MOJA ya mambo yanayorudisha nyuma maendeleo ya Watanzania katika nyanja nyingi za maisha ni kulazimishana wote tukubali utendaji wa mtu fulani katika nyanja fulani ni bora na usio na dosari hata moja kutokana na mtu huyo kujenga hali ya yeye kukubalika kwa jinsi alivyo au kwa mazuri yake kiutendaji.
Anayepata bahati kama hiyo huwa hakosolewi na anayemkosoa anaweza kutengwa na sehemu kubwa ya jamii kwa kuitwa mtu mwenye chuki binafsi kwa mtu huyo au kupakaziwa kuwa anatumiwa na wapinzani wa mtu huyo ama kutangazwa kuwa ana upeo mdogo wa mambo hata kama kukosoa kwake kuna mantiki katika upungufu alio nao mtu huyo anayekosolewa katika mipango ya utekelezaji.
Katika kuogopa kutengwa,kuzomewa au kuonekana wana upeo mdogo,Watanzania wengi huacha kuonyesha upungufu wa Mtanzania mwenzao kipenzi cha wengi na aghalabu Watanzania hao hujiingiza kwenye mkumbo wa kumsifu sana Mtanzania mwenzao bila kuonyesha upungufu wake.Hili lina dosari kubwa kwa maendeleo yetu kwa sababu mtu huyo kipenzi cha watu hatajua upungufu wake ama ataona yuko sahihi hata kwa yale anayotenda pasipo usahihi.Hapo ndipo tunaposhindwa kuendelea.
Mtanzania mmoja aliyepata bahati hiyo ni Rais wa TFF,Sir Leodgar Paul Chilla Tenga.Hakuna ubishi kaka yangu huyu amefanya kazi kubwa mno ya kuing’oa soka yetu pale ilipokwama tangu enzi ya wamu ya kwanza ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.Ni mwendawazimu tu ndiye atashindwa kuyaona mafanikio hayo.Amesimamia kupatikana kwa katiba isiyo na upenyo wa migogoro na migawanyiko ndani ya TFF,amerudisha uhusiano uliopotea kati ya TFF na serikali mpaka kuifanya serikali isaidie mambo mengi katika kuinua soka yetu kama kuwaleta na kuwalipa makocha,amejenga usimamizi mzuri wa fedha na kuwavutia wafadhili wengi walioingiza pesa nyingi kwa maendeleo ya soka yetu na ameimarisha uhusiano baina ya TFF na Chama cha soka cha Zanzibar,ZFA.
Muungano wa yote hayo umewezesha timu yetu ya Taifa kutinga kwenye fainali ya michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani(CHAN) itakayofanyika kati ya Februari 22 na Machi 8,2009 huko Ivory Coast.Kwa sasa,chini ya uongozi wa Tenga,nchi yetu imekuwa ya 99 kwa ubora wa viwango vya soka duniani toka nafasi ya 105 ambayo nayo tumeifikia baada ya kutoka nyuma au chini sana! Tenga na timu yake ya uongozi wa TFF uliopita walifanya kazi nzuri sana na wala hilo si la kubishaniwa.
Uzuri wa kazi hiyo ndiyo umemfanya apate bahati ya kukubalika kwa kila kitu.Ushahidi wa jambo hilo ulijitokeza katika uchaguzi uliopita wa TFF.Wadau wa soka waliogopa kabisa kupambana naye.Kila aliyetangaza nia ya kupambana naye alikatishwa tamaa vibaya sana kwa kuzingatia mafanikio ya Tenga.Ilibaki kidogo akose mpinzani kama si mwanamichezo Jamal Malinzi kujitokeza kupambana naye.Baada ya jitihada ya kumkatisha tamaa asigombee kushindikana(sizungumzii pingamizi alilowekewa na maamuzi yake) wengi walipakaza kwamba aliingia kwenye kinyang’anyiro hicho kama msanii tu kumsindikiza Tenga ili Tenga ashinde kwa kumshinda mtu mwingine,madai ambayo hayakuwa na mantiki.
