Menu
in

TULIIACHA MIGUU YA MWANJALI TUMEAMINI ILIYOKUWA MIGUU YA WAWA

Tanzania Sports

Historia imebeba alama katika maisha ya mwanadamu yoyote yule. Kila nafasi anayopata mwanadamu huweka alama ambayo hudumu kwa muda mrefu.

Kitu ambacho hakiwezi kudumu milele ni nguvu na uwezo ambao mwanadamu alitumia kuweka alama wakati amepata nafasi ya kufanya kitu ambacho alitakiwa kufanya.

Nguvu hupungua na uwezo hupotea baada ya muda na hii ni kwa sababu hakuna kitu kinachokuja kukaa milele kwa mtu.

Hapa ndipo utakapokumbuka kuwa Diego Maradona aliweka alama kubwa katika ulimwengu huu wa Soka, alama ambayo kwa sasa tunaikumbuka lakini nguvu zake alizotumia kutengenezea alama hizo hazipo tena miguuni mwake.

Miguu haina nguvu tena na hii ni kwa sababu umri umemwacha, umri ni kitu kikubwa kwa mchezaji wa mpira wa miguu.

Kuna wakati mchezaji huwa na kasi kubwa sana lakini kuna umri hufika kasi yake hupungua kwa kiasi kikubwa.

Umri ndiyo ilikuwa sababu ya Mwanjali kuachwa na klabu ya Simba. Mchezaji ambaye alikuwa mkomavu na kiongozi mahiri.

Uwezo wake ulikuwa mkubwa zaidi ya vijana ambao walikuwa wachanga kwake, miguu yake ilikuwa ina ukomavu wa hali ya juu hata kasi ilikuwa haijaanza kupungua katika miguu yake.

Hakubahatisha kitu chochote alipoamua kumfuata mchezaji yoyote kumkaba, kiufupi alikuwa kisiki ambacho kilikuwa bado kinahitajika ndani ya kikosi cha Simba.

Lakini cha kusikitisha hakuweza kuendelea ndani ya kikosi cha Simba sababu kuu ikiwa ni umri kuwa mkubwa.

Jambo ambalo linamsingi mkubwa katika maendeleo ya mpira kwa sababu nilihisi huu ndiyo utakuwa wakati mzuri kwa Simba kutumia vijana wachanga wenye vipaji baada ya Mwanjali kutoka.

Lakini imekuwa tofauti na kanuni za maendeleo ya soka, wameleta mchezaji ambaye hafiki kiwango cha Mwanjali na ana umri sawa na wa Mwanjali.

Paschal Wawa aliwahi kuwa mchezaji mkubwa na mwenye kiwango kikubwa miaka mitano iliyopita.

Miaka imeenda, siku zimesogea sana kiasi kilichopelekea mpaka kiwango chake kuwa hafifu ndani ya miaka ya hivi karibuni.

Paschal Wawa siyo yule ambaye tulizoea kumuona miaka mitano iliyopita. Kasi yake imepungua sana na nguvu kwenye miguu imetoweka kwa kiwango kikubwa.

Hana nguvu kubwa tena ya kupambana na wachezaji wenye kasi katika dunia hii ya mpira wenye kasi kila muda.

Simba wanaenda kutuwakilisha kwenye michuano ya kimataifa. Ni sahihi kwao kusajili wachezaji aina ya kina Paschal Wawa? Mchezaji ambaye anabebwa na historia yake nzuri ambayo aliiweka kipindi kile ambacho miguu yake ina nguvu na kasi?

Walimchunguza kwanza kabla ya kumsajili au walimsajili ili kumkomoa fulani? Tutaishi maisha ya kukomoana mpaka lini kwenye dunia hii inayohitaji mipango dhabiti ili ufanikiwe kufika kwenye kilele cha mafanikio?

Hapana shaka Simba kama walimwacha Mwanjali kwa kisingizio cha Umri walipaswa kuachana na usajili wa wachezaji aina ya kina Mwanjali.

Huu ulikuwa muda wao kusajili wachezaji ambao wangeisaidia Simba kufika mbali katika michuano ya kimataifa kuliko kumsajili mchezaji kwa sababu aliwahi kuwa mchezaji nyota bila kufanya uchunguzi kama umahiri wake wa kipindi cha nyuma bado upo mpaka sasa hivi.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version