TUIPUMZISHE TFF MZIGO , TUINGIE WOTE VITANI
Kuna vingi vya kujivunia Watanzania katika nchi yetu, kikubwa ambacho
huwa tunatembea nacho kifua mbele ni amani na mshikamano tulio nao.
Amani na mshikamano ambao umetengenezwa na makabila zaidi ya 120
ambayo yote kwa pamoja yameunganishwa na lugha moja kubwa ambayo kwa
sasa inazungumzwa sana Afrika yani Kiswahili.
Lugha ambayo imetufanya Watanzania wote kuwa wamoja kitu ambacho
kinampelekea hata Msukuma kutoka Mwanza, Simiyu au Shinyanga kuwa na
uhuru wa kwenda kuishi na kutafuta ujira wake kwa Wamakonde huko
Mtwara bila bughudha yote.
Kila Mtanzania amekuwa akijivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya amani ya
nchi yetu kwa sababu kwa namna moja au nyingine tumekuwa
tukishirikiana kwa lugha moja ambayo hutufanya tuelewane.
Kiswahili ni lugha yetu ya Taifa , Mpira ni lugha yetu ya Dunia,
lugha ambayo huunganisha Mataifa mengi ambayo huzungumza lugha tofauti
lakini wakazungumza lugha moja ambayo ni mpira.
Mshikamano ndicho kitu ambacho huzaliwa kwa kiasi kikubwa pindi watu
wanapozungumza lugha moja, kwa furaha tena kwa pamoja.
Mshikamano ndiyo huleta ushindi kwenye lugha hii ya mpira, ni ngumu
sana kwa nchi au klabu kuwa mshindi wa soka bila kupata mshikamano.
Hii ndiyo nguzo muhimu ya kupata furaha katika mpira, mara ya mwisho
kwetu sisi kupata furaha kwenye soka ilikuwa miaka 37 ambao ni umri wa
mtu mzima.
Sekunde zimesogea kukaribisha dakika ambazo zilipewa fursa za
kukaribisha masaa ambayo hayakuwa na hiyana kutengeneza siku ambazo
kwa pamoja zilituwezesha kupata miezi mingi iliyotufikisha takribani
miaka 37 iliyopita kupata furaha ya dhati kwenye soka.
Mwaka 2013 TFF ilianza kutekeleza programu yake ya vijana kwa ajili ya
kupata timu bora ambayo ingetuletea mafanikio na fahari kubwa
tuliyoisahau miaka 37 iliyopita.
TFF imefanya kazi kubwa sana kuanzia kutafuta benchi sahihi la ufundi
la timu ya taifa, ambalo lilihangaika kutafuta wachezaji sahihi ambao
walitakiwa kuingia kwenye timu ya Taifa ya vijana ambao walilelewa na
kutafutiwa mazingira bora na TFF.
TFF imefanya kadri ya uwezo wao kuwatengenezea mazingira mazuri hawa
vijana kuanzia kwenye mahitaji muhimu ya mwanadamu kama chakula,
malazi na mahitaji mengine.
Hawakutaka kuishia kuwapa mahitaji muhimu pekee, pia walitoa nafasi ya
timu ya Taifa ya vijana Serengeti boys kukaa pamoja kwenye hosteli za
TFF ili wazoeane kwa pamoja na vyote hivi vilikuwa vinagharamikiwa kwa
nguvu kubwa ya TFF.
Mechi za kimataifa za kuiimarisha timu ya Taifa ya vijana iliyochini
ya umri wa miaka 17 zilitafutwa, mataifa mbalimbali yalikuja hapa
kuwapima uwezo vijana wetu.
Kama kwamba haitoshi TFF ilifanikiwa kuipeleka timu hii India
kushiriki mashindano maalumu ya vijana ambayo yaliwajenga sana vijana
wetu hawa ambao leo hii tunapozungumza wapo Morocco wakijiandaa na
fainali za Afcon ya vijana nchini Gabon.
Bega la TFF ƙlimebeba mzigo mzito kwa umbali mrefu, muungwana
anahitajika kwa ajili ya kumtua huu mzigo tena ukizingatia TFF
inawalea na kuwasomesha watoto waliochini ya umri wa miaka 15 pale
Alliance.
