dhaifu,
macho yetu yakawa yanasubiri mechi za klabu bingwa barani ulaya tuone
hasira zake za kujenga Ufalme wake imara.

Shindano hili ndilo shindano lenye mvuto, limebeba hisia halisi za
mpira wa miguu na ndilo shindano lenye ushawishi mkubwa kwenye kupata
tunzo ya Ballon D’Or.

Hatua ya mtoano ilianza, Real Madrid ndiyo ulikuwa mtihani wa kwanza
kwa Neymar, tulitegemea kumuona atakavyoibeba timu yake mbele ya klabu
ambayo ni kubwa , klabu ambayo ina wachezaji wenye hadhi ya juu na
kizuri zaidi ndiyo klabu ambayo inatetea taji hili.

Hakuna kikubwa alichokifanya kuwashawishi wengi kuwa wakati wake wa
kusimama juu ya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi umefika.

Swali kubwa kwetu lilibaki ni nani atasimama katikati ya Lionel Messi
na Cristiano Ronaldo?, hatukutaka kuamini kuwa kuna mchezaji ambaye
anaweza kusimama juu ya hawa Wafalme.

Tulimtazama Mohammed Salah ƙkatika jicho lenye mashaka ndani yake,
hatukuweza kumwamini na kumpa nafasi moja kwa moja kuwa anaweza
kusimama katikati yao.

Tuliogopa kuingia makubaliano ya kibiashara naye, hii haikumzuia yeye
kuinadi bidhaa yake. Aliamini kupitia ubora wa bidhaa yake ndiyo maana
hakuchoka kuiboresha kila siku.

Aliibeba Liverpool, hata siku walipokutana na Manchester City wengi
walijua ndiyo safari ya mwisho kwa Liverpool.

Lakini Mohammed Salah alisimama na kutuonesha kuwa ni muda sahihi
kwetu sisi kumwangalia kama mshindani sahihi wa Cristiano Ronaldo na
Lionel Messi.

Mechi tano mfululizo alizoanza kwenye michuano ya klabu bingwa ulaya
msimu huu akifunga goli kwenye kila mechi na kufanikiwa kufikisha
idadi ya magoli kumi nyuma ya Cristiano Ronaldo mwenye magoli kumi na
tano.

Amevunja rekodi ya Roger Hunt, gwiji wa Liverpool mwenye magoli mengi
katika timu ya Liverpool nyuma ya Ian Rush.

Roger Hunt aliwahi kumaliza msimu mmoja akiwa na magoli 42, lakini
jana Mohamed Salah kafikisha magoli 43 akibakiza magoli manne kuvunja
rekodi ya Ian Rush mfungaji bora wa muda wote wa Liverpool aliyemaliza
msimu akiwa na magoli 47.

Mwanga tayari ushaanza kuonekana mpaka sasa Salah ana magoli 43,
Cristiano Ronaldo akiwa na magoli 42 na Lionel Messi akiwa na magoli
40 .

Hapana shaka hawa ndiyo farasi watatu ambao watakuwepo kwenye mbio za
kuwania Ballon D’or tofauti na mwanzoni tulivyokuwa tunawaza kuhusu
Neymar.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version