Menu
in

Tuendelaa kuipa moyo Taifa Stars…

JUZI timu yetu ya soka ya taifa,Taifa Stars ilicheza mechi ya kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika CAN dhidi ya Algeria kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Fainali za 28 za Mataifa ya Afrika zinatarajiwa kufanyika katika nchi za Gabon na Guinea ya Ikweta kuanzia Januari 21 mpaka Februari 12, 2012.

Taifa Stars ambayo ipo katika kundi D pamoja na nchi za Jamhuri ya Afrika ya Kati, Algeria na Morocco ilianza harakati zake za kutaka kufuzu kushiriki katika fainali hizo za mataifa ya Afrika kwa kucheza na Algeria na kutoka nayo sare ya 1-1, kabla ya kucheza na Morocco na kufungwa bao 1-0, Stars iliichapa Jamhuri ya Afrika ya Kati 2-1, pia ilifungwa na Jamhuru ya Afrika ya Kati 2-1 na kutoka sare 1-1 na Algeria.

Hivi sasa Stars imebakisha mechi moja dhidi ya Morocco mechi itakayochezwa mjini Rabat kati ya tarehe 7,8,9 mwezi Oktoba, 2011.

Ni wazi Taifa Stars baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Algeria juzi kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam imejiweka katika mazingira magumu ya kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani.

Lakini, hata hivyo huu siyo wakati wa wachezaji wa Stars, viongozi wa soka, serikali na mashabiki wa soka nchini kukataa tamaa kwa sababu kila timu inayomaliza ikiongoza kundi katika hatua hizi za kufuzu ndiyo inayofuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika, ingawa zipo nafasi mbili kwa ajili ya timu zilizofanya vizuri na kumaliza katika nafasi ya pili.

Ukiangalia msimamo wa kundi D ambalo ipo Taifa Stars utaona Tanzania inashika nafasi ya tatu na ina pointi tano wakati Algeria inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi tano.Timu zingine ambazo zipo kwenye kundi hilo ni Morocco inayoongoza ikiwa na pointi saba ikifuatiwa na Jamhuri ya Afrika ya Kati yenye pointi saba pia.

Hata hivyo jana Morocco na Jamhuri ya Afrika ya Kati zilikuwa zikicheza mjini Bangui, ambapo kama timu hizo zimetoka sare basi zitakuwa zimefikisha pointi nane kila moja na kama timu moja imeifunga nyingine basi mojawapo itakuwa imefikisha pointi 10 na nyingine kubaki za pointi saba.

Hivyo nafasi ya kufuzu bado ipo kwa timu zote za Kundi D kwa sababu mechi za mwisho ndizo zitakazoamua timu ipi ifuzu na timu ipi iwanie nafasi mbili kwa ajili ya timu zilizofanya vizuri na kumaliza katika nafasi ya pili katika kila kundi.

Ukiacha mechi ya mwisho ya Stars dhidi ya Morocco mjini Rabat, timu ya Algeria yenyewe itaikaribisha Jamhuri ya Afrika ya Kati na kama Taifa Stars itaifunga Morocco katika mechi yake ya mwisho Stars itakuwa imefikisha pointi nane, lakini kama Jamhuri ya Afrika ya Kati imeifunga Morocco katika mechi ya jana itafikisha pointi 10 na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu, pia Morocco ikishinda mechi yake dhidi ya Stars au kama imeshinda mechi yake ya jana itakuwa imefikisha pointi 10 na kuwa na uhakika pia wa kufuzu.

Tunaamini vijana wa Taifa Stars hawatakata tamaa na kuhakikisha wanakamilisha ratiba ya mashindano haya ya kufuzu kwa uwezo wa juu kama walivyocheza katika mechi ya juzi dhidi ya Algeria.

Tunaamini wachezaji wa Stars wanahitaji pongezi na walionyesha kulipigania taifa kwa hali na mali, walicheza kitimu, walijituma, walitengeneza nafasi nyingi za ushindi ila bahati haikuwa yao.

Tunatarajia kuona TFF, wadhamini, mashabiki pamoja na serikali wakiendelea kumpa ushirikiano mzuri kocha Jan Poulsen kwa ajili ya mechi ijayo na tunaamini kocha Poulsen ataweza kuchagua tena wachezaji ambao wataipeperusha vizuri bendera ya Tanzania na kuwaandaa vizuri kwa ajili ya kuhakikisha ushindi unapatikana.

Tunawapongeza pia mashabiki wengi wa soka nchini ambao walijitokeza kuishangilia Taifa Stars na kuacha tabia yao ya kushangilia wachezaji wa timu za Simba na Yanga tu waliopo kwenye kikosi cha Taifa Stars.

Mashabiki wa soka wa Tanzania walichangia kwa kiasi kikubwa kuwaongezea hamasa vijana wa Stars katika mechi dhidi ya Algeria kutokana na moyo wao wa uzalendo wa kuwashangilia ambao watanzania wanatakiwa kundelea nao bila kukata tamaa hata tukifungwa.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version