NYOTA wa mchezo wa kikapu wa Tanzania, anayecheza katika ligi ya NBA ya Marekani Hasheem Thabeet amesema viongozi wa mchezo huo nchini wasimtumie kama ngazi kwani mafanikio aliyoyapata ni juhudi zake binafsi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi usiku katika hafla iliyoandaliwa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Larry Andre, Hashim alisema ameshangazwa na viongozi wengi kumtumia yeye kama daraja kwa kujidai kuwa ndio waliomsaidia hadi hapo alipofikia wakati si kweli.
”Nadhani kuna watu wanataka kujinufaisha kwa kusema wamenisaidia kwa ajili ya uchaguzi wa chama chao, lakini si kweli. Nashangaa baadae wengine wamenifuata hadi Marekani na kudai kuwa wametumwa kunipongeza alisema.”
Hashim alikuwa akimaanisha baadhi ya viongozi waliomfuata huko kwa madai wametumwa na Rais Kikwete kwa kuwa amekuwa akimtembelea mara nyingi na kumpa moyo.
Akizungumzia kuhusu mchezo huo nchini, Hashim alisema mpira wa kikapu utachukua miaka mingi kufikia mafanikio kwa kuwa viongozi hawana nia ya kusaidia wachezaji.
”Watu wanaohusika ndio wanafanya mchezo huu ushindwe kuendelea kwani tangu niondoke nchini hadi sasa, hali ni ileile hakuna maendeleo, hata viwanja viko katika hali ileile,” alisema.
Alitahadharisha kuwa kutokana na hali hiyo itakuwa vigumu kwa Mtanzania mwingine kupata nafasi kama yake kwa hapa nchini bila ya kujipeleka mwenyewe kwa juhudi zake, ìlabda mmoja katika milioni moja sijui kama itatokea.”