Timu zaanza kujichuja msimamo EPL
*Chelsea pointi nyingi, Arsenal ina ukuta mgumu
*Swansea juu kwa mabao, Southampton mkiani
Mzunguko wa tatu wa Ligi Kuu ya England (EPL) umemalizika, timu zikiwa zimejigawanywa kwa utofauti mkubwa.
Yapo makundi ya hadhi mbalimbali, ambapo timu inayoongoza ligi – Chelsea – imeshinda mechi zote na ya mwisho, Southampton, imeshindwa zote.
Lakini kati ya zote, Arsenal wanashikilia rekodi ya kuwa na ukuta mgumu zaidi, kwani hawajaruhusu hata bao moja kwenye mechi hizo tatu – mbili za ugenini na moja ya nyumbani Emirates.
Kwa ujumla, bado mabadiliko mengi yanatarajiwa, kwa sababu klabu ndio kwanza zimekamilisha usajili wa dakika za mwisho.
Yawezekana hata baadhi ya wachezaji walioingia katika muda wa lala salama kwenye klabu kadhaa, hawajaoneshwa mazingira yote, achilia mbali kupata namba.
Ingawa hivyo, kisheria na kikanuni licha ya usajili kukamilika Agosti 31, ligi iliingia mzunguko wa tatu siku iliyofuata, na pointi zinahesabika tangu mechi ya kwanza, iwe klabu ilikuwa imempata au haijampata nyota iliyomsaka kwa udi na uvumba.
Ni Reading na Sunderland zinazoweza kusema zinasubiri kujisogeza mbele kwenye msimamo, kwa vle zimecheza mechi mbili kwa sababu ya uwanja wa Sunderland – Stadium of Light ulijaa maji walipokuwa wacheze.
Mabingwa wa Ulaya, Chelsea wanaongoza ligi kwa kujikusanyia pointi tisa, imefunga mabao manane na kufungwa mawili.
Angalau wamebaki na heshima ya kuongoza ligi, baada ya kupata kipondo cha mabao 4-1 kutoka kwa Atletico Madrid katika mechi ya Super Cup la Ulaya iliyofanyika nchini Monaco. Yalikuwa maudhi kwao, na haijaeleweka watarudije kwenye ligi.
Timu ngeni katika ligi, Swansea iliyopanda msimu uliopita na kusifiwa kwa kutandaza soka safi inashika nafasi ya pili na mabao mengi ya kufunga kuliko nyingine zote.
Vijana hao wa kocha Mdanishi, Michael Laudrup wameanza kuogopewa, na walivuta macho ya wengi msimu uliopita baada ya kuingia kwa kujiamini EPL, chini ya Brendan Rodgers aliyehamia kuwanoa Liverpool sasa.
Timu hiyo inafungana kwa pointi na West Bromwich Albion na Manchester City – zote zikiwa zimeshinda mechi mbili na kutoka sare moja. West Brom wanaofundishwa na aliyekuwa kocha msaidizi wa Liverpool, Steve Clarke nao wameonesha uhai mkubwa, tofauti na walivyotarajiwa.
Ama kwa Manchester City, wameonekana kana kwamba kuna kitu wanakosa, ikiwa ni pamoja na kuonekana kuchoka katikati ya mchezo.
Bado hawajaonesha makeke yaliyowapa ubingwa, japokuwa kidogo kidogo Yaya Toure anaonekana ‘kufufuka’.
Manchester United, West Ham United na Everton zinafuatia kwa kufungana kwa pointi, baada ya matokeo ya aina yake mwishoni mwa wiki.
United ilishachukuliwa kwamba imeangukia pua ilipomenyana ugenini kwa Southampton, na hadi mpira unaelekea kumalizika walikuwa nyuma kwa mabao 2-1, wakiwa wametanguliwa pia kufungwa.
Mashabiki wa nyumbani katika Uwanja wa St. Mary’s walikuwa wakishangilia kusubiri dakika zikatike, lakini Sir Alex Ferguson aliangalia saa yake na kuwahimiza vijana.
