Nimezikumbuka zile nyakati. Nyakati za Ibrahim Ajib akiwa kwenye uzi wa njano na kijani katika mitaa ya jangwani. Nyakati ambazo Ibrahim Ajib alikuwa mfalme haswa ndani ya kikosi cha Yanga.
Hakukuwepo na mchezaji mkubwa wakati anacheza Yanga. Yanga ilikuwa inaunga unga. Kesho yao ilikuwa ngumu kuzidi leo na jana yao. Kila kesho ilipokuwa inawadia ilikuwa ngumu kwao.
Hawakuwa na uhakika wa kupata mishahara ya wachezaji , hawakuwa na uhakika wa kupata pesa za kuisafirisha timu yao kwenda mikoani kwa ajili ya mechi za ligi kuu.
Hawakuwa na uhakika wa kupata ushindi kipindi hicho kwa sababu kikosi chao kilikuwa cha kawaida sana. Kikosi ambacho kilikuwa hakina uwezo wa kuipa Yanga uhakika wa alama tatu, ubingwa kwao halikuwa lengo kubwa.
Kikosi chao kiliwapa nafasi ya wao kuwa wanyonge. Hawakuwa na nafasi ya kutamba mbele ya wenzao ambao ni Simba. Katikati ya kikosi chao cha kawaida walikuwepo Ibrahim Ajib pamoja na Makambo.
Ibrahim Ajib alikuwa na uwezo wa kutengeneza magoli kwa wingi sana. Msimu huo alimaliza akiwa na jumla ya pasi 20 za magoli. Wakati Ibrahim Ajib akimaliza msimu akiwa na pasi za mwisho 20 Makambo alimaliza msimu akiwa na magoli 18.
Hawa angalau waliifanya Yanga ipumue kwa kipindi hicho. Ibrahim Ajib alipika magoli mengi na Makambo alifunga magoli mengi. Magoli mengi aliyofunga Makambo yalikuwa ya kichwa. Alitumia kichwa chake ipasavyo kufunga magoli.
Kila mpira uliokuja juu kwa kupitia mpira wa adhabu ndogo, kona, faulo au krosi Makambo aliruka juu na kuutumia ipasavyo mpira huo. Makambo alikuwa na ufanisi mkubwa sana kwenye mipira ya juu.
Leo hii Yanga imefanya usajili mkubwa sana ndani ya kikosi chao. Kila idara ina wachezaji ambao ni bora. Lakini kuna wachezaji wawili ambao naona wanamkosa sana Makambo katika kikosi cha Yanga.
Tuisila Kisinda ni mchezaji wa kwanza ambaye ana mkosa sana Makambo katika kikosi cha Yanga. Ni mchezaji ambaye anatokea pembeni. Mara nyingi huwa anapiga sana krosi kwenye lango la timu pinzani.
Tatizo kubwa ambalo kwa sasa lipo kwenye kikosi cha Yanga ni namna ambavyo krosi za Tuisila zinavyokosa mtu wa kuzitumia kwa ufasaha. Krosi nyingi zinapotea kwa sababu hakuna mtu ambaye anauwezo wa kuzitumia kwa ufasaha hizo krosi.
Mchezaji wa pili ambaye anamkosa Makambo ni Carlinhos. Huyu ameshajitanabaisha kuwa ni mchezaji mzuri kwenye kupiga mipira iliyokufa . Lakini mipira mingi anayoipiga hakuna anayeicheza kwa ufasaha hiyo mipira ya juu.
Inawezekana Yanga imefanya usajili mzuri na mkubwa lakini hawajabahatika kupata mtu ambaye ana uwezo wa kucheza mipira ya juu kama alivyokuwa Makambo. Kwa sasa mipira hii ya juu inazalishwa kwa wingi na Kisinda pamoja na Carlinhos.