Menu
in , , ,

TOFAUTI YA SIMBA YA MSIMU ULIOPITA NA MSIMU HUU

Tanzania Sports

1: Kuna mengi ya kuumiza na kuna wakati mwingine yanakera sana hasa hasa unapotumia nguvu nyingi mwanzoni zikakuishia mwishoni. Hiki ndicho kitu ambacho Simba kilikuwa kinawakera na kuwaumiza sana hasa hasa msimu uliopita. Walifanikiwa kuongoza kwa tofauti ya alama nane dhidi ya Yanga lakini mwisho wa ligi Yanga ilichukua ubingwa kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa. Na hii ni kutokana na presha kubwa ya kutaka ubingwa iliyokuwa ndani ya kikosi cha Simba, viongozi na mashabiki.

Presha hii iliwafanya wachezaji wa Simba kukosa umakini kutokana na shinikizo la ubingwa lililokuwa ndani yao.

Hiki kitu hakikuwepo msimu huu, Simba ilifanikiwa kuongoza kwa tofauti ya alama 7 msimu huu lakini Yanga walifanikiwa kulingana alama na Simba. Wengi walitegemea kitatokea kama kilichotokea msimu jana lakini hali ilikuwa tofauti sana. Wachezaji wa Simba, viongozi na mashabiki wa Simba walikuwa watulivu na hawakuruhusu presha kubwa ndani yao kitu ambacho kiliongeza umakini mkubwa ndani ya kikosi cha Simba.

2: Kuna ile kauli inayosema watu hujifunza kulingana na makosa. Makosa ni mwalimu mkubwa wa mwanadamu. Na hiki ndicho kitu ambacho Simba wamekionesha kwa vitendo kwani msimu jana hawakuchukua ubingwa kwa sababu ya tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa. Yanga walifunga magoli 57 na kufungwa magoli 14 na tofauti ya magoli ya kufungwa na kufunga ikawa 43 wakati Simba ilifunga magoli 50 na kufungwa magoli 17 na tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa ikawa 33. Hii ni tofauti na msimu huu ambapo Simba imefunga magoli 59 na kufungwa magoli 13 na tofauti ya magoli ya kufungwa na kufunga ni 46 wakiwa wamewazidi Yanga ya msimu uliopita kwa magoli matatu (3).

3: Safu ya Ulinzi na Safu ya ushambuliaji.

Moja ya safu iliyokuwa tegemeo msimu jana ni safu ya kiungo cha Simba. Ilikuwa na wachezaji ambao walikuwa wanaibeba Simba. Wachezaji wake walikuwa wanyumbulifu na asilimia kubwa ya magoli ya Simba yalifungwa na viungo wa Simba lakini msimu huu timu iko kwenye uzani sawa.

Msimu jana mchezaji aliyemaliza ligi akiwa na magoli mengi ni Kichuya aliyekuwa na magoli 12 na aliyemfuata alikuwa Mavugo aliyekuwa na magoli 7. Lakini msimu huu ni tofauti kwa sababu mpaka sasa mchezaji anayeongoza kwa magoli ana magoli 18 na anayemfuata ana magoli 13.

Msimu jana hakukuwepo na idadi ya wachezaji wa eneo la ulinzi waliokuwa wanahusika kwenye magoli. Lakini msimu huu ni tofauti mfano Erasto Nyoni mpaka sasa hivi ametoa pasi 6 za mwisho na kufunga magoli 3, Asante Kwasi akiwa amefunga magoli 3 mpaka sasa tangu ajiunge na Simba.

Kwenye eneo la kujilinda wameimarika zaidi kwa sababu mpaka sasa hivi Simba wameruhusu magoli machache ukilinganisha na msimu jana. Msimu jana walifungwa magoli 17 na msimu huu mpaka sasa hivi wamefungwa magoli 13.

4: Mabadiliko ya kimfumo na mbinu katika kikosi cha Simba.

Hapana shaka huwezi kuitofautisha Simba ya msimu jana na msimu huu bila kulitazama hili.

Simba ya msimu jana ilikuwa timu ambayo inatumia mfumo mmoja tu wa 4-4-2, lakini msimu huu tangu Pierre Lenchantre na Masoud Djuma kuichukua timu imekuwa ikibadilika sana kimfumo, imekuwa ikitumia mifumo tofauti kulingana na mahitaji ya mechi husika. Mpaka sasa wamefanikiwa kutumia 4-4-2 (Diamond shape), 3-5-2, 4-3-3.

Wamekuwa wakitumia mbinu tofauti sana, mfano wanapokuwa wakikaba wanakuwa wengi kuanzia katikati ambapo wanakuwa wachezaji watatu (3) na nyuma wanakuwa na wachezaji 5 lakini wanapokuwa wanashambulia wanakuwa na wachezaji wawili pembeni, wawili eneo la mbele na mmoja nyuma ya washambuliaji wawili wa mbele.

Katika hatua hii ya mwishoni mwa ligi kuu, Simba imekuwa timu ambayo ikimuheshimu kila mpinzani ambaye anakutana naye. Wamekuwa na tahadhari kubwa kuanzia kwenye upangaji wa kikosi mpaka uwanjani. Mfano mechi kadhaa zilizopita wamekuwa wakichezesha wachezaji wengi wenye asili ya kujizuia zaidi, kwa mfano katika mechi ya jana waliwachezesha Erasto Nyoni, Mlipili, Kotei, Mkude, Asante Kwasi na Shomari Kapombe, hawa wote wana asili ya kuzuia na hii ni kuonesha tahadhari na kumheshimu mpinzani.

5: Uongozi wa Simba.

Msimu huu Simba inaonekana inapata huduma ambazo Yanga walikuwa wanazipata katika misimu mitatu iliyopita waliyofanikiwa kuchukua ubingwa, wachezaji wanapata mishahara kwa wakati na huduma zingine za msingi za mchezaji.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version