Licha ya kueleza mipango mizuri ya utekelezaji wakati wa kampeni yake,Malinzi alikejeliwa vibaya sana kwa mipango hiyo kukosolewa na baadhi ya wadau kwa maneno makali na ya kivita vita si kwa sababu mipango hiyo aliyoinadi kwenye sera zake ilikuwa mibaya na isiyotekelezeka bali kwa sababu alimpinga Tenga,kipenzi cha watu,kiongozi aliyeongoza “bila dosari yoyote”! Ilifikia wakati hata Katibu Mkuu wa TFF,ambaye ni mwajiriwa wa Shirikisho hilo,Frederick Mwakalebela kupiga kampeni ya wazi wazi kwa Tenga wakati,kwa nafasi yake ya kazi,alipaswa asijibainishe kwa mgombea yoyote kwani yeyote,baada ya uchaguzi,angeweza kuwa kiongozi wa chombo kilichomwajiri! Alifanya hivyo kwa kuwataka wajumbe wamchague Tenga ili akawapokee,kama Rais wa TFF,wachezaji wa Taifa Stars walipokuwa wakirudi Tanzania toka Sudan walikoishinda timu ya Taifa ya nchi hiyo kwa magoli 2-1 na kutinga kwenye fainali za Ivory Coast kwa jumla ya magoli 5-2.
Ili tuzidi kuendelea kisoka,ni vizuri tujenge utamaduni wa kuelezana upungufu wa viongozi wetu wa soka kiutendaji na ki mpangilio wa mambo.Kufumbiana macho penye dosari,kwa sababu tunapendana sana au tunaikubali sana kazi nzuri ya mtu,hakutatusaidia kwenda mbele.Kuna suala la TFF kuwa na kitega uchumi.Hili alilizungumza Malinzi kama moja ya sera zake kwamba angejenga jengo la ghorofa 10 la kitega uchumi cha TFF.alizomewa sana na kuonekana kuwa mtu anayeota ndoto.Malinzi alikuwa sahihi sana kwa hili.Ndani ya miaka minne ya uongozi wa TFF,iliyopendwa na wadau wengi wa soka wakiwemo taasisi kubwa za fedha,FIFA na makampuni makubwa na tajiri ya kibiashara,isingeshindikana kuwepo kwa ujenzi wa kitega uchumi cha aina hiyo.Suala hapa lingekuwa mikakati ya ya kupata fedha hizo kwa njia mbalimbali ikiwemo mikopo na mgawanyo wa majukumu-hawa kuinua soka na hawa kusimamia mradi wa kitega uchumi.
Haipendezi na ni hatari kwa TFF kuishi kwa kutegemea msaada wa FIFA na pesa ya wafadhili inayolenga kwenye maeneo ya makubaliano tu.Ndiyo maana Rais wetu,Dr.Jakaya Mrisho Kikwete alipowapa changamoto ya kujiandaa kumlipa kocha,TFF walichanganyikiwa.Wasingefanya hivyo kama wangekuwa na vyanzo vyao vya uhakika vya mapato.Huo wa kutokuwa na vitega uchumi ni upungufu mkubwa wa TFF ya Tenga unaopaswa kuondolewa sasa.
Upungufu mwingine wa TFF hiyo ni ubovu wa kanuni zake.Mpaka sasa timu inayofanya kosa la kumchezesha mchezaji asiyestahili kikanuni kucheza inanyang’anywa ushindi wa mechi hiyo.Hata kama ilishinda uwanjani 4-0,ushindi huo wa pointi tatu wanapewa mezani wale wachovu wa uwanjani na magoli matatu hewa! Kwa hiyo,ghafla timu iliyofungwa 4-0 inageuka kuwa mshindi wa 3-0! Upungufu huo umeachwa licha ya wadau wachache kuupigia kelele kwamba ni afadhali mkosaji apunguziwe pointi alizonazo huku matokeo ya 4-0 ya mfano wangu yabaki hivyo hivyo.hata Malinzi alilinadi hilo kwenye sera zake.
Sababu ya kuwepo kwa upungufu huu ni kuwepo kwa upungufu mwingine kwenye taratibu za uendeshaji za TFF.Shirikisho hilo linachagua baadhi ya mambo ya kuwasiliana na vilabu ambavyo inavilea.Mengi ya mambo hayo ni yale ambayo ina maslahi nayo lakini mambo yenye maslahi kwa vilabu,TFF hiyo huvitegea vilabu ili viharibu au vikosee iviadhibu au vipate hasara.Kwa mfano,TFF haina utaratibu wa kuvijulisha vilabu kuhusu wachezaji wao wasiostahili kucheza mechi fulani kwa sababu fulani za kikanuni.Inaviacha vilabu vyenyewe vibebe jukumu hilo na vinapokosea ndipo linakuja suala la mpinzani mchovu kupewa pointi za mezani!