Mashetani Wekundu walikuwa taabani, kwani walibanwa tangu kipindi cha kwanza, huku mfungaji wao moya Robin Van Persie akikosa penati baada ya kusawazisha bao la kwanza.
Alikuwa ni yeye RVP aliyenunuliwa kwa Pauni milioni 24 aliyesawazisha kosa kwa kufunga mabao mawili ya haraka haraka na kuwafanya United watoke kifua mbele na kusogea juu kwenye msimamo.
Southampton kwa upande mwingine, walipokea msiba huo kiume, kwa sababu umemaanisha wameshindwa mechi zote tatu na kufungwa idadi kubwa ya mabao – manane.
Ukweli ni kwamba walionesha kandanda safi, sawa na walivyofanya kwenye mechi nyingine dhidi ya Manchester City, ambapo waliambulia matokeo kama haya haya.
Arsenal, Wigan na Newcastle United wanafunga nusu ya kwanza ya juu, baada ya matokeo ya mwisho wa wiki, ambapo Arsenal waliwafunga Liverpool mabao 2-0 katika Uwanja wa Anfield, huku Newcastle wakitoka sare ya bao 1-1 na Aston Villa.
Baada ya kusubiriwa na kusemwa sana Arsene Wenger, hatimaye vijana wake waliibuka Jumapili hii na kuwacharaza watoto wa Anfield bila huruma na kufikisha pointi tano.
Walikuwa wachezaji wake wapya, Lukas Podolski na Santi Cazorla waliopeleka furaha kwa washabiki wa nyumbani, baada ya kumfunga kipa mzoefu Pepe Reina wa ‘The Reds’.
Kikubwa kilichoonekana katika mchezo huo ni Arsenal kushinda vita ya eneo la kiungo cha kati, kilichotawaliwa vyema na Mikel Arteta na Abou Diaby aliyerejea kwenye fomu, na alikuwa nyota wa mchezo.
Mbele yao, Wenger aliwaweka Cazorla, Podolski na mchezaji wa kimataifa wa Uingereza, Alex Oxlade-Chamberlain aliyetoka baadaye kumpisha Aaron Ramsey. Arsenal hawakuingia kwenye kichaa cha usajili wa dakika za mwisho, kubwa Wenger akisema anakiamini kikosi chake.
Liverpool walijitutumua, lakini jitihada za akina Luis Suarez, Fabio Borini na chipukizi Raheem Sterling ziliishia kwa nahodha Thomas Vermaleen au golikipa namba mbili, Mtaliano Vito Manone, huku Steven Gerrard akipotea kabisa dimbani.
Nusu ya pili ya chini katika msimamo wa ligi ina Fulham waliofungwa mabao 3-0 na West Ham Jumamosi; Stoke City na Sunderland.
Kadhalika wapo Tottenham Hotspurs walioibuka kidedea kwenye vita ya kusajili dakika za mwisho, ambapo hadi sasa hawajashinda mechi, zaidi ya kutoka sare mara mbili na kufungwa mechi moja.
Norwich wana pointi mbili tu, lakini wanaanza kuibuka walikoanguka siku ya kwanza, wakitarajiwa kufanya vizuri, ikiwa watashikilia uthabiti wao.
Kama unaweza kuliita eneo la hatari katika mechi hizi tatu tatu tu zilizochezwa, basi kuna waliomo.
Hao ni Reading (wamecheza mechi mbili), Aston Villa, Liverpool na QPR wamo humo, kwa sababu wana pointi moja tu.
Southampton watatakiwa kujitafakari upya, ili waondokane na hali ya kutokuwa na pointi yoyote, wakiwashikilia wote walio juu kwenye msimamo.
Ukiachilia mbali nafasi zinazoshikwa na timu kwenye msimamo, kwa ujumla mechi hizi 58 zilizokwishachezwa hadi sasa zinaonesha ni ligi ya kuvutia na kutarajia hatari kutoka kwa timu yoyote.