Ni muda wa sisi Watanzania kuingia katika vita kama ilivyokuwa kwenye
vita ya Kagera ya kung’oa utawala wa nduli Idd Amini ambapo Watanzania
wengi walijitolea mali zao, damu, fedha na hamasa mpaka ushindi
ukapatikana ndicho kitu ambacho Watanzania tunatakiwa tufanye ili tuwe
sehemu ya mafanikio ya mpira wetu kupitia hawa vijana wa Serengeti
boys.
Lugha yetu inatuunganisha pamoja, muungano ambao umekuwa na matokeo ya
sisi Watanzania kuwa na mshikamano mkubwa. Ni wakati sahihi
tushikamane kuichangia Timu yetu ya Serengeti boys kwa chochote kile
kidogo tulichonacho ambacho naamini kupitia hicho kidogo tutazalisha
kitu kikubwa ambacho kitatupa lugha ya pamoja inayoitwa furaha
Watanzania wote.
Kuna njia za kuichangia timu yetu hii popote ulipo , mfano kwa njia ya
simu waweza kuchangia chochote kile, iwe mia kupitia namba 0687 333
222 au Account ya Benki ya DTB 00 866 280 03.
Kama ilivyokuwa furaha kwa Watanzania kuwa kati ya watu walioshiriki
mafanikio ya ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika basi ni wakati
sahihi kwetu sisi Watanzania kushiriki katika mafaniko ya soka letu la
Tanzania kupitia kuichangia timu yetu ya vijana ya chini ya umri wa
miaka 17.
TFF imeshatutafunia nyama ngumu, ikatulainishia imebaki sisi kumeza.
Nchi hujengwa kwa nguvu za wananchi wote kuungana kwa pamoja, ni ngumu
kupata mafanikio sehemu ambayo hakuna mshikamano kitu ambacho sisi
tumebalikiwa nacho.
Tutumie ushikamano wetu tulionao kuhakikisha siku moja nchi yetu
inatamanika na kila nchi katika maendeleo ya soka.
Neno uzalendo halitoshi kutamkwa mdomoni peke yake bila ya kushiriki
matukio ambayo ni ya kizalendo.
Hii timu ni yetu sote, sisi ndiyo baba na mama wa hii timu tunatakiwa
tushiriki kuielea kwa pamoja. Malezi bora ya mama na baba kwa pamoja
huleta mtoto bora.
Ni ndoto yetu Watanzania kuona timu yetu ya Taifa ikishiriki
mashindano makubwa duniani, kushiriki kwa mashindano makubwa duniani
kwa timu yetu ya taifa ya wakubwa hakuanzii kwa kupata wachezaji
wakiwa wakubwa, ila kunaanzia kulea kwanza vijana katika misingi ya
kisoka. Na moja ya vitu vinavyojenga vijana ni wao kupata motisha
ambayo hupandisha morali ya kupigana.
Tunataka vijana wetu wapigane kwa kiasi kikubwa huko Gabon, ili
wafanikiwe kupata nafasi ya kushiriki michuano ya dunia ya vijana
waliochini ya umri wa miaka 17 nchini India.
Tunatakiwa kwenda wote Gabon mpaka India, hata kama hutopata nafasi ya
kwenda Gabon au India kuishabikia na kuiunga mkono timu yetu ya
Serengeti boys ila una nafasi kubwa ya kuishabikia na kuiunga mkono
kupitia mchango wako mdogo ulionao ili kuongeza hamasa kubwa kwenye
kikosi cha yetu ya Taifa ya vijana waliochini ya umri wa miaka 17.
Vijana wametuonesha wana nia ya kufika mbali, TFF wamewatunza kwa
kiasi kikubwa sasa ni wakati wa Taifa kuingia vitani kwa pamoja, kama
ilivyokuwa senti 10 ya bibi yangu ilivyosaidia ushindi wa vita ya
Kagera nina uhakika sh. Mia yako itasaidia kwa kiasi kikubwa kutia
hamasa mafanikio ya timu yetu ya vijana walio chini ya umri wa miaka
17 yani Serengeti boys.