Kuna mfano wa hivi karibuni,Yanga imekuwa ikishughulikia kuwanunua wachezaji wawili wa timu ya Tusker ya Kenya,mabeki John Njoroge na Joseph Shikokoti huku TFF ikiona taratibu hizo zinaanza wakati dirisha dogo la usajili likiwa limeshafungwa wiki moja kabla! TFF ilipaswa iwazuie Yanga kuendelea na taratibu za kuwanunua wachezaji hao.Haikufanya hivyo mpaka klabu hiyo kuingia hasara nyingi kwenye biashara hiyo.Sasa ndiyo inawaambia wamekosea.Ilipaswa iwaeleze mapema kuhusu kosa hilo ili klabu hiyo isiingie hasara ya bure.Kauli yangu hii haifuti kosa la Yanga wenyewe katika biashara hii lakini TFF,kama mlezi,ilipaswa iwaambie inaowalea kwamba huko mnakoenda siko.Huu ni upungufu mmoja mkubwa wa TFF ya Tenga kuwa mbali na vilabu kwa baadhi ya mambo muhimu.
Upungufu mwingine wa TFF ya Tenga ni kuacha baadhi ya kamati zake za maamuzi kusikiliza kesi za wadau mbalimbali wa soka bila kuwapa nafasi ya kujitetea.Kilichopo ni maamuzi kutolewa kwa kuangalia tu taarifa ya mwamuzi na kamishna bila mshtakiwa kujieleza na bila kuwepo kwa ushahidi wa video,kwa kesi za matukio ya uwanjani.Kimfumo,mwamuzi anakuwa upande mmoja wa kesi husika.Kwa mfano,anapotoa kadi nyekundu kwa mchezaji kwa madai ya kumpiga mwenzake,taarifa yake itakuwa hivyo na ikitokea mtu akadai yule mchezji hakumpiga mwenzake bali yeye ndiye alipigwa halafu aliyepiga ndiya alianguka chini na kulalamika kuwa amepigwa,lazima mwamuzi atatetea taarifa yake ili aonekane hakukkosea.Kukosekana kwa usikilizaji wa haki wa kesi wa kusikiliza pande zote na kutokutumika ushahidi wa video ni upungufu mkubwa wa taratibu za maamuzi ya kesi za TFF.
TFF hii haikufanya jambo lolote la kuonekana la kuimarisha soka la vijana.Haijakuwa na mkakati wa kushawishi serikali ianzishe shule maalum za michezo ikiwemo soka ambapo TFF ingekuwa mbia katika uendeshaji wa shule hizo.Angalau tu,mipango kama huo ingekuwemo kwenye makaratasi ili tujue kwamba iko mbioni kutekelezwa.
Upungufu wa TFF ya Tenga unaweza kuwa mwingi lakini naomba kumalizia na upungufu wa kutokuwepo kwa tovuti ya TFF ambapo pia mpaka sasa taarifa muhimu za soka zinazohusu timu zetu zote ikiwemo ya Taifa na wachezaji wetu kama idadi ya mechi walizocheza wakianza,walizocheza wakiingia baadaye,magoli waliyofunga,kadi walizoonyeshwa na kadhalika hazijaanza kutunzwa na siku zinaenda.Muulize kijana Jerry Tegete amecheza mechi ngapi akiwa Yanga na ngapi akiwa timu ya Taifa,amefunga magoli mangapi na mechi zipi alianza na zipi aliingia baadaye,atashindwa kukupa majibu ya uhakika ingawa hana muda mrefu akichezea timu hizo.
Kama nilivyosema karibu ya mwisho wa makala hii,kunaweza kuwa na upungufu zaidi ya huo lakini huu unatosha kwa leo kwa kujadiliwa.Hata hivyo,napenda kurudia kusema kwamba TFF hii imefanya mambo makubwa sana kwenye maendeleo ya soka yetu.Upungufu ni suala la kimaumbile,hivyo si ajabu kwake kuwa na upungufu kama mtu yeyote asivyoweza kuepuka kuwa na upungufu.Lakini tusioneane haya au tusione kwamba ni kashfa kuelezana upungufu kwa ajili ya kuuondoa kwa maendeleo yetu.